Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. BONIPHACE M. GETERE. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza nizishukuru Kamati zote mbili. Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nina mambo kama matatu ya kuchangia. Ningeomba nianze na jambo la NIDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Serikali ni kuwaibika kwa wananchi wake, sielewi ni kitu gani kinafanyika kwenye jambo la NIDA mimi sielewi mpaka leo. Tangu mwaka 2012 mpaka leo, miaka 11, vitambulisho vya Taifa (NIDA) ni asilimia 30.08 tu ambayo imekamlilika. Kwa mujibu wa taarifa zilizoko hapa za Kamati, watu waliotegemewa kuandikishwa ni milioni 34,080,610 na walioandikishwa na kupewa vitambulisho vya namba yaani kwa maana ya kupewa namba ni milioni 19,634,720 maana yake ni kwamba watu milioni 14,445,000 mpaka leo haijulikana wana namba au wana nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo waliopata vitambulisho ni 10,230,710 na milioni 9,400,004 hawajapata, hiyo ni asilimia 30 kwa hesabu zilizoko hapa. Sasa mimi najiuliza; vitambulisho vya NIDA ndiyo maisha ya Watanzania sasa hivi. Yaani kila kitu leo ni NIDA. Uende benki, uende kila mahali. Sasa najiuliza, hivi sustainability ya Vitambulisho vya Taifa ni ipi sasa? Kama milioni 34 imeshindikana, je, tukisema watu umri wa miaka 18 mpaka 85 pengine milioni 50 vitatengenezwa vitambulisho vya Taifa kwa miaka mingapi?

Sasa nashindwa kuelewa hivi kitambulisho kimoja cha taifa ni bei gani? Ambayo inaweza kutosha tukasema tunatoa Bilioni 3 au Trilioni 3 tukamaliza tatizo lote la vitambulisho vya taifa kwa hawa watu 34?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata zangu kwenye Kata ya Mgeta, Kata ya Zalama, Kata ya Mihigo, Kata ya Mihunyali, Kata ya Uhunyali na Kata ya Mang’uta, Nyamuswa hivyo vyote ni asilimia 25 tu wamepata vitambulisho. Kuna kata moja asilimia sijui tatu, hamna vitambulisho vya Taifa na wimbo umekuwepo, wimbo, wimbo, tutauimba mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanadai vitambulisho vya Taifa mpaka lini na taasisi zipo na fedha wanasema walishatoa zipo? Nataka kutoa ushauri kwa wale ambao tumeandikisha vitambulisho vya Taifa kwenye wilaya zetu na kwenye majimbo yetu…

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natoa ushauri kwenye majimbo yetu kwamba Serikali sasa iangalie kila jimbo kwa kila halmashauri ambazo zimeandikisha vitambulisho vya Taifa, idadi kiasi gani, wajue kwamba ni kiasi gani cha vitambulisho vya Taifa ambavyo havijatoka, waende watoe huko huko vijulikane na bajeti ijayo au Bunge linalokuja tuambiwe sasa, hili suala la vitambulisho vya Taifa lina mwisho wake, ni lini litaisha sasa? Kwa sababu sasa imekuwa kesi hii? Hatuwezi kuwa na nchi ambayo ina vitu vidogo vidogo vinaathiri maisha ya watu, wanahangaika huko, tukubaliane sasa hii kazi inaisha lini? Nadhani maazimio yaje hapo watuambie hii kazi inaisha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo lingine la mfumko wa bei. Sijui kama tunadanganyana au tunaangalia Taifa. Kutokana na covid 19, nchi zote duniani uchumi wao ulishuka kuanzia asilimia mbili mpaka asilimia saba na mfumko wa bei Nchi yetu ya Tanzania uko nafuu kidogo, sijui kama tunaangalia hili au tuna matatizo. Mfumko wa bei kwa Tanzania unalinganishwa na nani unaposema ni mkubwa? Kwa sababu uchumi ukishuka lazima kuwe na mambo kama hayo. Niseme tu kwwenye uchumi wa sasa kwa mfumko wa bei nchi yetu ni nafuu ukilinganisha na nchi zingine. Tunatazama leo hakuna mtu anadanganywa, lipo wazi hilo, hakuna haja ya kudanganyana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa hilo kwamba mfumko wa bei kwa nchi yetu mara nyingi tunasema ni vyakula, najua hali ikienda vizuri kama ninavyoiona kwenye maeneo mbalimbali kwenye halmashauri, vyakula vitakuwepo na bei ya vyakula itashuka, lakini kuna kitu nakiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mchumi lakini Wachumi wako humu wataniambia hivi kama tuna ujenzi wa miradi mikubwa kama Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mradi wa Reli, Bandari, Vituo vya Afya, Hospitali na Barabara na miradi mingine mingi mikubwa. Kama tunayo miradi mikubwa inayochukua sementi kwa wingi sana, inayochukua nondo kwa wingi sana, inayochukua mabati kwa wingi sana, inayochukua misumari kwa wingi sana, hivi tunategemea mfumko wa bei kwa vifaa vya ujenzi utashuka? Hauwezi kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoona ni kwamba lazima sasa Serikali itengeneze mpango maalum wa viwanda ambavyo vinazalisha sementi kwa ajili ya miradi mikubwa na viwanda ambavyo vitabaki kwa wananchi vinginevyo kama ni hivyo, hivyo viwanda vitakufa vyote kwa sababu vina bei, hata miradi mikubwa ina bei kubwa au nafuu kuchukua kwa haraka zaidi watauzia kwenye miradi mikubwa, wananchi wataendelea kuhangaika na bei kubwa. Kwa hiyo, tuangalie ni viwanda gani vinazalisha kwa wingi na vizalishe kwenye kiwango kinachotakiwa ili wananchi wabaki na sementi na miradi mikubwa ibaki na sementi. Kwa hiyo nafikiria kwamba kwa hilo naomba niishauri Serikali namna ya kufanya kwenye jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilizungumzie ni deni la Taifa. Ni kweli deni hili ni himilivu kama tunavyoambiwa, lakini ni himilivu mpaka lini? Ni nani atakuja kupata burden ya deni, ni lazima tujifunge mikanda kuona kama deni hilo linakua kwa kasi tuone namna ya kulipunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mchumi pia ila nataka nishauri kwenye eneo hilo, kwa mfano kama leo tunalipa madeni kwa bilioni tisa, halafu tukakopa deni la masharti nafuu, tukawa tunalipa kwa bilioni nne. Halafu ile hela tuliyokopa kwa masharti nafuu tukalipa lile ambalo lina masharti magumu halafu tukabaki na salio, labda kwa mwezi tukawa tunalipa bilioni nne badala ya kulipa bilioni tisa, kwani hapo Mheshimiwa Mwigulu wewe unaonaje hapo. Kwa nini tuwe na madeni makubwa kiasi hiki? Tuone madeni makubwa yenye masharti magumu, tukope madeni yenye masharti nafuu tulipe, yaani tulipe lile deni lenye masharti magumu tubaki na lenye masharti nafuu, ili tubaki na akiba ambayo tutafanya kazi nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)