Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Azimio hili muhimu sana la kumpongeza Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumza kwa upana kuhusu faida za kukuza demokrasia nchini, lakini nitajielekeza katika ukuzaji wa demokrasia ya kiuchumi. Hata hivyo kabla sijaenda mbali, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tumuombee sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumza hapa kwa mifano tu na mwishoni nitataja kule Hai mambo ambayo tumeyaona. Mheshimiwa Rais miradi yote mikubwa ambayo mtangulizi wake alianza sasa hivi kazi inaendelea. Bwawa la Mwalimu Nyerere, Madaraja, kila shughuli ambayo ilikuwa imeanzishwa inaendelea, Mheshimiwa Rais anafanya kazi vizuri sana. Shirika la Ndege, ndege zimeendelea kununuliwa hakuna kilichosimama. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo kwenye demokrasia. Hili tunaloliona Mheshimiwa Rais anapaswa kupongezwa kwa dhati. Niseme hapa wenzetu wa Upinzani waelewe Mheshimiwa Rais ana dhati ya kweli na wao wapokee dhati hiyo kwa kweli. Sio tunazungumza kwenye level ya Taifa tunaridhiana halafu huku chini watu wanaenda kufanya vitu vya tofauti. Tuwe na dhati na tuwe wakweli kutekeleza demokrasia ya kweli. Nalisema hili kwa sababu kuna unafiki ndani yake na fitina ndani yake. Huku wanazungumza lingine na wakifika huku chini wanazungumza lingine.

Mheshimiwa Spika, natoka Jimbo la Hai, tunafahamu changamoto zinazotokana na tatizo la kutokuwa na demokrasia ya kweli. Kwa hiyo kama kuna watu ambao wana neema na wamefurahi kwa kweli ni watu wanatoka Jimbo la Hai kwa sababu tunafahamu changamoto zinazotokana na matatizo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunafurahi kule hai miradi kedekede inatekelezwa. Tulikuwa na tatizo la maji, pale Boma Ng’ombe tumeletewa Bilioni 3.3 kazi inaendelea. Miaka mingi tulikuwa hatuna barabara, sasa zinachongwa, vituo vya afya vitano vinajengwa, hospitali ya wilaya tumeletewa pale bilioni 3.1, kazi inaendelea na hivi juzi tumeletewa fedha nyingine za madarasa. Haya yote ni mafanikio ya kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais. Tuna kila sababu ya kulinda kazi hizi kubwa anazozifanya kwa dhati.

Mheshimiwa Spika, niseme maeneo mengi yameguswa. Pale kwetu tulikuwa na kiwanda cha Machine Tools Kilimanjaro leo kinafanya kazi, kimekufa kwa miaka kumi na tatu, haya ni mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais wetu anayafanya. Hata hivyo, niseme wenzangu wamezungumza hapa, Profesa amezungumza akasema wale ambao wanamwangusha Mheshimiwa Rais tuwaonyeshe mlango. Hata hivyo, nachelea kusema tuwaoneshe mlango, kwani hawaoni mlango? Mlango si upo? Kesho ita press pale, sema bwana mimi naachia ngazi, nimekuwa kikwazo kwa nchi hii, waingie wengine wala hawahitaji kusubiri.

Mheshimiwa Spika, nawashauri wale walioko Serikalini na ameona Mheshimiwa Rais amezungumza kwa lugha ile, Mama yetu tunaempenda sana na yeye ndiyo mzigo humu ndani, si aende na kuita Waandishi wa Habari sema nalichota bao na tugawane? Tuachie ngazi waingie wengine wafanye kazi wasimkwaze Mama yetu.

Mheshimiwa Spika, niseme, wewe uturuhusu sasa hili Bunge linalokuja tufanye nao kazi, wale wanaomwangusha Mheshimiwa Rais ili Azimio hili liwe na meno ni lazima wale wanaomvuta nyuma Mheshimiwa Rais tushushughulike nao. Walioko huku ndani na hata walioko kule nje ambao wanafanya kinyume na yale ambayo yako kwenye maridhiano.

Mheshimiwa Spika, nimeeleza hapa hawa walioko hapa ndani wanafanya na sisi tutashugulika nao, lakini pia walioko kule nje, hata wenzetu walioko upinzani wajue tunashughulika nao kwa sababu hatuna mzaha kwenye hili, tunataka maendeleo. Vile vile wachukue mfano mzuri, kama kuna maridhiano ndani ya Serikali waende na maridhiano mazuri kwenye vyama vyao. Huko kwenye vyama vyao pia kwenye upinzani kuna uonevu mkubwa mno. Waende na wao wakatekeleze demokrasia kama hatua ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Huwezi kuhubiri leo maridhiano halafu wewe kwenye Chama chako unaumiza watu, unakandamiza watu, wewe ni mfalme, unaishi unavyotaka, hapana. Waheshimu katiba za vyama vyao na waheshimu taratibu walizojiwekea kwenye vyama vyao ili nchi hii iwe na amani pande zote. Watanzania tufurahi kwenye nchi yetu, tuishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na mwisho wa siku tutakuwa sasa tumemuunga mkono Mheshimiwa Rais. Hii ya kusema, tunapiga picha tunaridhiana leo unakwenda unaumiza wengine nyuma si sawa. Kama tunaridhiana, turidhiane kwa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tuseme jambo moja hapa, haya yote mazuri yanayotokana na Mheshimiwa Rais huwezi kuyatofautisha na Wabunge wa CCM. Haiwezekani, Wabunge ndio wanaopitisha bajeti hapa, kama kuna mazuri anayoyafanya Mheshimiwa Rais, Wabunge tuko hapo chini yake ndiyo tunanyanyua. Vile vile ilani inayotekelezwa ni dhahiri ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo haya yote tunayozungumza hapa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, haya yanatokana na Ilani nzuri ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nachukua fursa hii kuwaomba wananchi huko nje walipo wote, wamuunge mkono Mheshimiwa Rais, waiunge ilani yake, wawaunge mkono Wabunge na Madiwani walioko kule, kwa sababu kwa kipindi kifupi mambo makubwa yamefanyika sana sana. Tunaomba Watanzania tushikamane twende kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nasisitiza kwa kuhitimisha hoja hii kwamba, wale walioko humu ndani na watumishi wa umma walioko nje, ambao kwa sauti ile ya Mheshimiwa Rais unaona kabisa unahusika, step down mapema usisubiri tuanze kukutaja, ondoka kiungwana ajali kwenye siasa ni jambo la kawaida utajirekebisha baadaye. Baada ya hapo niombe viongozi na vyombo vya dola vilivyosikia sauti ya Mheshimiwa Rais, pengine watakosa kuona mlango kama alivyosema Profesa hapa, vyombo vya dola viwasaidie kusukuma kuona mlango ulipo. Watusaidie viongozi wa dola ambao wamepewa mamlaka kuwaonesha hao wabadhirifu, hao wezi mlango uko wapi wa kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)