Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu kwa njia ya maandishi pamoja na kwamba nimeomba kuchangia lakini napenda kuwasilisha mchango pia kwa sababu ya ufinyu wa muda.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama chetu Chama cha Mapinduzi kwa usimamizi imara kabisa wa ilani, mengi yanayofanyika majibu sisi sote na wananchi ni mashuhuda, jimbo la Ndanda lenye kanda mbili hivi sasa kuna miradi mingi inaendelea tena kwa kasi ambayo haijawahi kutokea, miradi ya maji, zahanati, vituo vya afya na mingine mingi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mazuri hayo kuna mambo machache ya kurekebisha; kwanza ni suala la Mtwara Corridor; nini msimamo wa Serikali kwenye utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao kimsingi ni mhimili mkubwa sana kwenye ujenzi wa uchumi wa Mikoa ya Kusini, kwani inagusa mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma, uendelezaji wa bandari ya Mtwara na ustawi wake, reli ya Kusini na maboresho ya barabara Mtwara Mbambabay.

Mheshimiwa Spika, pili, tumeona mambo mengi mazuri ambayo ni kama maono ya binafsi ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, hivi ni kwa nini Serikali isifikirie kuona namna ya kuwa na Sheria ya Kilimo kwa ajili ya kulinda mawazo mazuri yote yanayoletwa hapa ndani na Waziri wa Kilimo, kwa sababu siku akibadilishwa inawezakana akaja Waziri mwingine akawa naye na maono yake, lakini mazuri yote kama yatalindwa kisheria basi yatakuwa na tija na muendelezo kwa ajili ya manufaa ya Taifa hili. Tumeona namna alivyohangaika awamu hii Wizara ya Fedha kuhakikisha pesa ya export levy inarejeshwa kwa wakulima na amefanikiwa, sasa ije kwenye Finance Bill na liwe jambo la kudumu badala ya kuwa ni la matakwa ya mtu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na udhaifu mkubwa sana kwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho, tumekuwa na kikao na wewe hivi karibuni, tumeongea suala la matumizi mabaya ya ofisi, naamini pia Mwenyekiti wa Bodi anafanyia kazi mambo ambayo tuliyasema wakati wa mkutano huo, lakini kwa kifupi waangalie namna anavyofanya kazi zake, kuna watu wamekuwa na madai ya muda mrefu ya bonds akiwemo ndugu Kapwapwa kwa jina la Kampuni TF Commodities Ltd. ambaye kwa sasa anadaiwa na benki hivyo naye anakusudia kuishtaki CBT. Nilitoa mapendekezo kama amekuwa Kaimu kwa miaka mitatu au athibitishwe au aondolewe kwani bodi iliyoko sasa ni mpya.

Tatu, kumekuwa na suala la namba za vijiji kwa muda mrefu sasa, vijiji vya Mkalinga, Sululu ya Leo, Chipunda na vingine vingi, hivi kuna ugumu gani kutoa hizo namba za vijiji wakati vitongoji hivyo vimetimiza vigezo vyote, kuna maombi pia ya kata ya Nambawala ili wananchi waweze kujiletea maendeleo yao.

Mheshimiwa Spika, kuna suala pia la mgogoro wa ardhi katika Kata ya Moanyani, umekuwa ni mgogoro wa muda mrefu kama Wizara ya Mambo ya Ndani (Magereza) hawana uwezo wa kulipa fidia wananchi basi watangaze na kuliachia eneo hilo kwani kumekuwa na migogoro kila mara ya maeneo hayo. Bodi pia ina migogoro na wazabuni wa pembejeo kwenye zao la korosho mambo ambayo yanahitaji akili kubwa zaidi kuyatatua kabla hayajaleta migogoro mikubwa uko mbele.

Nne, kuna suala la inflation, Serikali iangalie tena uwezekano wa kulirekebisha suala hilo kwani linaleta mzigo mkubwa sana kwa wananchi sambamba na bei ya mafuta, kwani sehemu karibu nusu ya bei hizo ni tozo, kwa hiyo Serikali iliangalie vyema.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu.