Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia. Awali ya yote napenda sana kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya, pia napenda kuipongeza Wizara ya Maendeleo, Jinsia na Watoto pamoja na Waziri wake na Naibu kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo utajielekeza katika suala la ukatili wa watoto. Suala la ukatili kwa watoto limekuwa ni changamoto kubwa sana katika Taifa letu na limekuwa likiongezeka mara kwa mara. Kama tunavyofahamu watoto ndiyo Taifa la kesho, watoto wanaandaliwa kuanzia wanapokuwa tumboni, tangu mama anaposhika mimba na maendeleo ya mtoto pale ndiyo yanapoanza. Mimba ikiwa haitatunzwa vizuri hata ukuaji wa huyo mtoto atakapozaliwa hautakuwa mzuri. Mimba inabebwa vizuri na mwisho mtoto anazaliwa, lakini sasa anapofika duniani na kuanza maisha anakutana na changamoto. Hili ni jambo la kusikitisha sana na katika Kamati yetu ya Huduma za Jamii tumeliangalia suala hili la vitendo vya ukatili wa watoto na jinsi ambavyo linaendelea katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa takwimu za Polisi ambazo Wizara imetupatia ya mwaka 2021, inaonesha kwamba, ripoti ambazo zimeripotiwa Polisi japokuwa hizi ripoti zilizoripotiwa Polisi wote tunaamini kwamba zitakuwa siyo zote zilizoripotiwa, lakini kwa hizi chache ambazo zimeripotiwa bado zinatosha kutupatia picha halisi ya ukubwa wa hili tatizo. Kwa mfano, matukio yaliyoripotiwa jumla yake ni 11,429 ambayo hayo yametolewa taarifa katika vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Spika, matukio yaliyotolewa taarifa ni ya ubakaji ambayo ni matukio 5,899, mimba kwa wanafunzi ni matukio 1,677 na ulawiti ni matukio 1,114 pamoja na kuzorota kwa masomo ni 790 na mashambulio ya mwili ambayo ni 350. Hizi ni zile ripoti ambazo zimeenda kuripotiwa katika vituo vya Polisi, lakini tunajua kabisa katika utamaduni wetu wa Kiafrika tofauti na tamaduni za nchi za nje ambapo mtoto hata anapopigwa kibao na mama yake anachukua simu palepale mezani na kuwapigia ustawi wa jamii na ustawi wa jamii unamchukua na kumpeleka katika vituo vya kulelea watoto na huyo mzazi hatamwona mtoto wake, hilo ni tofauti na kwetu kwa hiyo wazazi wanaogopa sana kuwafanyia ukatili watoto.

Mheshimiwa Spika, katika nchi zetu za Kiafrika na Tanzania ikiwemo, vitendo vya ukatili kwanza tafsiri yake ni ngumu, kumchapa mtoto kama Waziri Mkuu alivyosema leo na mimi pia nilikuwa nataka kusema, mimi kiboko hapana! Kiboko siyo adhabu kwangu, mtoto tiba yake ni kuongea na mtoto lakini sasa katika nchi yetu, tunaona kwamba familia hazijachukua nafasi yake. Ubakaji wa watoto takwimu zake hatuna, kwanza ubakaji umeanzia wapi kwa mtoto? Mtoto wa miaka mitatu, mtoto wa miezi sita amebakwa imeanzia wapi? Huu ni utamaduni wa wapi? Mimba za wanafunzi! Suala kubwa ambalo mimi hapa naliona ni kwamba wazazi hatujachukua nafasi zetu kuongea na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata mtoto akizaliwa tu pale unapokuwa mama unamnyonyesha, unapoongea na mtoto anakuelewa hizo ni tafiti zinavyoonyesha. Mama unapongea na mtoto na mtoto anacheka ananyonya anakuangalia unamsemesha anaelewa! Kwa hiyo, hata baadae atakapokuwa na mwaka wa kwanza na mwaka wa pili unavyoendelea kuongea naye unasogeza ukaribu wa yule mtoto, kwa hiyo inakuwa ni mwanzo wa kuwa karibu na watoto.

