Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwanza niseme naunga mkono hoja zote za Kamati ambazo zimewasilishwa Mezani; Kamati ya Bajeti pamoja na Kamati ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaelekeza mchango wangu kwenye Wizara ya Mambo ya Nje. Hapa nataka kuchangia kwenye diplomasia ya uchumi. Mwenyekiti wa Kamati alipokuwa akiwasilisha hoja yake, alisema kwamba tunapotaka kutekeleza diplomasia ya uchumi kwenye Wilaya zetu, hususan kwenye Halmashauri pamoja na tawala za mikoa, watendaji wetu wa Serikali hawana uelewa kuhusiana na diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii naona ni kwa sababu, zipo hata jumuiya za kikanda ambazo sisi ni wanachama huko, kumekuwa na utaratibu wa Serikali kutokurudi kutupa taarifa ya jumuiya hizo. Kwamba, kwa wakati huo malengo yale ambayo sisi tulijiunga kwenye hizo jumuiya, mpaka sasa hivi tunaendelea kunufaika na nini; na mpaka sasa hivi nini kinapaswa kuboreshwa? Wachukue maoni ya wadau? Tunapoongelea diplomasia ya uchumi ni pamoja na hizo jumuiya ambazo ndiyo zinatufanya tuwe washirika pamoja na wenzetu tunapotaka kutekeleza hiyo diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kurejea kidogo kutoka kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwenye Sura ya 7, Ukurasa wa 182, ule ukurasa wa 184 inapoongelea diplomasia ya uchumi, nitasoma kipengele kimoja tu. Kinasema kwamba, “Kulinda uchumi na maslahi mapana ya Taifa kwa kutumia jiografia ya nchi kimkakati na ushawishi wa kihistoria, hususan kwenye ukanda wa Kusini.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi katika miaka mitano ambayo tunatekeleza, inapoongelea kwenye suala la mambo ya diplomasia ya uchumi inatambua kwamba ni lazima tutumie hizi jumuiya za kikanda, lakini na historia zetu za kiuchumi huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka kuongelea sana sana kwenye hii jumuiya. Mwaka 1996 tulikuwepo kwenye COMESA, mwaka 2000 tukajitoa kwenye COMESA. Swali ambalo nataka kujiuliza hapa, sasa hivi ni miaka 20 imepita toka sisi tujitoe kwenye umoja huu ambao ulikuwa unaunganisha nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na nchi ambazo ziko Mashariki ya Afrika. Ziko baadhi ya nchi ambazo ziko kwenye SADC, lakini haziko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini nchi hizi zinapatikana COMESA tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, nchi kama Misri na Ethipia; hivi kwa mfano, unamuachaje Misri awe ni mshirika wako katika kutekeleza diplomasia ya uchumi, ikiwa Misri mwenyewe ndiye anatujengea Bwawa la Mwalimu Nyerere? Egypt wao ndio wanatujengea Bwawa la Mwalimu Nyerere? Je, zipo fursa ngapi za kiuchumi ambazo sisi tulipaswa tupate kutoka kwenye nchi ya Misri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya Misri ndio watu ambao tunawauzia bidhaa za ngozi. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba, Serikali haijawahi kuja na ripoti miaka 23 iliyopita, sisi tulivyojitoa COMESA kipindi kile kwamba, labda ada ilikuwa kubwa, tulikuwa tunalinda bandari zetu kwamba tungekuwa wanachama, watu wangepitisha mizigo yao bure; tulikuwa tunalinda viwanda vyetu vya ndani, lakini sasa hivi zama zimebadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunajitoa COMESA mwaka 2000 tuchukulie process zilianza mwaka 1999, tayari tulikuwa tuko karne ya 20, sasa hivi tunaongelea kuanzia mwaka 2000 na sasa hivi tuko karne ya 21 teknolojia imebadilika, mambo ya uchumi yamebadilika na uongozi umebadilika. Tumetoka kipindi kile akiwa Rais ni Hayati Mheshimiwa Mkapa, sasa hivi tuko na Mama Samia ambaye yeye ni mwanadiplomasia wa kwanza. Je, hatuoni tunaendelea kumpa kazi ya ziada ya kwenda kuanza kuongea na watu wa Misri na watu wa Ethiopia ili tukaenao mezani, tukubaliane baadhi ya mambo wakati tunayo platform ambayo ni COMESA ingetusaidia kuweza kushirikiana na wenzetu kuwa pamoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nauliza swali la msingi hapo juzi, Serikali walijibu kwamba, kwa sababu tuko EAC na tuko SADC hatuoni umuhimu wa sisi kuwepo tena COMESA. Sidhani kama hili ni sawa kwa sababu, hizi nchi ambazo ziko East African Community na hizi nchi ambazo ziko SADC na hizi ambazo ziko COMESA peke yake haziko kwenye nchi zote hizi mbili, tunazikuta wapi tukitaka