Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii.

Kwanza kabisa nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Ummy kwa kurudishwa katika Wizara hii yeye pamoja na Naibu wake, kwa kweli naamini kabisa sasa mambo yatakaa sawa. Ambaye hamjui Mheshimiwa Ummy akaiulize Covid Ummy ni nani ndiyo mtamfahamu kwamba Ummy ni nani. Hata Covid ikimsikia Ummy inakimbia.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa hiki kitendo alichokifanya cha mabadiliko MSD, kwa kweli amefanya kitendo kizuri sana na kuwafariji Watanzania ambao wengi sana walipata maumivu makali sana ya mambo mengi maovu ambayo yalikuwa yakitokea. Na bahati nzuri amemchagua Mkurugenzi ambaye ni jembe ambaye naamini kabisa, timu yao kwa kushirikiana na Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri, sasa mambo yatakaa vizuri. Kwa hiyo mimi niseme nawaombea Mwenyezi Mungu ili watufikishe salama.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba Mheshimiwa Waziri aangalie, kuna mambo ambayo ni ya muhimu sana naomba ayatupie jicho la tatu, yeye pamoja na wasaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, kuna hizi gharama za kufungua faili na kumuona daktari, naziona hapa; kwa kweli hizi gharama zimepanda sana kutoka shilingi 3,000 zimefika 7,000 hadi 10,000. Kwa Mtanzania wa kawaida na haswa mwanamke ni ngumu sana ku-afford gharama hizi kutokana na hali halisi ya maisha ya Kitanzania. Kama mnavyojua, kwa mfano ukiangalia kule kwetu, vijijini, kama vile Mkoani Mara, kule shughuli zetu ni ndogo ndogo ambazo zinakuwa kidogo ni ngumu sana, na haswa mama anapouguliwa na mtoto au yeye mwenyewe anapouguliwa; na ukizingatia sisi wanawake wa Mkoa wa Mara wengi ndio sisi viongozi wa familia au tunao hudumia familia kwa ujumla. Naishauri Serikali iziangalie gharama hizi kwa jicho la pili ili kuangalia namna ya kumpunguzia mwananchi gharama hizi ili aweze sasa kwenda kutibiwa kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niongelee hili suala la dawa hospitalini. Kwa kweli hali ya dawa hospitalini hairidhishi kabisa. Zile dawa muhimu sana pale wanapoenda kutibiwa wagonjwa hospitalini na hasa wale wagonjwa wanaoenda wengine wakiwa wana bima, wanapoenda kutibiwa hospitalini wanaambiwa waende wakanunue nje ya geti la Hospitali, Zahanati na kwenye vituo vya afya. Jambo hili si zuri sana kwa kweli, hili ni tatizo, na waathirika wakubwa ni akina mama na watoto.

Mheshimiwa Spika, isitoshe Mheshimiwa Rais ametoa pesa bilioni 129 kwa ajili ya kununua madawa. Sasa je, hawa ambao wanachelewesha chelewesha au kubana bana hizi fedha hawaoni kama wanamchonganisha Mheshimiwa Rais na wananchi?

Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe kama mtoto wa Chifu Hangaya, msimuangushe mama yetu, amefanya kazi kubwa sana. Fedha aliyowapa fanyieni kazi, otherwise kila siku mtakuwa mnatumbuliwa na mnalalamika. Naamini kabisa, kwa huu uteuzi wa sasa wa Mheshimiwa Ummy pamoja na Mkurugenzi mpya na ofisi yake, naamini kabisa sasa mambo yatakaa vizuri. Mheshimiwa Ummy usituangushe. Waheshimiwa Wabunge tunakuamini sana, tunaamini mambo yatakaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hospitali za Rufaa za Mikoa kwa kweli kipekee nimpongeze sana kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa kutuendelezea hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoani Mara. Mama ametoa fedha ambazo zimeendeleza hospitali hiyo. Sasa, mimi niwaombe watendaji kuwa fedha hiyo itoke ili hospitali hiyo imalizike. Pia niombe, kuna suala la wauguzi, tunaomba pia tupate madaktari bingwa ili kudumisha ile huduma ya afya zaidi. Kipekee zaidi nimpongeze pia mama yetu kwa kazi nzuri sana aliyoifanya ya kuongeza ajira kwa Watanzania. Ajira Mheshimiwa Rais alizozitoa zimeleta faraja kubwa kwa baadhi ya Watanzania, kwa kweli tunamshukuru sana na kumpongeza Mungu ambariki.

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali lakini pia nimuombe mama. Mama hapa ulipokaa basi tunakuomba uongeze ajira mama kwa kuwa hazitoshi, ajira bado watu wengi wana vyeti ambavyo viko kwenye mifuko yao na wengine wameviweka chini ya kitanda. Mama tunakuomba ongeza ajira kidogo, wapo watu wengi ambao hawana ajira. Kwa hiyo mimi niseme tu nashukuru sana Serikali yangu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia zaidi nampongeza sana mama kwa kitendo alichokifanya juzi cha kuwajali Watanzania wafanyakazi kwa kuwaongezea mishahara, Mungu akubariki sana mama, tunaamini mama unaupiga mwingi, haulali usingizi unatuhangaikia Watanzania, tunasema tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais. Jamani Waheshimiwa Wabunge akina mama na akina baba pigeni vigelegele jamani kwa Chifu Hangaya wakeeee!

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)