Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nichukue nafasi hii kupongeza Serikali na hasa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri ambayo wameifanya toka wamekabidhiwa ofisi hiyo na hasa kwa kipindi hiki ambacho wamekaa wanaboresha mitaala na wanaboresha sera katika elimu. Nitakwenda moja kwa moja kwenye point, kwanza nitazungumzia kuhusu ajira kwa Wahadhiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongea mara nyingi kwamba Wahadhiri hawatoshi, wameajiriwa 2017 mpaka 2018 ndiyo kulikuwa na ajira. Kuanzia hapo wanasema ajira zimeongezeka, lakini siyo ajira mpya yaani ni ajira mbadala, labda mtu ame-retire au mtu bahati mbaya amefariki, ndiyo kunakuwa na replacement.

Kwa hiyo ajira zimekuwa ni shida na madarasa yale tunajua ya Vyuo Vikuu makubwa wanafunzi ni wengi bado ajira haitoshi kabisa. Hata leo ukiwauliza hapo mbele wanasema tumeajiri, wanipe data wameajiri Wahadhiri wangapi katika kila chou, waje na majibu wameajiri Wahadhiri wangapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo tuliomba, kwa sababu kuna shida hii ya ajira, hebu tuongeze retirement age ya maprofesa. Leo tumesomewa hapa idadi ya maprofesa waliokuja pale, bado wana nguvu ya kuweza kutoa msaada katika vyuo. mfano juzi tulikuwa na profesa Ishumi, mawazo aliyokuwa ananipa pale mimi mwenyewe nilishangaa akina Profesa Maboko bado akili zao zinafanya kazi safi, kwa hiyo tuongeze retirement age.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri alinijibu siku moja akasema hilo tumelichukua. Haya majibu ya kusema hilo tumelichukua sijui wanayachukua wanayapeleka wapi? Sisi tunataka utekelezaji ndiyo unafaa, unalichukua unalibeba unalipeleka wapi? Wazo limetolewa kama linawezekana lifanyiwe kazi, waongeze muda wa maprofesa, miaka 65 bado wadogo sana. Wizara imeona maprofesa walivyo wadogo na wanavyofanya kazi; akina Profesa Ndekidemi bado anafanya kazi ya kutosha. Profesa Muhongo yuko hapa, wanafanya kazi nzuri. Naomba Wizara iongeze age ya retirement kwenye vyuo vikuu ili hawa watu watusaidie kwenye vyuo vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mshahara pia. Hawa Ma-VC, nilizungumza. Ma-VC hawana mishahara, yaani wamepewa vile vyeo hawana mishahara. Wakati mwingine inalingana kabisa na wale Wahadhiri wa kawaida. Hivi kutakuwa na heshima kweli katika kufanya kazi? Mtu ni mkuu wa Chuo mshahara wake unalinga na na lecture wa kawaida. Hebu Waziri wa Elimu libebe hilo, wewe ni Profesa, unafahamu kazi za maprofesa wenzako huko vyuoni, libebe hilo ukalifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika vyuo vikuu, ipo haya ya kuruhusu freedom katika academics. Tuwaachie uhuru vyuo vikuu kwenye suala la taaluma lisiingiliane na watu wa Utumishi. Zamani kulikuwa na utaratibu, wale wanaofanya vizuri tunawabakiza pale na wanachaguliwa na wetu wenyewe pale pale vyuo vikuu. Anabaki pale kama tutorial assistant baadaye analelewa, anafanyiwa mentoring, anapanda, anaenda kusoma mpaka anakuwa na Ph.D; lakini tukiliondoa hilo kwenye upande wa taaluma, yaani University hazina freedom kabisa. Hiyo lazima tuiangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika kuajiri, tunaposema tuongeze retirement age pia tuhakikishe sasa hivi Universities ziwe kweli universal, tuwaruhusu walete maprofesa kutoka nje ya nchi. University zetu kweli jamani zimekuwa local; very local. Tuwaruhusu walete maprofesa kutoka nje ili kweli tuweze kupata elimu mchanganyiko inayokidhi haja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye hizi suala za fedha za HIT. Fedha za HIT ni mkopo na mikopo huwa inalipwa na wote, na vyuo vyote. Naomba mgawanyo wa fedha uende kwenye Private Universities na Public Universities. Siyo unanijibu hapa siku moja Mheshimiwa Waziri unaniambia kwamba na wale private watapata kamgao as if wao hawastahili. Inapokuja mikopo hapa, tunalipa wote na sehemu zote zinalipa mikopo sawa kupitia kodi. Kwa hiyo, naomba Wizara ihakikishe ije na majibu mazuri kwenye ule mgao wa HIT; Private Universities wanapata vipi na Public wanapata vipi? Kwa sababu hawa watoto wanaosoma ni watoto wetu sote. Kwa hiyo, hata yale manufaa ya mkopo wayapate wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nipongeze kwenye…

(Hapa kengele iliilia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Ni kengele ya ngapi? Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazofanywa na TET; hawa TET (Taasisi ya Elimu) kazi yao ni kuandaa mitaala, kufuatilia na kutoa mafunzo. Mwaka 2005 wakati imekuja hiyo programu ya ufundishaji mahiri (competence base) walimu hawakupewa training ndiyo maana leo hii tunalalamika hapa, walimu hawajui kufundisha, wanawafundisha watoto hawawezi wakawa na skills kwa sababu hii programu walimu hawakupata mafunzo na kama walipata, walipata wachache mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naiomba Wizara, kwa sababu mmekaa mnaandaa hii mitaala na tumeipigia kelele sana hapa Bungeni, inapokuja kwenye kutoa mafunzo, tuwape fedha za kutosha hii taasisi ili watoe hayo mafunzo, lakini niwaombe hawa wanaotengeneza mitaala, waangalie ule mfumo wa chakula, nami nipo tayari kwenda kusaidia hata bila posho; mfumo ule wa chakula na mfumo wa uzazi wauangalie vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mfumo wa uzazi toka mwanzo tunafundisha tohara ni muhimu. Sasa kwenye mfumo wa uzazi waanze kuingiza ukeketaji ni haramu, waweke kwenye mfumo wa uzazi. Watoto wakianza kujengeka toka mwanzo kwenye ile reproduction kwamba ukeketaji haufai, itawajengea hiyo kuelewa na huo ukeketaji tunaoupigia kelele unaweza ukapungua. Ukeketaji ni ukatili, wekeni ndani ya mfumo wa uzazi mnapokwenda kurekebisha hiyo mitaala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia angalieni mfumo wa chakula. Kwenye ule mfumo wa chakula andikeni umuhimu wa chakula; umuhimu wa chakula kwa watoto wa kike na watoto wa kiume. Sasa hivi huu mfumo wa chakula unaambatana na uzazi. Leo hapa tunalalamika vijana wengi hawana nguvu za kiume. Inaanzia kwenye mfumo wa chakula. Kwa hiyo, watu wa mitaala andikeni pale, vijana wale chakula gani? Wewe… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Daktari.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.