Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Mwanakhamis Kassim Said

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi hii kwa kuweza kuchangia Wizara hii ya Mambo ya Ndani. vitabu vya Mwenyezi Mungu vinasema siku zote kama mwanadamu mwenzio hukumshukuru anachokifanya kwa hivyo hutoweza kumshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye nchi yetu, tunamwambia aendelee awe na subra, awe na uvumilivu, awe na ngozi ngumu, lakini awatumikie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijikite moja kwa moja kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Mimi ninazungumzia zaidi Zanzibar. Nchi yetu ya Zanzibar sasa hivi kumekuwa na magari mengi sana. Magari yanasababisha foleni kubwa sana, kama unatoka nyumbani saa tisa basi unaweza ukarudi saa 12 au saa moja. Lakini tunamshukuru Kamishna amepanga mipangilio mizuri kwa sasa, Askari wako barabarani wanafanya kazi ya Jeshi la Polisi na kuwasaidia wananchi. Ninasikitika kwa sababu ya Askari wetu hawana vitendea kazi, hili ni tatizo kubwa sana, Askari leo unamkuta ana simu ya mkononi ndiyo anawasiliana na Askari mwenziye aliyepo mbali. Hata misafara yetu kwa sasa ya Viongozi wetu Zanzibar ni mtihani, kwa sababu Askari wetu hawana vitendea kazi. Leo sisi wenyewe tunapigiana simu muda wote unaambiwa simu imezimwa au mteja yule hapatikani, je, Askari huyu Kiongozi anatoka anakwenda safari Askari ana simu ya mkononi anampataje?

Mheshimiwa Spika, hili limekuwa ni tatizo mimi limenikumba niliambiwa nataka kuvamia msafara wa Kiongozi, wakati msafara unakuja mimi niko njiani sipata kukaa popote, Askari akanisimamisha nataka kuvamia na niliwekwa kituoni muda mrefu sana. Kwa kosa la vitendea kazi la Askari wetu. Si barabarani si ofisini ni matatizo. Serikali lazima isimamie Jeshi la Polisi kuwapa vitendea kazi. Tutazunguka, tutazungumza, tutawasema Askari wetu hawafanyi kazi lakini Askari wanajitahidi kufanya kazi. Vitendea kazi hawana, muda wote, siku zote, tunawazungumzia Askari wetu vitendea hawana. Kwa nini Serikali hawatusikii? Tunakwenda kwenye vituo vya Polisi unavikuta viti vya plastic vile vya cello vimefungwa vilemba, vimefungwa kamba. Viwanda vya viti vile vipo hapa nchini, kweli Serikali haina wa kwenda kununua viti vya kupeleka kwenye Ofisi zile za Polisi? Kwa kweli hali hii siyo nzuri, hata wale wafanyakazi hatuwapi moyo wa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna askari wazuri…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa!

SPIKA: Mheshimiwa Mwanakhamis kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwakagenda.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mwanakhamis. Amezungumzia kwamba Jeshi la Polisi halina vifaa ni kweli, kibaya zaidi sehemu za mipakani Kyela, Tunduma unakuta Askari hawana gari ya doria na tunajua kabisa hapo ni mpakani. Nilikuwa nampa tu taarifa kusisitiza kwamba anachosema ni sahihi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda siyo kazi yako kujua usahihi au makosa ya mchango wa Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mwanakhamis.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vituo vya Polisi sijafika Mikoa mingine au maeneo mengine lakini utasema vyote ni Baba mmoja Mama mmoja. Ukienda kile utafikiri kama nimetoka hichi, ukienda na kile kingine utasema nimetoka kule. Lakini hali ya Jeshi letu la Polisi ni mbaya sana! siyo ofisini si barabarani, ajali zimekuwa nyingi hata Zanzibar ajali sasa hivi ni nyingi, wananchi wetu ajali ni nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Askari barabarani wazuri na kuna Askari wengine hawako vizuri wana majibu mabaya wanayowajibu wananchi, wanatujibu hata sisi, hivyo suala hili lifanyiwe kazi! Askari wana majibu mabaya barabarani hawana kauli nzuri, ni nusu tunasema wanatunyanyasa, wanatuadhibu! Mimi siyo mara moja siyo mara mbili tena niko Jimboni kwangu, nimejibiwa na Askari Traffic majibu mabaya na Askari ninamjua.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)