Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai na afya, nitumie nafasi hii kwa kweli kuwatakia Wakristo ambao wako katika mfungo wa kwaresma na Waislamu ambao wako katika mfungo wa Ramadhani, heri ya funga na funga hii itusaidie katika kuleta baraka katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu nitumie nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, kipenzi chetu na mfano wa kuigwa wa wanawake wa Kiafrika katika uongozi bora na wote wanaomsaidia akiwemo Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na wengine wote katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine hata tunapofika mahala tukasimama na kushauri na kukosoa baadhi ya mambo hatumaanishi kwamba kazi haifanyiki, kazi iliyofanyika ni kubwa sana, tunamshukuru sana Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niweke salaam za pekee za shukrani kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na zaidi ya yote kwa mahusiano mazuri na uchapakazi mzuri, mahusiano mazuri na sisi Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watumishi wengine wote wa Umma. Mheshimiwa Waziri Mkuu wewe ni mtu wa mfano wa kuigwa katika tabia njema na mahusiano mema, tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, pongezi hizo ziende sambamba na kupongeza hatua inayochukuliwa na ofisi ya Waziri Mkuu katika kusaidia tatizo la ajira kwa vijana nchini kwa kutoa mafunzo kwa vijana kwa program maalum ambayo inatolewa VETA inayoitwa Programu ya Waziri Mkuu. Nimetembelea Chuo cha VETA - Kigoma, nimewaona vijana waliotoka pale awamu ya kwanza, nimewaona wa awamu ya pili na sasa tunasubiri awamu ya tau. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yako tunawapongeza. Program hii endeleeni nayo ni ya manufaa katika kuwapa vijana ujuzi wa kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo ni vizuri ieleweke kwamba kutokana na hali zetu za maisha na hasa familia zingine ambazo ni duni wanazotoka vijana hawa, ni vizuri kuweka utaratibu wa baadhi ya vijana wanapotoka pale kupewa vitendea kazi ili waende wakaanze kujiajiri moja kwa moja. Kumfundisha mtu useremala bila kuwa na vifaa vya useremala ni kweli umempa ujuzi lakini umempa vilevile mzigo katika suala la kujiajiri. Kama inashindikana kufanya hivyo kwa kijana mmoja mmoja tufanye hata kwa vikundi, tutoe fedha za Serikali mbona zipo nyingi zinapotea na nyingine tutaanza kuzijadili hivi karibuni, tupeleke kwa hawa vijana wetu wajiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Kigoma nilipotembelea VETA nimeona jambo la ajabu sana, kuna kijana mmoja anaitwa Zuberi Abdallah Ismail, huyo kijana ni mwanafunzi pale, kwa ubunifu ameweza kutengeneza redio, anarusha matangazo yeye mwenyewe katika eneo dogo, yule kijana akichukuliwa akaendelezwa anaweza akafanya mambo makubwa sana.

Nilimuuliza wewe ulipataje mawazo haya akasema nime- search kwenye redio nikaona frequency ambayo ukiweka haipati matangazo yoyote, yaani hakuna Radio Station yoyote nikaitumia frequency hiyo akatumia 87.5 akaanza kurusha matangazo yake huko Ujiji na yanakwenda umbali wa mita kama 200. Unaona sasa hawa ndiyo vijana wanaweza. Transmission system kaitengeneza mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, tukifika mahala tukakuza vipaji hivi tunaweza kutengeneza magari, pikipiki, lakini hii imekuwa ni nchi ambayo mpaka forklift ya kubebea mizigo bandarini tunaagiza kutoka nje na sisi tunao watu wana akili wamezaliwa na wanawake kama walivyozaliwa hao wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni vitambulisho vya Taifa - NIDA. Hapa ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize vizuri pamoja na kwamba ninaona Mheshimiwa Waziri Ummy anamsemesha sana, nataka niseme kwamba katika jambo ambalo tunaweza tukadaiwa na Watanzania na tukakosa maelezo ya kutosha ni vitambulisho vya NIDA. Ninataka niseme kwamba anayefikiria vitambulisho vya NIDA vinatolewa kwa hiari ya Serikali siyo sahihi asome Ilani ya Uchaguzi Ibara ya 105(q) kinasema hivi: ‘‘Kuwezesha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, kuendelea kutambua, kusajiri na kutoa vitambulisho vya Taifa kwa Raia wa Tanzania, Wageni Wakazi, kwa kuhakikisha watu wote wenye sifa ya kusajiliwa wanapata utambulisho wa Taifa, wanasajiliwa na kupatiwa vitambulisho na Taasisi zote za Umma na binafsi zinaunganishwa na mfumo wa NIDA’’.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo limeahidiwa na CCM kwenye mikutano ya kampeni, hii ni ahadi kuhakikisha kila mtu. Leo hii Mkoa wa Kigoma kati ya watu waliochakatwa kuomba vitambulisho watu 964,967 ni watu 582,683 sawa na asilimia 60.4 tu ndiyo waliopata vitambulisho, haiwezekani! Leo tunazungumza suala la vitambulisho vya Taifa leo ni mwaka wa 12 tulianza mwaka 2011 na nataka ieleweke na Serikali hapa ielewe vizuri kwamba inakwamisha maendeleo ya watu mengi sana kwa kuwanyima vitambulisho vya Taifa.

