Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hoja hii ya kihistoria.

Mheshimiwa Spika, kiongozi yeyote duniani hupimwa kwa nyakati na mazingira ambayo anachukua nchi katika kuiongoza. Mazingira aliyoyachukua Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Katika kuiongoza nchi hii, yalikuwa ni mazingira magumu, yalikuwa ni mazingira ya kipindi cha giza, yalikuwa ni mazingira ambayo kila mmoja wetu katika nchi hii alikuwa hajui ni wapi tunaelekea.

Mheshimiwa Spika, katika historia ya nchi yetu hajawahi kutokea Rais aliyepo madarakani akafariki akiwa madarakani. Vile vile, katika nchi yetu ilikuwa ni wakati mgumu kwamba sasa tunakwenda katika mlengo upi? Mazingira aliyotoka nayo Mwalimu Nyerere wakati anaichukua nchi hii yalikuwa tofauti, Mzee Mwinyi hivyo hivyo, Mzee Mkapa hivyo hivyo, Mzee Kikwete hivyo hivyo, Mzee Magufuli ilikuwa tofauti na Mheshimiwa Samia ikawa tofauti vile vile.

Mheshimiwa Spika, uhodari wa Rais Samia unaonekana katika maeneo haya. Kama nilivyosema alichukua nchi wakati tukiwa katika majonzi, vile vile alichukua na kuongoza nchi hii akitoka katika Chama kikubwa ambacho ilikuwa ni kazi ngumu kukiunganisha. Ninyi mnafahamu duniani kote anapotoka Rais madarakani kunakuwa na mipasuko mikubwa, yanatengenezwa mazimwi kumtisha Rais aliyeko madarakani, zinatengenezwa hoja za kusema wale ni wa kwako na wale sio wa kwako, zinatengenezwa hoja kwamba wale ni bora na wale sio bora. Hata hivyo, vikwazo hivi Mheshimiwa Samia alivuka ndani ya Chama cha Mapinduzi na Chama hiki imekuwa imara.

Mheshimiwa Spika, hapa leo tunaposema, huwezi ukatanabaisha kwamba wale wa Rais Samia, wale sio wa Rais Samia, wale wa Chama cha Mapinduzi bora, wale sio wa Chama cha Mapinduzi bora, wote sisi tumekuwa chombo kimoja kwa sababu ya uthubutu wa Rais Samia.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo sote tutakubaliana wakati Mheshimiwa Samia anachukua madaraka nchi yetu tulikuwa tumehasimiana sana kisiasa kwa tabia zetu, kwa namna tulivyotoka. Mheshimiwa Samia amechukua uongozi wa nchi hii kukiwa vyama vya siasa vina Wenyeviti wakongwe wamekaa miongo na miongo, wamehasimiana huko nyuma. Hata hivyo hakuangalia historia zote, akasema ni lazima tukae pamoja, ni lazima tuanze mwanzo. Ilikuwa ndiyo Rais Samia kama ni kupoteza alikuwa anapoteza. Maana yake aliamua kwamba pamoja na yote yaliyotokea tunataka sasa nchi yetu tuheshimiane katika demokrasia.

Mheshimiwa Spika, katika jambo hili Mheshimiwa Rais amefanya vizuri sana, amewaunganisha Watanzania wote. Nataka niseme katika jambo la kusamehe ni jambo gumu. Mfano tu mdogo, Mheshimiwa Rais amesamehe mambo mengi na amekubaliana na hoja za wapinzani walizokuwa wanasema. Akiwa kwenye Mkutano wa Chama cha Demokrasia wa Wanawake lugha kubwa aliyoongea ni kwamba tusameheane, lakini wenzetu walisema kuna wenzetu 19 hatuwezi kuwasamehe, tuone namna ya kusameheana ilivyo ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kusema wengine walienda gerezani sijui na wengine walifanyaje, Rais akasema yote hayo tusameheane, lakini wale wakasema wenzetu 19 hatuwezi kuwasamehe asilani. Kwa hiyo tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa moyo wa kuthubutu na kwa moyo wa kusamehe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nije kwenye suala la uchumi. Mheshimiwa Rais alichukua nchi hii ikiwa na miradi mikubwa. Kwenye reli sote ni mashahidi na mambo mengine. Hata hivyo, tumeshuhudia namna ambavyo miradi yetu imeendelea hakuna namna ambao ulilala ha hili vile vile tunampongeza Rais wetu kwa maana ametuvusha na nchi yetu imeweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika diplomasia, sisi tumekaa vizuri, vita ya Ukraine na Russia ni vita ya nadharia katika diplomasia. Ni nani anataka kuwa mbabe na nani anataka wengine aweze kumfuata. Hata hivyo, sisi hapa tumepita vizuri na tumeshikilia msimamo wetu kwamba Tanzania haifungamani na upande wowote na heshima yetu inaendelea kuwepo na tumeendelea kusonga mbele.

Mheshimiwa Spika, vile vile niseme kwenye suala zima la kujenga taasisi, kilichotokea juzi kwenye ripoti ya CAG bado tuna shida ya kujenga uwezo wa kitaasisi. Yale yote ambayo Mheshimiwa Rais amesema tena kwa hasira kubwa ni kwamba wale wote wanaokabidhiwa taasisi za kuiongoza nchi hii ni lazima wawajibike vilivyo na ni lazima wafanye kazi vilivyo. Nakubaliana na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo kwamba Bunge hili lipewe nafasi lisimuonee mtu, lakini ni lazima tutajane, ni lazima tusemane na kwa mazingira ya Rais wetu alivyo, si lazima mpaka ufikishwe hatua ya kutenguliwa. Wapo watu ambao wamefanya makosa hayo, kwa hiyo kwa heshima ya Rais waweze kujiuzulu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)