Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya upendeleo, ili niwe ni miongoni mwa Wabunge ambao wamechukua nafasi hii kuunga mkono azimio hili la kumpongeza mama yetu. Sasa naomba nisema hivi, na nitazungumza kwa ufupi, ili na wengine wapate nafasi.

Mheshimiwa Spika, naomba kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu. Tumshukuru kwa sababu, kwanza ameamua kutekeleza kwa vitendo kulinda na kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwenye hili, waswahili wanasema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni; kwa kitendo chake cha kushirikisha vyama na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha kwamba, nchi yetu inaendelea kuwa na amani na yenye maendeleo, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa maana hiyo kwenye mfumo huu wa demokrasia kuna msemo wa Kiswahili unasema, wengi wape lakini wachache wasikilizwe. Kwenye hili, mama yetu ameonesha mfano kwa vitendo na sisi kama Wabunge, kama Bunge, tunao wajibu wa kuendelea kumuunga mkono kwa sababu ni jambo alilolifanya kwa vitendo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba niendelee kusema hivi kwamba, kwenye hoja ya mambo ya uchumi mama yetu amefanya mambo mengi. Wenzangu wamezungumza mambo mengi sana, ametoka nje, ametafuta wawekezaji, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza pale wawekezaji wengi wako njiani wanataka kuja, sisi naomba Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono mama yetu. Tumuunge mkono kwa sababu, jitihada hizi zinahitaji amani, jitihada hizi zinahitaji imani, bila ya imani wawekezaji hawawezi kuja, lakini bila ya amani wawekezaji pia hawawezi kuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule nyuma niliwahi kusema kwamba, amani tuliyonayo Tanzania ni tunda adimu ambalo duniani halipo, tuendeleze. Na sisi Wabunge tukishikamana tunaweza kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ningeomba basi kwa sababu, jitihada zote zinazofanyika ni kuweka nchi pamoja, ni kuweka wananchi pamoja, ili tuweze kujenga Taifa letu, ningewaomba sana basi tumuunge mkono katika jitihada zake za kuhakikisha kwamba, uchumi unaendelea kukua. Mama yetu naomba tukuthibitishie uchumi huu utakua, lakini na wewe mama yetu endelea kutupa nguvu, ili tukupe nguvu, ili kazi ziende vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hili kwa sababu hii, Mheshimiwa Ole-Sendeka amezungumza hapa kwamba, kwa kweli mama yetu anafanya jitihada za kuleta wawekezaji, lakini tuko baadhi yetu ambao tunamshika mashati, ili kumrudisha nyuma. Kule nyuma mama aliwahi kusema, rangi zake ni nyingi tusizitafute, lakini juzi tumeiona moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba niombe hivi, na ninaomba niombe kwa heshima kubwa sana, mama amezungumza lugha nyepesi ya kistaarabu wale wenyewe wajitathmini na watupishe. Sikuelewa hiyo lugha yake, lakini naomba niiseme hivi, wale waliopewa nafasi na wanazijua nafasi zao kwamba, mama amechukia kwa sababu tunamrudisha nyuma, naomba sana tumpishe ili afanye kazi zake, tusimrudishe nyuma. Na mama yetu tunakuomba sana, umewapa nafasi na waswahili wanasema mwenye kuvuliwa nguo huchutama, naombeni sana wale wote wenye kujijua hili wasisubiri kuvuliwa nguo halafu tukawazomea maana kwa kweli, tutawazomea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa heshima na taadhima Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono jitihada hizi, mama amefanya kazi kubwa, anaendelea kufanya, lengo na dhamira yake ni kuhakikisha kwamba, Taifa letu linasonga mbele, naomba sana. Kwenye hili naomba nitoe angalizo au nitoe pendekezo; mnaposafiri baharini wako wengine wanayo kawaida ya kutoa boti, sasa ili boti hili lisizame naomba tukubaliane hivi, wale ambao tunawaona wanaendelea na wana jitihada za kutoa boti, ili tusifike safari yetu, tunaomba tuwatose kabla hatujazama sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)