Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru sana kupata fursa hii ya kuchangia azimio hili muhimu. Historia inajieleza kwamba nchi yetu toka ipate uhuru imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia ajenda zilizoko mezani mwa Afrika na dunia kwa ujumla katika maeneo ya uchumi, siasa na maeneo ya kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mungu kwamba katika awamu hii ya sita tumepata kiongozi ambaye anayatambua haya na yuko tayari kuyaishi. Sote ni mashahidi kama mtoa hoja alivyozungumza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba demokrasia na utawala bora vinastawi katika nchi yetu. Sasa hii ni muhimu katika kuleta utengamano na amani ndani ya nchi, lakini pia katika kukuza uchumi.

Mheshimiwa Spika, hakuna nchi ambayo inaweza ikakua kiuchumi kama hakuna demokrasia na utawala bora kama ambavyo sasa hivi hapa Tanzania tulivyo. Tunao ushahidi kabisa wa nchi nyingi ambazo zina uchumi mkubwa sana wa maliasili na kila kitu, lakini kwa sababu hakuna amani na utulivu, uchumi ule na zile mali haziwafai kitu chochote kw kuwa amani na utulivu unakuja pale ambapo kuna demokrasia, utawala bora na haki. Kwa hiyo, kwa hilo lazima tumpongeze sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa diplomasia ya kiuchumi, kwanza pamoja na maana zake nyingine nyingi, lakini diplomasia ya uchumi ni zile hatua za makusudi ambazo Taifa linazichukua ili kuonesha mahusiano mazuri na dunia na pia kukuza uchumi na ajira za wananchi wake bila kujali kama kuna gharama zozote za kisiasa ambazo zinaingia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu tumeona faida kubwa sana ya diplomasia ya kiuchumi ambayo Mheshimiwa Rais ameisimamia. Majimboni kwetu kote kuanzia Jimboni kwangu Mwanga na Waheshimia Wabunge wote wanashuhudia kwamba iko miradi mikubwa ambayo inaendelea kuliko kipindi kingine chochote ambacho kimewahi kuwepo katika historia ya nchi yetu. Hii miradi inaendelea, mingine kutaokana na fedha ambazo zinatoka nje na pia hali ya uchumi inaimarika kutokana na utawala bora na hali ya demokrasia ambayo tunayo katika nchi.

Mheshimiwa Spika, kubwa la kumpongeza Mheshimiwa Rais ni kwamba amesisitiza kabisa masuala haya ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu kwamba yatafanyika kwa kuzingatia mila na desturi zetu sisi Watanzania. Hatuingii katika masuala haya kwa lugha za mitaani kusema kichwa kichwa, bila kuangalia kwamba sisi Watanzania tumetoka wapi na historia yetu imetoka wapi? Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anatuongoza vizuri kwamba tuingie kwenye mambo haya ambayo ni muhimu katika dunia, lakini kwa kuzingatia mila zetu na desturi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni rahisi sana watu kusema kwamba aah, mbona haya mambo tayari yapo kwenye Katiba! Ni sahihi, yapo kwenye Katiba, hata hivyo zipo nchi nyingi ambazo mambo yapo kwenye Katiba za nchi zao lakini wanakosa viongozi ambao wana utashi wa kuyatekeleza na kuyasimamia, na hiyo hasa ndiyo sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa uchache tu kwa kweli niungane mkono na mtoa hoja pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na kuomba kwamba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika hili na Tanzania kwa ujumla katika hatua hizi za utekelezaji wa sera hizi za kidemokrasia, utawala bora na diplomasia ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)