Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami nichangie katika Wizara hii ya Afya. Awali ya yote, napenda kumshukuru sana Mungu kwa kunipatia nafasi nami kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Napenda sana kumshukuru Rais wetu kwa ajili ya kumwamini Mheshimiwa Ummy Mwalimu kuwa Waziri katika Wizara hii ya Afya pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Mollel. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pasi na shaka Mheshimiwa Ummy Mwalimu ni mchapa kazi, Rais hajakosea. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, baada ya mchango kuhusu afya ya akili, sasa huyu ni mtaalamu wa afya ya akili. Kwa hiyo, tumsikilize mtaalamu wa afya ya akili akichangia. (Makofi/Kicheko)

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba muda wangu dakika moja uweze kuniongezea. Nampongeza mchangiaji aliyechangia katika masuala ya afya ya akili. Aliloliongea nami nataka kuliongezea hapo hapo.

Mheshimiwa Spika, suala la afya ya akili na magonjwa mengine kwa kweli ni changamoto. Katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2020, ukurasa wa 138 (w), lengo la chama chetu wakati tunainadi ilikuwa inasema hivi, nanukuu: “kutoa elimu na uhamasishaji kwa wananchi kuhusu kinga, udhibiti na kuzuia magonjwa yasiyoambikiza ikiwepo afya ya akili.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2021 inaonesha kwamba, watu takribani milioni 38 hupoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambikiza ikiwepo afya ya akili. Hawa watu ni wa umri kati ya miaka 30 mpaka 69 hasa katika nchi zinazoendelea.

Mheshimiwa Spika, magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ni changamoto katika nchi yetu na magonjwa haya Waheshimiwa wengi waliochangia hapa wameyaelezea. Ukiangalia hata matatizo yote ya kijamii ni kutokana na magonjwa ambayo siyo ya kuambukiza ikiwemo hiyo ya afya ya akili. Magonjwa hayo ni kama shinikizo la damu, moyo, kisukari, saratani na mengine kama ya afya ya akili, kupooza, hata kutokuona vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, magonjwa haya, kama alivyotangulia kusema aliyechangia, ni ya maisha na hivyo basi tiba yake ni ghali sana. Hupoteza nguvukazi ya watu, watu hubaki na umasikini, mahusiano huvunjika na mwisho watu kuchanganyikiwa na hivyo basi, nchi kuendelea kuwa masikini.

Mheshimiwa Spika, haya magonjwa yasiyo ya kuambikiza ni ghali kwa sababu magonjwa mengi matibabu yake ni ya maisha. Yaani mtu akishagunduliwa kwamba ana matatizo ya akili itachukua muda kumtibu huyu mtu mpaka apone kabisa. Mtu akigundulika ana magonjwa ya kisukari, mtu akigundulika ana shinikizo la damu, matibabu yake ni ya maisha, lazima awe anakwenda katika vituo vya afya mara kwa mara. Pia dawa za kutibu haya magonjwa ni ghali sana na hivyo huigharimu Serikali pesa nyingi kuyatibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, visababishi vya magonjwa haya ni maisha ya kawaida ikiwepo na kutumia vitu kama tumbaku, pombe za kuzidi kiasi, vitu kama lishe isiyozingatia misingi ya afya, kwa mfano, kutumia sukari nyingi, mafuta mengi au chumvi nyingi. Vilevile kutoshughulisha mwili, kwa mfano kutokufanya kazi za kutumia misuli na vile vile kutokufanya mazoezi. Kuna sababu nyingine kwa mfano za uzee au za kurithi zinazosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza, lakini haya hatuwezi kuyazuia.

Mheshimiwa Spika, ni vyema sasa Serikali ikatilia mkazo masuala ya magonjwa yasiyo ya kuambikiza. Moja katika sera yetu ni kutoa elimu. Hivyo basi, naishauri Serikali itilie mkazo elimu ya afya ya jamii katika jamii yetu ili tuweze kuzuia magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza ili wananchi wetu waweze kubaki salama. Naishauri Serikali kuimarisha kitengo hiki cha afya ya jamii katika Wizara. Hii itapunguza magonjwa mengi na hivyo kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kutibu magonjwa haya yasiyoambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, itabidi sasa Serikali chini ya Waziri wetu mwenye dhamana ya afya kuangalia ni jinsi gani anaweza akatumia mbinu, interventions, katika kuhakikisha kwamba afya ya jamii inaenda mpaka ngazi za chini kabisa katika family level ili kuweza kugundua magonjwa haya na kuweza kuwaelimisha hawa wananchi kujua ni njia gani au ni visababishi gani vya magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya akili. Hivyo basi, naishauri Serikali kuimarisha kitengo badala ya kuimarisha zaidi tiba, iweze kuweka balance kati ya tiba na kuzuia. Pawepo na uwiano ulio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kama pesa nyingi zitawekezwa kwenye tiba, dawa na MSD, lakini vilevile katika kuzuia, pawe na uzito ule ule. Vijijini, wataalm wasambazwe huko; shuleni kuanzia msingi watoto wafundishwe kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiuza ili watakapofika miaka 30 wajue wanafanyaje? Wajue kufanya mazoezi, wajue kula lishe bora ili hizo ndoa ambazo zimeshasemwa na wachangiaji ziimarike. Lishe bora iwekwe katika familia, watu wajue wanafanyaje katika kuzuia ili wasipate kisukari? Wanafanyaje kuzuia wasipate pressure? Wafanyaje ili wazuie kutokupata magonjwa ya akili kama yalivyosemwa na kushangiliwa hapa?

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, katika mchango wangu niseme tu, kinga ni bora kuliko tiba. Hilo halipingiki. Tuhakikishe kwamba sasa Wizara iweke kipaumbele pia katika kinga. Simaanishi kwamba tiba isiwepo, kwa wale ambao tayari wameshapata magonjwa haya, tiba iwepo, lakini tuzuie mafuriko kabla hayajaingia yatudhuru zaidi. Tuwekeze zaidi katika kinga. Sawa, haitachukua muda mfupi kama tunavyofikiria, lakini tuzuie ili ile generation inayokuja juu isiweze kupatwa na magonjwa hayo. Hata kama ikipatwa, basi iweze kujua namna ya kuishi nayo na namna ya kujua dalili za awali kabisa na kupata tiba mapema.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nami pia naunga mkono hoja. (Makofi)