Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nami naomba kwanza niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Omari Kigua kwa namna ambavyo hali ipo huko mtaani ni lazima sasa Wabunge tunao wajibu wa kuishauri Serikali kuona namna bora sana ambayo tunaweza ikatusaidia kutoka katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunakubaliana kwamba miongoni mwa sababu ambazo zinachangia ongezeko hili la mafuta ni sababu za nje, lakini sisi kama nchi lazima tutafuta maeneo ya matumaini kwa watu wetu kwa sababu Serikali hii ni yao na imeahidi kuwatumikia, kwa hiyo, ni vyema itakatafuta namna bora ya kuweza kuondoa changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo ambalo ningeshauri kwanza ni sisi kwa mwezi matumizi yetu ya ndani ya mafuta ni kama lita Milioni 300, hiki ni kiasi ambacho tunakitumia ndani japo uagizaji tunafika mpaka kwenye lita Milioni 600 lakini haya mengine yanakwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuishauri Serikali kwamba katika eneo hili tungekuja na mpango wa stabilization fund ambayo itakwenda ku-stabilize bei ya mafuta. Maana yake Serikali ije iombe kibali kwa Bunge, wakakope japo bilioni 300 kwa maana kwamba angalau kila lita moja ya mafuta tuiwekee ruzuku ya shilingi 1,000 ili mafuta haya yaweze kushuka bei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii itatusaidia kwamba hatutakwenda kugusa hizi tozo pamoja na kodi nyingine zilizopo pale, kwa sababu hizi tozo zilikuwepo miaka sita iliyopita na hazijawahi kuwa tatizo. Kwa hiyo, leo siyo kwamba kwa kuwa mafuta yamepanda bei tatizo ni hizi tozo, hizi tozo zinatusaidia maeneo megine kama kupeleka umeme vijijini, barabara, maji na kadhalika. Kwa hiyo, ni lazima kuje na maarifa mengine ya ziada ambayo yataendelea kuhakikisha kwamba tozo zinaendelea kuwepo ili miradi ya maendeleo iendelee kufanyika kwa sababu ni wajibu wa Serikali kupeleka miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, bila kufumua bajeti ya Serikali ambayo imeshapita kupitia hizo tozo, solution hapa ni kuja na price stabilization fund, tuweke ruzuku katika kila lita moja ya mafuta tunaweza tukajipa kipindi cha miezi mitatu mitatu, kwamba labda miezi mitatu hii tutazame, tu-pump shilingi bilioni 300 katika mwezi wa kwanza wa uagizaji, mwezi wa pili, lakini baadaye tuangalie na hali huko duniani inaendelea vipi. Hilo ni jambo la haraka ambalo Serikali linaweza likalitazama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, jana kulikuwa na kikao kizuri sana ambacho Mheshimiwa Waziri Mkuu alikiitisha, tunampongeza kwa jitihada hizi, lakini katika kutazama sana pale sikumuona Waziri wa Viwanda na Biashara na mimi naamini yeye ndiye mwathirika mkubwa sana katika eneo hili, kwa sababu hapa eneo ambalo tunalizungumza zaidi ni kwenye usafiri, lakini tunasahau eneo muhimu sana la uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, huko kuna viwanda ambavyo vinatumia mafuta haya haya kuzalisha bidhaa maana yake bila kuangalia eneo hili la price stabilization fund, mfumuko wa bei kwenye baadhi ya bidhaa utakuwa mkubwa sana na wananchi hawataweza kuhimili hiyo hali. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Serikali kwa ujumla kwamba ni vizuri sana katika hatua hii kumshirikisha kwa dhati kabisa Waziri wa Viwanda na Biashara ili aweze kuangalia sekta hii yote ya kibiashara na viwanda kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)