Mheshimiwa Spika, wapo watu ambao wanataka kuingiza umeme majumbani kwao wanaombwa kadi za NIDA, wapo watu wanataka kuingiza maji, wapo watu wanataka kuingia katika mfumo wa TRA, wapo watu wanataka kuomba passport za kusafiria kwenda kwenye masuala mbalimbali ya maisha yao lakini wanakwama kwa sababu ya vitambulisho vya NIDA. Na hili ningekuomba sana Mheshimiwa ni kwa sababu nimelisema katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo Msimamizi Mkuu wa Serikali na tunakujua Mheshimiwa Waziri Mkuu wewe ni mtu makini na mahiri, tukuombe sana kama hapa katikati labda ulitikisika tikisika na vineno vya wahuni usijaali simama imara fanya kazi, umeaminiwa! Katika Tanzania hii ni historia Waziri Mkuu mmoja kuaminiwa na Marais wawili, chapa kazi hakuna kurudi nyuma simamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ninataka kuzungumzia usafiri wa mabasi yaendayo Mikoani. Kuna watu wangu wa Kigoma wanapata adha isiyokuwa na sababu. Sababu kubwa inayozungumzwa ni tatizo la usalama. Watu wanakuja kituo cha basi cha Magufuli wanalala pale ili Saa 12 asubuhi waondoke maana mtu hawezi kutoka Mbagala akaja akawahi basi, analala pale anatoka hapo anakwenda akifika Kaliua Tabora analala, kesho yake ndiyo afike Kigoma. Ninaishauri Serikali, jambo jepesi kabisa kwamba wekeni utaratibu wa kiusalama, lakini kwa sababu eneo lile la Kigoma ambalo lilikuwa na Wakimbizi ndiyo lina tatizo la usalama, mabasi ya Kigoma yaondoke saa Nne usiku Dar es Salaam, yapite maeneo yote haya yafike eneo lile la Kigoma wanapita, siyo watu wanakuja kulala stendi ya Magufuli, wanakwenda tena kulala stendi ya Kaliua!

Mheshimiwa Spika, kadri tunapofika mahala tukawapotezea watu muda ndiyo tunavyofanya shughuli za uzalishaji kuchelewa. Nchi zilizoendelea watu wanasafiri usiku, asubuhi wanafika mahala wanafanya shughuli zingine za kimaendeleo.ninaiomba sana Serikali…

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, taarifa!

T A A R I F A

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, nilitaka ninampa taarifa Mheshimiwa mzungumzaji ni kwamba yale mabasi kulala Kaliua yanaukuza uchumi wa Wilaya ya Kaliua ni hilo tu,, ahsante. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda unaipokea taarifa hiyo>

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa naipokea lakini kila mafanikio yana changamoto, kwa hiyo hayo mafanikio anayoyapata yeye ni changamoto kwangu, kwa hiyo tu-balance, ameshavuna nyingi sana za watu wa Kigoma, sasa awaache na wenyewe waendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)