Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia machache kuhusu taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo na Huduma za Jamii.

Awali ya yote natoa shukrani sana za pekee kwa Mheshimiwa Dkt. Stanslaus Nyongo pamoja na Wajumbe wa Kamati hii ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa kazi nzuri waliyoifanya. Amewasilisha taarifa hapa na kwa uongozi wake makini mpaka hapa tulipo, Wizara hii imetimiza sasa takribani mwaka mmoja ikiwa na utekelezaji kama uliowasilishwa.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya na uongozi wake kwa kuiunda hii Wizara na kuweza kuipatia fedha katika mtiririko mzuri hadi katika miezi sita ya kwanza karibu asilimia 50 ya fedha zilishapatikana na kazi ikafanyika kama ilivyowasilishwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maeneo yote ya utekelezaji naipongeza Kamati kwa kuibua changamoto ambazo baadhi wameziripoti hapa na nitazazisemea baadhi ambazo ni za msingi sana katika kuendelea kuifanya Wizara hii kuwa na utekelezaji mzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upungufu wa watumishi, tutaendelea kuomba nafasi za ajira kwa kadri ya uwezo wa Serikali. Hata hivyo, tutakuja na ushawishi ili sekta zote sasa za binafsi pamoja na za umma zione umuhimu wa kuajiri hizi kada za maendeleo ya jamii. Kwa sababu katika zama za sasa na changamoto tunazokwenda nazo kiuchumi, Maafisa Maendeleo wanahitajika katika kila taasisi, lakini maafisa Ustawi wa Jamii nao wanahitajika kila taasisi. Yaani ukiwa na kundi la watu bila ustawi wa jamii matatizo yake ndiyo kama haya tunayoyaona, kwa sababu wale watu wanakuwa bado hawajaandaliwa kubadilika fikra waende na nyakati za sasa.

Mheshimiwa Spika, tunaandaa pia sheria ya taaluma hizi za maendeleo na ustawi wa jamii ili waweze kusajiliwa kama wanataaluma, waweze pia kupata fursa ya kufungua huduma binafsi kama ilivyo huduma za elimu na afya hivyo kuongeza wigo wa wataalam hawa na upatikanaji wa huduma, wananchi waendelee kunufaika sambamba na ajira za Serikali ili walioko kule sokoni waweze kupata hizi ajira.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ukatili wa kijinsia na kwa watoto. Imeibuka hapa hoja nzuri sana ya masuala ya ukatili hasa kwa Watoto na pia kwa jinsia, imeonekana na wanaume pia ni wahanga.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee kwanza kwa Watoto; kwa upande wa watoto na wanawake tunao mpango wa Serikali tangu mwaka 2017, tulikuwa tunatekeleza, unaitwa Mpango Kazi wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto. Mpango huu umejielekeza kuangalia mambo mtambuka yakiwemo masuala ya kuinua uchumi wa kaya, jambo ambalo Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelitilia mkazo sana, kwa sababu wanawake walikuwa wameachwa nyuma sana kama ilivyoelezwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa.

Mheshimiwa Spika, hatuna maana ya kuwaacha wanaume nyuma, tuna maana ya kupiga mbio ili tuvute kundi la akinamama lisogee na wenyewe juu ili huu ukatili unaopatikana kutokana na uchumi, wenyewe urudi chini. Hata hivyo, tunazo programu zingine mbili ambazo zinawalenga jinsia zote wa kiume na wa kike. Moja inamlea mtoto kuanzia miaka 0-8 na nyingine inachukua kuanzia miaka 10-19, kuwaandaa hawa vijana kuanzia umri wa awali mpaka wawe vijana balehe wavuke salama. Huku tukiangazia kuwafundisha elimu, kuepuka magonjwa, lishe nzuri pamoja na fursa za uchumi. Kwa hiyo akinababa tunaomba mtupe nafasi kwanza tuwasogeze sogeze akinamama, mliwaacha nyuma sana, hatuna maana tutawarudisha nyuma, tutakwenda pamoja kupitia hizi programu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mpango huu wa kutokomeza sasa ukatili mpaka kule vijijini, kuna Kamati za Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto. Hata hivyo, hawa watoto ni wa kiume pia mle ndani. Sasa suala la akinababa kwamba wanakatiliwa, tunawakaribisha kwenye madawati ya jinsia. Yapo kwenye vituo vyote vya polisi. Ukiona umepigwa na umeonewa karibuni. Sasa hivi tuna mitandao ya akinababa wanaonyanyaswa na wake zao. Tukajiunge huko tupaze sauti, tufanye utafiti vizuri tuje na program baadaye ambayo inasheheni data za kitaalam. Maana hamjitokezi, tunashindwa kujua ukubwa wa tatizo. Kwa hiyo tunawakaribisha kwenye madawati ya kijinsia.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kwamba vita ya kupinga ukatili haitatokea tu kwa mikakati, sera na sheria nzuri, bali kwa mabadiliko ya kifikra, tunaposema tuwe karibu na watoto, tuwe karibu na watoto, tunapoimbaimba don’t touch here and there, sio kwamba tunachekesha chekesha. Tuimbe wote ili watoto waimbe na sisi, waelewe ishara kama unavyomwambia pale pana nyoka haendi, aelewe kwamba hata maeneo haya na haya mtu akikugusa ukatae. Hatuchekeshi tuko serious, kuwa karibu na watoto tuunge mkono. Nawapongeza wotu wanaoimba don’t touch, moto uendelee mpaka watoto tucheze nao, turuke nao sarakasi, ukutiukuti ili akiguswa kama ambavyo akiona nyoka au simba anakueleza. basi pia iwe ni ishara ya yeye kwenye fahamu zake kuona kwamba hili ni hapana nimwambie baba na mama.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, nashukuru sana kwa Kamati, mapambano yanaendelea, ukatili Tanzania haukubaliki, ahsante. (Makofi)