Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa nami kuchangia kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nina masuala kadhaa kama manne hivi ambayo naenda kugusia.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia, kwa masikitiko kabisa, nianze kujielekeza kwa kutokutekelezwa kwa bajeti ambazo tunazipitisha kwenye Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Fungu Na. 65 ambalo tulitenga takribani shilingi bilioni 26.6 na tukazielekeza kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Wizara ambayo ni muhimu kabisa, lakini cha kusikitisha, mpaka kufikia Februari, 2023 zilikuwa zimepelekwa shilingi bilioni 5.5 tu kama asilimia 22 tu. Tulitenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kukarabati na kujenga vyuo vya watu wenye ulemavu, kundi ambalo ni maalumu kabisa, lakini mpaka leo hata senti moja haijawahi kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha hizo ambazo tulizitenga, pia ilikuwa ni kwa ajili ya kwenda kukuza kazi ya staha nchini, programu ya kukuza ujuzi, Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19, Mfuko wa Maendeleo ya vijana, vyote hivi ni muhimu, lakini bajeti inatekelezwa kwa asilimia 22 tu.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi, mwaka wa fedha 2022/2023 waliomba shilingi bilioni 26.6; mwaka huu ambao wanaenda kutekeleza mambo hayo hayo, wameomba shilingi bilioni 14 kama fedha za maendeleo. Wametekeleza below, lakini pia mwaka huu wa fedha wameomba chini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tunaomba, Serikali ijielekeze hii Wizara ni muhimu sana. Kila mwaka tafiti zinaonesha vijana takribani 900,000 wanaingia kwenye soko la ajira, lakini ni vijana kati ya 50,000 na 60,000 tu wanaopata ajira. Sasa tunaacha Watanzania zaidi ya 800,000 plus bila ajira. Kwa hiyo, hii ni Wizara nyeti sana ambayo ingeweza kuwekeza fedha ikahakikisha ina-absorb vijana aidha kwenye sekta zilizo rasmi na zisizo rasmi, na hiyo ni pamoja na makundi ya watu wenye ulemavu kama nilivyosema.

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ni kuhusiana na utawala bora. Waziri Mkuu ameainisha jinsi nchi yetu inavyoendelea na utawala bora, nami kwa kweli napenda kutumia fursa hii kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwanza kuirejeshea nchi yetu uanachama kwenye OGP (Open Government Partnership) ambayo ilikuwa imeondolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, tulimwona Mheshimiwa Rais anatekeleza kwa vitendo. Juzi aliposema kwa machungu kabisa kwamba anakemea ubadhilifu ambao ulikuwa inflated katika manunuzi ya ndege Dola milioni 49 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 117 za Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, nilijaribu kufuatilia, ile ndege ilikuwa inunuliwe kwa dola milioni 92 ambayo ni sawa sawa na fedha za Kitanzania shilingi bilioni 220. Zikawa zimelipwa advance payment dola milioni 55, zikabaki dola milioni 32. Sasa kweli nchi yetu ilivyo sasa hivi, tuna bajeti iyojitegemea, tunategemea wahisani, mikopo na kila kitu. Balance imebaki ya dola 32 imekuwa inflated kwa dola milioni 86, ongezekeo la dola milioni 49.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nasema nampongeza Mheshimiwa Rais kwanza kwa kuwa muwazi; pili, kwa kukemea uwajibikaji, pale aliposema, wale wote ambao walikuwa wanahusika na ku-invoice hizi amount, waweze kuwajibika.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Waziri Mkuu ndio msimamizi wa mambo yote ya Serikalini, Bunge lako Tukufu tungependa, kwanza aje atueleze mpaka sasa hivi, na baada ya ile statement ya Mheshimiwa Rais; kama Bunge lazima tuisimamie na kuishauri Serikali, hizi fedha ni nyingi sana. Tungesema tuzielekeze kwenye madarasa, tungeweza kujenga zaidi ya madarasa 5,800 Tanzania. Leo tusingekuwa tunaona watoto wanalundikana. Juzi nimeona kule Uvinza, Kigoma zaidi ya watoto 2000 wanalundikana kwenye darasa.