Mheshimiwa Spika, suala kubwa ni kuvunja ukimya kwa watoto, tutakapovunja ukimya kwa watoto, watoto wakiwa karibu hakuna jambo watakaloficha. Kama katika nchi zilizoendelea, mtoto anaweza kupiga simu yaani mama yake amempiga tu kibao kidogo tu ananyanyua simu, anamwambia mama I will call the social worker and she/he will call the social worker kwa mama yake aliyemzaa, hivi kwetu Watanzania tunakwama wapi? Tukianza kuwazoeza watoto wetu kuongea mambo mazuri tu, mambo ya kawaida, mambo ya ngono, mambo ya sehemu za siri, mambo ya vitu vingine, watoto wanaelewa na watatupa taarifa na huu ukatili mwingi utapungua. Tunakuja kusubiri mtoto amelawitiwa mara thelathini, mara arobaini mpaka ameshakubuhu, siku umemkamata ndiyo mama au baba mbio unakwenda Polisi kuripoti, hasa unaenda kuripoti nini? Baada ya muda tena, na wewe mwenyewe mzazi ni maskini unapenda pombe, unakuta tayari.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi labda napenda kusema tu, Serikali umefika muafaka wa kuchukua hatua. Tukae chini tuchukue hatua madhubuti ya kuhakikisha kwamba tunakuwa karibu na watoto na vile vile tuhakikishe tunawaweka watu ambao ni wataalamu wa kuweza kuongea na watoto pamoja na wazazi wao. Tuimarishe maongezi kati ya watoto na wazazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili pia hizi sheria zirekebishwe. Once sheria imeshakuwa imewekwa mezani wazazi wasije wakasema aah! tumeshaelewana tunaomba tu hili la kijamii tukalimalizie nyumbani. Haya masuala ya kwenda kumalizia nyumbani yanawasababishia watoto ukatili; nao hao wakiwa wakubwa watafanya ukatili kwa watoto wao. Kwa hiyo, jamii itakuwa na mwendelezo wa ukatili miaka na miaka na haitaisha. Tukianza kuziba mwanya huku chini tutaweza kurekebisha hii tabia ya ukatili kwa Watoto.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho niseme kwamba, elimu itolewe hata kwa hao waathirika. Mtoto anapoathirika hili linabaki kuwa donda linabaki kwenye moyo wake na halitaisha; na ili liweze kuisha ataendelea kulipiza. Kwa hiyo, atakapokuja kuwa mtoto mvulana anaanza darasa la pili la tatu la nne atakuwa anafanya vile akifikiria kwamba anajifariji kumbe naye anaongeza tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi napenda kuishauri Serikali hili jambo tuliangalie vizuri sana. Tusilichukulie tu ukatili, ukatili, ukatili chanzo cha ukatili ni nini kwenye jamii yetu? Na katika nchi zilizoendelea wamefanya nini kupunguza ukatili? Nchi ya Norway ambako mimi nimesoma hivi vitu havipo, na watoto wakifanyiwa hivyo hata ukimuangalia tu anakuambia why are you looking at me? Mtoto mdogo anakuambia why are looking at me? Yaani kuonesha kwamba anajielewa. Kwa hiyo, watoto wetu wa Kiafrika tuwajengee kuanzia wakiwa wadogo wajielewe, wajenge ile uwezo wa kushangaa mtu anapotaka kumwambia lolote sio hii ya kumwambia aah wewe ni mjomba, wewe ni mtoto wa kaka yangu, wewe ni mdogo wangu ngoja nikuogeshe tulale pamoja, mtotoo anaona kama ni kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tunaomba Serikali ichukue sheria kali sana na kuhakikisha kwamba elimu inatolewa ya kutosha kuweza kuhakikisha ukatili kwa watoto unaisha ili tujenge jamii inayokuja tofauti kabisa, na hii iwe ni historia ya masuala ya ukatili kwa jinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Dkt. Paulina nilikuwa najiuliza hapa, kwa hivyo kumchapa mtoto kibao ni ukatili?

Mheshimiwa Paulina, kumchapa mtoto kibao ni ukatili? Inabidi aende polisi? (Kicheko)

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, nimetolea mfano wa nchi zilizoendelea, lakini mimi sipendi kuchapa mtoto kwa ujumla, kibao, kiboko naona kwamba ni ukatili kwa sababu hata huo mkono utakao mchapa unaweza ukamsababishia kutokusikia maisha. Kwa hiyo, sijui labda umetoka kwenye stress zako, sio wewe Mheshimiwa, samahani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mtu ametoka kwenye pombe zake kwenye stress zake amegombezana na hawara zake anamchapa mtoto kibao, hajui ule mkono aliomchapa nao amemchapa kwa kiasi gani, atamsababishia kilema cha maisha, nilikuwa namaanisha hiyo. (Makofi)