Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie Kamati zetu mbili zilizowasilisha hapa leo, Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Kamati yetu ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia upande wa taarifa iliyowasilishwa na Kamati yetu ya Bajeti na hususan ukurasa wa 62 wa taarifa, kipengele kile cha 6.5. Kamati inazungumzia ujenzi wa barabara kwa mfumo wa uhandisi, usanifu, manunuzi, ujenzi na utafutaji wa fedha kwa maana ya EPC+F. Ninaishukuru sana Serikali kwamba katika mpango huu ipo barabara maarufu ya Handeni - Kibilashi - Kiteto - Kondoa - Singida ambayo nayo imebahatika kuingia humo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na barabara hizi tunazozijenga, lipo jambo moja la ajabu sana tunalifanya kama Taifa. Nchi yetu ina mtandao wa barabara wenye thamani inazofikia Shilingi Trilioni 21. Barabara za kitaifa zina kilometa 36,361 na zina thamani ya Shilingi Trilioni 18. Barabara zetu za Wilaya zina mtandao wa kilometa 143,881 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 2.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza pamoja na kuwa na asset hii kubwa ya kitaifa inayosaidia uchumi wetu, hatuifanyii matengenezo. Hivi sasa barabara zetu za kitaifa zile kubwa na ambazo ndiyo mrija wa uchumi wetu zinahitaji matengenezo yanayokaribia Shilingi Trilioni 2.4 na Serikali imekuwa ikija hapa inadai haina fedha hizo za kukarabati barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tusipoliangalia litakuja kutuingiza kwenye gharama kubwa na litakuja kufanya uchumi wetu udhoofu, wananchi wetu wasafiri kwa shida, mizigo isafiri kwa taabu, vilevile watu waliopo kwenye sekta ya uendeshaji ya usafirishaji wataendesha shughuli zao kwa gharama kubwa sana ya kununua vipuli kwa sababu ya barabara mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano, athari ambazo zinaweza zikapatikana tukichelewa kufanya matengenezo ya barabara kwa kadri ya wataalam wanavyoelekeza. Miaka kadhaaa iliyopita tuliacha kufanya matengenezo ya barabara karibia 13, tukaziacha tu mwaka wa 11, 12 nyingine mpaka mwaka wa 20 tukaziacha. Matengenezo yale yalikuwa yagharimu Shilingi Bilioni 250, hatukufanya. Tulivyokuja kufanya, tumekuja kufanya matengenezo hayo kwa Shilingi Trilioni 1.28, ndiyo kusema tulikula hasara ya Shilingi Trilioni Moja nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sielewi kwanini Serikali inajivuta vuta na sielewi kwanini Serikali inajizungusha zungusha kukarabati barabara zetu hizi za kitaifa ambazo nakwenda kuzitaja hapa ziingie kwenye Hansard kwa kumbukumbu.

Barabara ya Kibaha - Mlandizi, Chalinze - Ngerengere, Melela - Iyovu, Igawa -Uyole, Uyole - Songwe, Mlandizi - Chalinze, Same - Himo, Himo - Arusha, Rusahunga - Rusumo, Shelui – Malendi - Nzega kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Nyanguge – Mwanza – Mara - Border, Makutano - Sirari, Usagara-Mwanza, Mtwara – Mingoyo - Masasi, Madaba - Makambako, Songea -Madaba, Ipole - Miemba, Rungwa - Ipole, Nzega - Manonga, Mwanza - Shinyanga - Usagara, Uyole - Kasumulu, Kobelo - Nyakasanza, Songea - Peramiho, Mikumi - Kidatu, Lupilo - Mahende na Himo -Marangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi ukikuta barabara ya chini ina umri wa miaka 17. Barabara yenye umri mkubwa katika hizi kuliko zote ina umri wa miaka 37. Kwa nini tunakuwa hivi? Yaani ni kweli kwamba hatuoni umuhimu kabisa wa kutafuta hii Shilingi Trilioni 2.4 tukafanya ukarabati wa barabara hizi? Mfuko wetu wa Bodi ya Barabara, kwa mwaka makusanyo yake ni kama Shilingi Trilioni moja. Vyanzo vyake vya mapato ni tozo za mafuta ambazo zina-constitute karibia asilimia 97 ya fedha zote wanazopata, tozo za magari ya kigeni na tozo za kuzidisha uzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vyanzo hivi havitatosha kukarabati barabara zetu na barabara ukiitengeneza leo ukaikarabati unaipa uhai mrefu mwingine wa kuishi. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali na kwenye maazimio yetu kama Bunge tuweke maazimio kwamba Serikali lazima ije hapa na mapendekezo siku zijazo ya vyanzo vipya vingine vya mapato kwa ajili ya Bodi ya Mfuko wa Barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Barabara wanafikiria kutumia infrastructure bond kama sehemu mpya, nakubaliana nao ni chanzo kizuri, wanataka kwenda kutoza, kuweka tozo kwenye gesi asilia, kwenye yale magari ambayo yanatumia gesi asilia, siyo jambo baya. Wanataka kutoza kwenye toll bridge na wanataka kutumia hizi njia ya EPC+F.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba nilishukuru barabara ya Handeni – Kibilashi - Kiteto kwenda kwenye hii njia ya EPC+F, kuna haja kubwa kama nchi, huu mfumo tunaotaka kuuendea wa EPC+F tukaupitia upya. EPC+F ina- implication moja kwa moja kwenye Deni la Taifa. Kwa hiyo, ni vizuri Bunge lako likaambiwa, kwa mfano zile barabara Nane ambazo zimetajwa kwamba zinajengwa kwa EPC+F mpango huo umefikia wapi na implication yake itakuwaje? Watawezaje ku-spread hiyo? Kuliko tukawa tunakuja hapa kuwaaminisha wananchi barabara zinajengwa halafu hazijengwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya, nakushukuru sana, nilitamani kushauri eneo hilo, matengenezo ya barabara, Shilingi Trilioni 2.4, Serikali itoe maelezo na iweke kwenye mikakati yake kuja hapa na vyanzo vipya kwa ajili ya Bodi yetu ya Mfuko wa Barabara. Ahsante sana. (Makofi)