Mheshimiwa Spika, tungesema tuzielekeze kwenye ujenzi wa vituo vya afya hizi ambazo wamezi-inflate 117 laiti Rais asingeziona zilikuwa zinaenda kupotea ambazo zingeweza kujenga vituo vya afya 234 tuka-save maisha ya Watanzania ambao wanakufa kwa kukosa huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, tungesema tuzielekeze kwenye kujenga nyumba za walimu, waache kupanga mbali, mvua zikinyesha miundombinu mibaya hawafiki shuleni, watoto wanashindwa kupata elimu, tungejenga nyumba za walimu (ngoja nifanye hesabu zangu) takribani elfu mbili na kitu, kwa sababu tuseme wao average cost ni kama Shilingi milioni 40 hivi. Haikubaliki, haiingii akilini, tutakuwa Taifa la ajabu kabisa kuruhusu watendaji hawa kuendelea kukaa na kubadilisha hizi.

Mheshimiwa Spika, nikawa najiuliza, probably zimekuwa zikitokea huko nyuma kwa haya manunuzi ya ndege, maana yake najua ndege zilipelekwa Ikulu. Kama haya yalikuwa yanatokea wana-inflate hivi, Taifa letu limeweza kudidimizwa kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha, Pay Master General anatoka kwake na kila siku anavaa hiyo tai ya Tanzania, na hata leo amevaa kuonesha uzalendo. Tunataka kujua haya yote yanayotokea. Inaumiza sana! Haya yote yanayotokea, imeonekana tu hii. Ni mangapi yanatokea huko ambayo yanapoteza fedha za Watanzania masikini walipa kodi ambao wangeweza kuelekezwa na tukafanya mambo makubwa sana kwenye Taifa letu? Tungechukua hata hizi fedha tukawekeza kwenye utalii wa michezo, tungejenga viwanja vingi sana vya kisasa Tanzania, hata Mataifa mengine yakawa yanakuja tu-host michezo hapa, uchumi wetu ungekuwa maradufu.

Mheshimiwa Spika, tungechukua hii fedha ambayo isingeonekana inapotea, tukawekeza kwenye utalii hata utalii wa mikutano, tungepata fedha nyingi sana. Sasa nataka waiokoe hii Serikali. Waziri Mkuu anapokuja hapa ku-windup hapa watueleze bayana, mostly watendaji kama kweli wameshapisha kama Rais alivyosema. Hata wakipisha, lazima tuangalie the source of it ili tuweze kukomesha haya mambo ya ubadhirifu wa fedha Tanzania once and for all.

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nataka nigusie, Waziri Mkuu ameonesha hapa kwa kina kabisa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, muda wangu.

SPIKA: Bahati mbaya muda wa taarifa huwa unatumika wa yule anayechangia. Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji, amenitaja kwa jina, akataja na tai na hakusema kwamba hivi vitu vinapita vingapi? Nilitaka nimpe taarifa kwamba, utaratibu wa malipo uliowekwa hapa nchini, na niwatoe hofu Watanzania, ni utaratibu imara sana. Hivi vitu haviwezi vikapita pita ovyo ovyo.

Mheshimiwa Spika, moja, hakuna malipo ya kila mwezi yanayoweza kufanyika bila Mheshimiwa Rais kujua. Kwa hiyo, la kwanza, mahitaji yote ya Wizara zote yanapokuja Wizara ya Fedha, tunayapitia tunawianisha na mapato, tunayaombea ridhaa kwa Mheshimiwa Rais. Yakishapata ridhaa ndipo yanakwenda kulipwa.

