Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia katika Hotuba ya Bateji ya Wizara ya Maji ambayo kwa Mwaka huu wa Fedha inakwenda kutumia bilioni 709.36.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nipende kupongeza na kutambua jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji, na hasa dhamira njema na utashi kwa Mheshimiwa Rais wa kuwapatia wananchi wake maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani pamoja na matumizi mengineyo. Ni jitihada hizi za Serikali ambazo sasa tunaona dhamira njema ya Mheshimiwa Rais. Tunaongelea Mradi Mkubwa unaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kuleta katika Makao Makuu ya nchi hapa Dodoma. Hili linatambua neema ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia, ukiiangalia Jiografia ya Afrika utagundua kwamba sisi ni moja ya nchi ambayo tumebarikiwa sana kuzungukwa na Maziwa Makuu matatu tena mojawapo ni Ziwa Tanganyika likiwa ni moja ya Ziwa lenye kina kirefu katika Maziwa ya hapa Duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na kwamba hesabu si nyepesi kihivyo lakini kutoka Ziwa Victoria kuja Dodoma ni kilomita 700. Ukichukua umbali huo huo kutoka Ziwa Tanganyika au kutoka Ziwa Nyasa utagundua kwamba kama tukivitumia vyanzo vikuu hivi vitatu nusu ya nchi ya Tanzania inapaswa kuwa supplied na maji bila kutafuta vyanzo vidogo vidogo vinavyokauka. Kwa hiyo, mimi nilikuwa napendekeza sana kwamba kwa dhamira njema ya Mheshimiwa Rais na utashi wa Serikali kama tumethubutu kubuni Mradi unaotoka Ziwa Victoria hadi Dodoma, utashi huo huo uelekezwe katika vyanzo vikuu vingine vya Ziwa Tanganyika ambalo ni Ziwa lenye kina kirefu, maji ambayo hayatakauka na Ziwa Nyasa na tuone kwamba vyanzo hivi vingine vidogo vidogo ndivyo vihudumie sehemu nyingine ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo matatu. Jambo la kwanza ni mfumo wa uondoaji maji taka pamoja na usafi wa miji. Hadi sasa kwa kadri ya ripoti ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba tumefanikiwa kuwa na mifumo hiyo kwa asilimia 15 na kwamba lengo letu ni kwenda asilimia 30 ifikapo mwaka 2025. Na utangundua kwamba tuna miaka mitatu ambayo imebaki na sisi ndiyo tuko nusu ya mwendo. Sasa nipende pia kutambua kwamba kama hatuwezi kuwa na uondoshaji na mifumo mizuri ya kuondoa maji taka katika miji yetu, miji yetu inakuwa siyo misafi na ndiyo maana utakuta mito inayotiririka katika miji yetu siyo misafi. Lakini katika nchi za wenzetu maeneo ambapo unakuwa na baraka ya mto kupita katikati ya Mji ndiyo maeneo ambayo yamefanywa kuwa ya vivutio, sehemu za utalii na mito inajengwa kiasi kwamba hata boti zinapita, watu wanafanya sherehe mle. Lakini sisi kwa sababu ya kutokuwa na mifumo mizuri mito yetu inakuwa inatiririsha maji taka. Na hilo Mheshimiwa Waziri nilizani kwamba Serikali iweze kutoa msukumo mkubwa ili kwamba Miji yetu iweze kuwa misafi. Kwa hiyo, Wizara ya Ardhi hapa pamoja Mipango Miji watusaidie, wananchi wasitutangulie ili kwamba tunapopanga makazi basi na mifumo ile ya kuondoa maji taka iweze kupangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu mabwawa ya Kimkakati ya Farkwa pamoja na Kidunda; yameongelewa na Wabunge wenhgi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati miradi hii inaibuliwa ni kweli kwamba idadi ya watu katika miji husika ilikuwa ni ndogo. Sasa kama tunaiita kwamba ni miradi ya kimkakati maana yake ni kwamba hata tengeo lake la fedha linapaswa kuwa la kimkakati. Haliwezi kusubiri bajeti ya kila mwaka kwa sababu la sivyo idadi ya watu itazidi kuongezeka katika miji, watu watakosa maji na tutajikuta kwamba tunashindwa kuwa na miji ambayo ni salama ni misafi na pia miji inakuwa hailingani na maendeleo tunayoyataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili Mheshimiwa Waziri nilidhani kwamba hebu tuendelee kulipanga kimkakati, na hasa haya mawili; kwa sababu Farkwa inapaswa ihudumie hapa Makao Makuu ya Nchi, lakini pia Dar es Salaam tunaona kwamba idadi ya watu inazidi kuongezeka. Kama wewe mwenyewe ulivyosema chanzo cha Ruvu kilionesha kukauka mwaka uliopita. Kwa hiyo, hili lazima lipangwe kimkakati ili tuweze kuwasaidia wananchi wa maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda kuongelea ni ujenzi wa mabwawa wa ukubwa na malambo madogo. Tumeendelea kushuhudia kwamba utekelezaji wa miradi hii mingine inafanikiwa lakini mingine haifanikiwi; na ni kwa sababu miradi inakamilika halafu kiongozi wa kitaifa anakwenda kukagua anakuja kupewa taarifa ya kwamba mradi huu siyo thamani ya fedha. Sasa hapa nadhani tunapaswa Serikali ifanye mkakati kwamba tunapeleka fedha nyingi sana katika kujenga haya malambo. Sasa mimi pendekezo langu, ili isitokee Kiongozi wa Kitaifa anakwenda kwenye mradi halafu anakuta mradi umetengenezwa vibaya tuwe na kamati za continues monitoring and evaluation zinazohusisha viongozo wa Tamisemi; ili Waziri wa Maji anapokwenda au Waziri Mkuu anapokwenda kukagua mwisho wa wakati basi hata Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na timu yote ya Tamisemi wanaweza kuwajibika kwamba tuliukagua kila wakati na hivyo tutaondokana na dhana ya fedha kutolewa lakini mradi unakuja kukataliwa kwa sababu fedha zimetumika vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama, Kamati hizi za Continues Monitoring and Evaluation zitakuwa zinagharimu fedha kidogo; tuzitumie ili kuepuka miradi kuja kukataliwa kwa sababu imekuwa inatumika vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja na ahsante sana.