kushirikiana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema tanataka kuweka umoja wa Afrika ili tuwe na sehemu moja ya kufanya biashara; je, tunapotaka kutekeleza haya, kama tunayo platform ambayo sasa hivi inaweza ikatuunganisha na nchi zaidi ya 20 na sisi tukawa huko ni wanachama, wafanyabiashara wetu wakanufaika, wafanyabiashara wetu wakasaidika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naona ipo haja Serikali iwe inakaa inatuletea ripoti. Hata sasa hivi tuko East African Community, lakini bado ziko changamoto nyingi sana ambazo wafanyabiashara wetu wanaendelea kupitia. Tuko SADC sasa hivi, lakini kulifikia soko la Congo tu pamoja na kwamba, Congo ni mwanachama mwenzetu kwenye SADC, lakini tunapata changamoto nyingi. Wakati mwingine unakutana na wafanyabiashara mpaka wanashauri kwamba labda tungekuwepo COMESA ingetusaidia kupunguza hizi changamoto kwa sababu, lengo la COMESA lilikuwa ni kuwepo na ushirika wa kiuchumi, kuwepo na soko moja ili kuondoa hizo changamoto za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naona kwamba, Serikali iende ikafanye tathmini itujie na majibu, katika miaka 23 ambayo tunayo mpaka tulipofikia sasa hivi, ipo haja ya sisi kurudi COMESA. Hata kama hawataona haja ya kurudi COMESA, waje watusaidie kuainisha tutambue. Pia takwimu hizo zitusaidie kwenda kule kwenye Halmashauri zetu na kwenye mikoa yetu kwa wananchi wa kawaida ambao tunataka watekeleze diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea mambo haya ya jumuiya, imeonekana diplomasia ya uchumi ni ya watu wa kaliba fulani, waliosoma tu, watu ambao wako juu, wakati watekelezaji wakubwa ni wakulima, wananchi wa kawaida. Wangefahamishwa haya mambo, yamkini wangejua kwamba, kama nchi yetu iko SADC tunanufaika na vitu gani? Kama nchi yetu iko kwenye umoja wa Afrika Mashariki tunanufaika na vitu gani? Wananchi hawana uelewa kabisa katika mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea, hapo tunaposema tuendelee kufanya tathamini zetu na Serikali iwe inatuletea taarifa kutoka kwenye jumuiya tulizonazo, mfano mzuri unaweza ukaona kwamba, unapoenda kwenye ule ukanda wa Ziwa tanganyika tumejenga bandari zaidi ya tano. Kuna Bandari ya Katanga, Bandari ya Kipili, Bandari ya Kabwe, na Bandari mpya ya Karema. Tulipokuwa tunauliza swali hapa, ni namna gani Serikali itatusaidia kuondoa changamoto ambazo tunazipata kupitia Zambia kuingia nchi ya Congo? Serikali ilikuwa inatujibu kwamba, tumeshajenga bandari na ni mkakati ambao utatufanya sisi tuingie DRC moja kwa moja bila kupitia nchi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tuna uelewa kidogo, mimi nikamfuata Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi nikamwambia Mheshimiwa Waziri majibu haya ambayo mnatupa, nafikiri Serikali haijafanya tathmini. Uende wewe na timu yako ukatembelee zile bandari ambazo zimejengwa kwenye Ziwa Tanganyika na uende upande wa pili ambao ni wa Congo, ili ukaone kama jambo hilo linatekelezeka ndani ya mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipoenda, amekuja kutupa taarifa. Unagundua kabisa kwamba ni kitu ambacho hakitafanyika mwaka huu wala hakitafanyika mwakani ili sisi tuweze kupitia Ziwa Tanganyika kuweza kufika Congo, especially, kufika Lubumbashi ambayo ndiyo miongoni mwa majimbo ambayo yanafanya vizuri sana kibiashara ambapo hata sisi Watanzania wengi wana-target kupeleka mazao yao huko. Ni kitu ambacho sio cha sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wao kwa kwenda kufanya tathmini, na kufanya takwimu ikatusaidia wao kuja na njia mbadala wajue tukitaka kuingia Congo kuna namna ambavyo hatuwezi kuikimbia Zambia. Aidha, sisi turudi COMESA ili kurahisisha kuondokana na hizo changamoto au kutafuta njia nyingine mbadala namna gani sisi tuisaidie nchi ya Congo kujenga barabara kwao ili tuweze kupita kutoka Ziwa Tanganyika kwenda moja kwa moja. Hayo yote yamefahamikaje? ni baada ya viongozi wetu wa Serikali kwenda kufanya tathmini na kuleta ripoti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo mambo ya kuendelea kukaa. Kama tulishajitoa COMESA sasa hivi tuko wakati mwingine, vita ya uchumi ni kubwa, kila mtu analiangalia soko la Congo. Nasi kwa kutumia soko la Congo tu peke yake linaweza likatuongezea mapato kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)