Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi na nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa Mbunge wa Biharamulo Magharibi kwa kuleta hoja hii. Mambo matatu tu katika kuunga mkono hoja hii. Jambo la kwanza ni kihistoria kidogo.

Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 4 Julai, 2001, nchi yetu ilikumbwa na msiba mkubwa. Tuliondokewa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Omar Ali Juma; na Mheshimiwa Benjamini William Mkapa, Mungu amrehemu, wakati analihutubia Taifa alitumia nafasi hiyo kwa kutumia maisha ya Dkt. Omar Ali Juma kutoa mafunzo ambayo tumeyapata. Kwamba tuna mafunzo sita kuhusu sifa za msingi ambazo kiongozi wa kitaifa Tanzania anapaswa kuwa nazo, alitoa sifa sita. Na mimi miaka miwili ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ninaridhika kwamba hizi sifa ambazo Mheshimiwa Benjamini William Mkapa alizitoa tarehe 4 Julai, 2001 Mheshimiwa Rais anazo; na kwa ridhaa yako naomba nizitaje.

Mheshimiwa Spika, sifa ya kwanza ni utu na uadilifu, sifa ya pili aliitaja upendo na heshima kwa watu wote, sifa ya tatu kupenda kazi na kutumikia wananchi badala ya kupenda kutumikiwa na kutukuzwa, sifa ya nne aliitaja kuweka mbele maslahi ya Taifa na Watanzania badala ya maslahi binafsi au ya kikundi, sifa ya tano unyenyekevu badala ya kupenda makuu na sifa ya sita, na kwa maoni yangu ni muhimu sana, kuzingatia kikamilifu misingi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, na aliitaja misingi hii tisa ambayo kwa hakika Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaizingatia kikamilifu. Msingi wa kwanza wa Taifa utu, pili haki, tatu usawa, nne fursa sawa, tano amani, sita umoja, saba upendo, nane mshikamano na ya mwisho namba tisa ambayo ni muhimu sana Muungano wetu wa Tanzania Bara na Zanzibar. Hakuna shaka katika miaka yetu yote katika nchi hii Muungano wetu upo salama sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili,hakuna shaka kwamba mambo haya yote Mheshimiwa Rais anayafanya kwa utashi kwa ujasiri na kwa kuzingiatia katiba na Sheria za nchi yetu. Lakini kumekuwepo na jitihada za hapa na pale kwa baadhi ya watu kujaribu kumtenganisha Rais wetu na Chama cha Mapinduzi. Nataka nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu anayoyafanya haya yote ili kutekeleza kikamilifu Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Spika, na nitoe mfano, katika Ilani yetu paragraph118 ukurasa wa 166 tumesema hivi; katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama cha Mapinduzi kitaendelea, sikiliza hiyo, kuheshimu na kulinda misingi ya demokrasia na haki za binadamu kwa ajili ya ustawi wa Taifa hili. Kwa hiyo suala hili Mheshimiwa analifanya kwa kutekeleza Ilani ya CCM kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, lakini paragraph ya 250 ukurasa wa 298 ameweka wazi. Ilani inasema katika kipindi cha miaka mitano ijayo Chama cha Mapinduzi kitaendelea kutekeleza jukumu la kihistoria la kimapinduzi la kuongoza pambano la kutetea na kulinda utu, usawa na haki chini ya misingi ya Ujamaa na Kujitegemea. Katika kutimiza wajibu huu CCM itaendelea kusimamia mambo matano yafuatayo, jambo la nne ni kuimarisha demokrasia nchini. Kwa hiyo wale wanaodhani kwamba wanajaribu kumtenga Rais na CCM wamenoa ni sehemu Rais anatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho; baada ya kupokea report ya CAG juzi, Mheshimiwa Rais ameshatekeleza jukumu lake, yamebaki majukumu mawili. Jukumu la kwanza kwa Bunge hili na jukumu la pili ni kwa Serikali kupitia Mawaziri wetu. Mimi niwaombe katika muda tulionao siku 88 za kukaa hapa Bungeni tunatarajia kuona kutoka Serikalini majibu yatakayo jibu zile changamoto za kimfumo, kisheria na kikanuni; tuzione kutoka kwa Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wetu Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais kaongea kwa uchungu sana kama alivyotoka kusema Mheshimiwa Ole-Sendeka kazi yetu; hiyo ni kazi ya Serikali, kwa upande wetu sisi. Sisi Tanzania hatuna utamaduni wa kupisha. Kazi yetu Wabunge tuwaoneshe wenzetu, ambao Mheshimiwa Rais amewasema, mlango wa kutokea. Kazi hiyo duniani huwa haifanywi na Serikali, huwa inafanywa na Bunge. Tunatarajia Bunge hili, watu wote ambao Mheshimiwa Rais amesema wapishe hawajaona mlango sisi tuwaoneshe mlango. Katka miezi hii mitatu hilo ni jukumu la msingi la Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,baada ya kusema hayo na mimi nichukue nafasi hii kwa heshima kubwa ninaunga mkono hoja hii tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na Rais popote alipo atembee kifua mbele ajue Bunge hili linamuunga mkono, lipo naye usiku na mchana. Ahsante sana. (Makofi)