Mheshimiwa Spika, hata hilo la ndege analolisema, yalipoletwa mahitaji, Wizara ya Fedha tuliona kwamba limekuja lina ongezeko ambalo kama ni la kimkataba lazima tupate ushauri wa Mwanasheria Mkuu. Kama ni la kimkataba na lina mzozo kwamba linabadilika kutoka bei iliyokuwepo ni lazima tupoate maoni ya Mwanasheria Mkuu. Hatukuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, vile vile kama lina mkataba, linahusisha variation, lazima tujue waliokaa na kuongeza hiyo variation mpaka ikubalike. Sasa haya yote hayakuwepo, tukakataa malipo hayo. Kwa utaratibu kwa kimalipo, ilibidi tutoe taarifa pia kwa mamlaka ambayo ndiyo inaidhinisha, na mamlaka ikachukua hatua ya kusema hayo malipo ya aina hiyo yasilipwe. Kwa hiyo, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wale ambao wamefanya huo utaratibu wa mwanzo ambao ulihusisha mpaka hizo hatua zikaweza kufika kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwatoe hofu Watanzania, mifumo ya malipo iko imara, na ndiyo maana tunaongeza nguvu kupambana kule site ambako fedha zinaenda, ndiyo maana tumemwongezea fedha CAG, na Mkaguzi wa Ndani. Mheshimiwa Rais akaelekeza uwazi, ambapo ni kitendo kikubwa Mheshimiwa Rais amekifanya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, angeamua kuweka usiri akaamua kutokuongeza fedha kwa CAG, Bunge ambalo CAG ndiyo jicho lake msingeweza kutambua tunayoshauri. Kwa hiyo, tumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Niwahakikishie Watanzania kwamba hazina yao iko salama na iko mikono salama. Mimi umasikini wa Watanzania Mheshimiwa Ester sijausoma kwenye vitabu, nauelewa na siwezi kupindisha fedha nyingi za aina hiyo wakati madaarsa yana hali hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa hiyo.

SPIKA: Mheshimiwa Ester Matiko, subiri kidogo. Kwanza unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha?

MHE. ESTHER N MATIKO: Mheshimiwa Spika, nitakuwa sijitendei haki. Siipokei.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ametoa maelezo yake, nimesema siipokei. Sasa haya ni malipo makubwa ambayo yanaenda mpaka yanamfikia Rais. Kuna malipo mengine madogo ambayo yanapotea ambayo hayamfikii Mheshimiwa Rais. Kama Taifa, Watendaji Serikalini ambao wamepata dhamana lazima waangalie kwa umakini kabisa. Hili hapa amelielezea vizuri, lakini hayo mengine ambayo yanapita yanaleta ubadhirifu lazima yakemewe. Hii ni alarming, tena alarming kubwa sana. Kama watu hawatakuwa na guts za ku-inflate 49 million dollars, you are talking about 117 billion shillings, it is not a joke! Yaani anapitisha bila uoga mpaka yanaenda kwa Rais. Rais! Mh!

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nizungumzie Mheshimiwa Waziri mkuu ameonyesha hapa na nakubali kabisa, tuwekeze kwenye maendeleo ya watu kwa maana ujenzi wa miundombinu mashule, hospitali, Vituo vya Afya na wewe umesema hapa asubuhi vizuri kabisa. Lakini kama nchi, kama taifa hatujaweza kuwekeza na kuweka jicho kwenye rasilimaliwatu unaweza ukajenga majengo ya kutosha usipokuwa na rasilimaliwatu ya kuendana na majengo uliyoyajenga ni kama vile unafanya kitu hakuna.

Mheshimiwa Spika, ninachukua mfano tu wa kwenye Elimu, kuna upungufu mkubwa sana wa Walimu hasa masomo ya Sayansi, Walimu kwa mfano shule ya msingi kuna upungufu wa zaidi ya asilimia 45. Walimu shule za sekondari kuna upungufu wa zaidi ya 51 na hiyo inakuja ku-reflect kwenye matokeo yao mathalani matokeo ya form two ambayo tuliyapigia kelele sana, ufaulu wao kwenye somo la hesabu unaonyesha upungufu wa Walimu ni takribani asilimia 71 failure yao ilikuwa asilimia 83 unaweza ukaona zinakuwa directly related yaani upungufu wa walimu asilimia 71 una- reflect wanafunzi kufeli kwa asilimia 83. Ukija somo la Physics upungufu wa walimu asilimia 77 Wanafunzi wakafeli kwa asilimia 82, ukija somo la Chemistry upungufu wa Walimu asilimia 64 Wanafunzi wakafeli kwa asilimia 67. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unafikiri private sekta wanafaulu kwa ajili ya nini? Miundombinu plus walimu, input zote za ufundishaji lazima ziwepo, tutajenga majengo, majengo tutajenga ni physical things vinaonekana vya tangible wananchi wataona, watatupigia makofi we are doing good job but in reality, we are killing education of this country, ahsante. (Makofi)