Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia mchango wa maandishi katika Wizara ya Afya na nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, pia nakupongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika pamoja na uongozi wote wa Bunge kwa kazi nzuri mnazoendelea kuzifanya.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia kwa umahiri suala zima la afya, nampongeza pia Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza Wizara ya Afya kwa kumshauri vyema Rais katika kusimamia suala zima la upatikanaji wa dawa nchini. Nampongeza Mama Samia Suluhu kwa ziara yake ya Uganda ambayo imeleta unafuu kwa waathirika wa virusi vya UKIMWI kupata dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI hapa nchi jirani ya Uganda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo kubwa na zuri limefanyika hivyo tunaipongeza Wizara na wataalamu wake wote kumshauri vyema Rais.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa dawa, bado tunaendelea kuishauri Serikali kama nilivyochangia katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba Serikali ione sasa namna bora ya kuongeza uwezo wa upatikanaji wa dawa kwa kuingia ubia kwa kufufua kilichokuwa kiwanda chetu cha dawa cha Mkoani Arusha (Tanzania Pharmaceutical Industry- TPI) hivyo Serikali kupitia MSD itachukua 60% ya hisa za uwekezaji wa kiwanda kile ambazo zilikuwa ni za mwekezaji binafsi na hisa 40% zitabakia kwa Msajili wa Hazina kama ilivyokuwa toka mwanzo. Kwa hiyo Serikali itakuwa na 100% ya hisa ili kufufua kiwanda chetu cha Arusha. Tunaamini kwa usimamizi mzuri wa MSD tutakuwa na uwezo mzuri wa kuzalisha dawa za kutosha kwa ajili ya wananchi wetu na pia tunaweza kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia kwa dhati na kwa moyo wa kizalendo na kwa kujitoa muhanga katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda ikiwa ni pamoja na viwanda vya kutengeneza dawa ili kuelekea katika kutimiza malengo endelevu ya milenia.

Mheshimiwa Spika, nikiwa kama mwakilishi wa wafanyakazi wa Tanzania Bara Bungeni, napongeza kitendo cha Mheshimiwa Rais na Serikali yake kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi na kuongeza mshahara kwa asilimia 23.3 jambo ambalo halijawahi kutokea katika Serikali yetu na suala la ongezeko la mshahara limekuwa ni kilio cha wafanyakazi kwa miaka isiyopungua sita.

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kuliomba Bunge kuazimia kumshukuru na kumpongeza Rais na Serikali yake kwa niaba ya wafanyakazi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuandika hayo naunga mkono hoja.