Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, napenda kushukuru kupata nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa napenda nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuliongoza Taifa hili la Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiofichika, ndani ya kipindi cha miaka miwili ya kiongozi wetu Mama Samia, mambo makubwa sana yamefanyika katika nyanja mbalimbali katika kuendeleza nchi yetu. Mimi binafsi nianzie katika suala la miundombinu.

Mheshimiwa Spika, katika suala la miundombinu Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake wamejitahidi kwa hatua kubwa sana, nikichukulia kwangu kwa mfano Bagamoyo, ndani ya miaka miwili ya Mama Samia tumepata zaidi ya shilingi bilioni moja katika ujenzi wa barabara zetu, ukiachilia mbali barabara na taa za barabarani sasa hivi zinawaka, kwa hiyo Bagamoyo inawaka na Bagamoyo inang’ara, hizi zote ni juhudi za Mheshimiwa Rais wetu kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la nishati. Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake amezungumzia suala la nishati na amezungumza karibuni sasa hivi asilimia
76.7 ya nishati tuko vizuri lakini bado kuna changamoto nyingi sana katika suala la nishati na hasa katika suala la umeme. Katika suala la umeme bado vijiji vingi pamoja na vitongoji vingi havijapata umeme. Ukienda sehemu mbalimbali bado utakuta nguzo zimewekwa lakini huduma ya umeme bado katika usambazaji wake. Suala la nishati ni muhimu sana katika nchi, wananchi wanapopata umeme ndipo maendeleo yanapopatikana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo bado tunanishati ya kupikia, nishati ya kupikia bado Tanzania tuna changamoto kubwa sana. Watanzania wengi sana asilimia kubwa wanatumia mkaa, hii inasababisha misitu yetu pamoja na vyanzo vyetu vya maji kuharibiwa kutokana na watu kukata misitu, hii kwa kweli ni changamoto kubwa sana. Hivyo basi, nilikuwa naishauri Serikali katika hili suala la nishati ya kupikia waweke mipango madhubuti kabisa kama walivyofanya ruzuku katika mafuta, watoe ruzuku katika gesi, watoe ruzuku katika vifaa vinavyoshughulika na majiko ya gesi ili Watanzania wengi waweze kupata gesi.

Mheshimiwa Spika, hakuna ubaya wowote kusema kwamba mwezi huu tunatoa ruzuku ya mafuta, mwezi huu tutatoa ruzuku katika gesi ya kupikia na vifaa vya gesi kama majiko pamoja na vifaa vinginevyo ili Watanzania wengi waweze kupata nafuu ya kupika kwa kutumia nishati hii ya gesi ili kuepuka kukata misitu hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda sana niipongeze Serikali ya Mama Samia ni suala zima la bandari. Suala la bandari Mheshimiwa Rais amejitahidi sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu jana katika hotuba yake amezungumzia kuna bandari ya nchi kavu ambayo iko maeneo ya Kwala, hii bandari ujenzi wake umefikia asilimia 87 itakapokamilika bandari hii itasaidia sana kukuza uchumi wa nchi. Kuna faida nyingi za bandari ile ikimalizika, hata msongamano wa magari makubwa kutoka Vigwazo kuelekea Dar es Salaam, utapungua kwa kiasi kikubwa sana, kwa hiyo watu wengi watafanya shughuli zao kwa wepesi zaidi.

Mheshimiwa Spika, tuzungumzie sula la Bandari ya Bagamoyo. Nimefarijika sana jana katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuzungumzia bandari ya Bagamoyo. Kwa kweli sasa imefika wakati hii bandari itakapojengwa uchumi wa Taifa utakua.

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto ambazo zinaukabili ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. Bandari ya Bagamoyo inajengwa katika Kata ya Zinga sambamba na ujenzi wa bandari, iliunganishwa ujenzi wa bandari fidia zile pamoja na kongani za biashara - EPZA mpaka sasa mwaka wa 13 wananchi wa Kata ya Zinga hawajui nini wafanye kutokana na fidia ambazo hawajalipwa na hivyo wanasikia kuwa ujenzi wa bandari unakuja na wao bado hawajalipwa fidia zao, kwa hiyo ninaiomba Serikali ihakikishe kwamba inafanya juhudi za maksudi kabisa wananchi wa Zinga waweze kupata fidia zao ili kuwe nafuu zaidi katika suala zima la ujenzi huu wa bandari.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la maji, ninaipongeza Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika miradi ya maji. Mimi kwangu kule Bagamoyo watu wengi karibia asilimia 87 wanapata maji katika Jimbo langu, lakini kuna baadhi ya sehemu zina changamoto kubwa ya maji hasa katika kata mbili, Kata ya Makurunge pamoja na Kata ya Fukayosi, hizi Kata zina changamoto kubwa sana ya maji, inafikia hatua wananchi wanakaa mpaka mwezi mzima maji ya bomba hayatoki, unapowauliza wenzetu wanaoshughulika na masuala ya maji watakwambia kwamba mitambo imekorofisha, umeme mdogo. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali ijitahidi kabisa kuhakikisha kwamba suala la upatikanaji wa maji katika hizi Kata na maeneo yote ambayo hayana maji katika nchi hii yanakuwa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi sasa katika suala la kilimo, ninaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mama Samia katika suala zima la kilimo. Ule mpango wa Serikali kuandaa vijana ili waende sasa wakalime ni jambo la msingi sana, lakini naomba kadri siku zinavyokwenda waongeze idadi ya vijana katika suala zima la kilimo. Kwa sababu tumeangalia takwimu ambazo zimechukuliwa mwaka huu, kila Wilaya imepata vijana Wanne. Hivi kweli kila Wilaya ikipata vijana Wanne kutakuwa na maendeleo gani katika suala la kilimo? At least tuongeze wigo sasa kuhakikisha kwamba vijana wengi wanachukuliwa kutoka katika Wilaya zetu kwenda kushiriki katika mafunzo waweze kupata tija katika hayo mafunzo ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache ninashukuru sana, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)