Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Pia naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri pamoja na wataalam wote walioandaa hotuba hii. Hali kadhalika, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana ya kutuletea maendeleo Watanzania. Mwenye macho aambiwi tazama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia kuhusu mfumuko wa bei ambayo ipo ukurasa wa 17 na upandaji wa bei katika hotuba hii, ambayo ipo katika ukurasa wa 82. Ni ukweli usiopingika kuwa bidhaa nyingi zimepanda bei kutokana na masuala mbalimbali, lakini baadhi ya wafanyabiashara hupandisha bidhaa hizo bila kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia upandaji wa vifaa vya ujenzi ikiwemo bidhaa ya nondo. Awali nondo milimita 12 ilikuwa ikiuzwa kati ya shilingi 16,000 mpaka shilingi 17,000, lakini sasa hivi nondo hiyo imeshapanda na kuuzwa kati ya shilingi 27,000 hadi shilingi 28,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna chuma chetu kule eneo la Liganga, sasa ili kuweza kupata bidhaa hii kama malighafi yetu wenyewe, ni budi Serikali ikaweka utaratibu au mkakati mzuri wa kuhakikisha kwamba chuma chetu cha Liganga kinapatikana kwa wingi ili kusudi tuweze kupata malighafi ambayo itapunguza baadhi ya bei ikiwemo na bei ya nondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 10 wa hotuba hii, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu ujenzi wa madaraja makubwa na ujenzi wa barabara. Niendelee kuipongeza Serikali, lakini sisi wana-Dodoma tuna kila sababu ya kuishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo makubwa ambayo tumefanyiwa sisi katika suala zima la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukurani hii, naiomba Serikali yetu sikivu itusaidie katika ujenzi wa daraja la Godegode. Daraja hili kwa kweli limekuwa ni kero sana wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa. Kwa kweli pindi inapofikia mvua, daraja hili mawasiliano yanakatika kabisa. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu Tukufu, hili daraja la Godegode hebu lipewe kipaumbele ili tuwanusuru hawa wananchi wa Mpwapwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna korongo kubwa ambalo linaendelea katika Mji wa Mpwapwa, nalo pia limekuwa ni hatari kwa maisha ya wananchi wa pale Mpwapwa. Basi naomba hatua za haraka zichukuliwe ili kusudi tuweze kukinga badala ya kutokea madhara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, aliweza kuzindua barabara ya mzunguko tarehe 9/2/2022 yenye kilomita 112.3 na hatimaye ujenzi ule umeanza. Sisi wana-Dodoma kwa kweli tunampongeza sana; na kwa niaba ya wananchi wa Dodoma naomba niendelee kumpongeza sana Rais wetu kwa sababu hii inaendelea kuifanya sura ya Makao Makuu iweze kuonekana katika Mkoa wetu wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilete ombi kwa Serikali kwamba kuna upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya Arusha - Kibaya - Kongwa, lakini mradi huu haujatangazwa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba, kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu na fursa ni nyingi sana na tunatamani Dodoma ifunguke kweli kweli, natoa ushauri kwa Serikali, itakapotangaza mradi huu wa hii barabara, basi ujenzi huu uanzie kutokea Wilaya ya Kongwa na hatimaye iweze kwenda Kibaya hadi Arusha. Naamini kwa ombi hili Serikali italichukulia uzito wa pekee ili kusudi sisi wananchi wa Dodoma iweze kutufungulia maeneo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa TARURA una barabara ambayo ni kiungo kikubwa kati ya Kondoa - Tumberu na Thawe. Barabara hii nayo inahitaji sana kutengenezwa kwani inatakiwa ipitike kipindi chote, lakini wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakipata adha kubwa sana kwa sababu barabara hii bado ina shida. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kama itawezekana, basi Serikali nayo ione kwamba sisi wana-Dodoma tunaleta special request ili kusudi iweze kupatikana pesa iweze kujenga barabara hii ili wananchi wa Dodoma waweze kupata urahisi wa kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba nikumbushe ujenzi wa barabara ya Ihumwa – Hombolo, Ihumwa – Stesheni SGR. Hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Marehemu Rais Dkt. John Pombe Magufuli, basi tunaiomba Serikali iendelee kutusaidia kutekeleza mradi huu katika bajeti hii kama itawezekana ili tuendelee kuifungulia Dodoma kwa suala zima la usafiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijatenda haki kama nisipo zungumzia kuhusu suala zima la zabibu, kwa sababu zabibu ni nembo ya Dodoma, zabibu ni biashara Dodoma, zabibu ni siasa Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo, bado zao la zabibu lina wazalishaji. Wananchi wanaozalisha wapo, lakini tatizo ni kwamba hakuna soko la uhakika la zabibu. Kwa hiyo, nilikuwa naikumbusha Serikali ione namna bora ya kusimamia mkataba wa kilimo wa zao la zabibu ili kusudi tuweze kupata uhakika wa soko kupitia TBL ambayo ni kampuni tanzu ya TBL.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu waraibu ambayo pia ameizungumzia Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake. Kwanza niendelee kuipongeza Serikali kwa kuanzisha kliniki zinazohudumia waraibu wa dawa za kulevya, maarufu tumekuwa tunawaita mateja, lakini hilo siyo jina zuri, lakini wale ni wagonjwa, kwa sababu wana tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia program ya kukuza ujuzi na kutoa mafunzo kwa waraibu 200, hii ni hatua kubwa sana kwa sababu Serikali inaona umuhimu wa hawa watu na hawa ni binadamu na wana haki zote kama binadamu yeyote yule katika nchi yetu hii. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba kupitia program hii, ni vizuri hawa waraibu wakapata mikopo ya Halmashauri 4, 4, 2; yaani wale waraibu ambao wameshapata dawa, wamepitia methadone, wameweza kupona na wamekuwa katika hali ya kawaida, basi Serikali ione jinsi gani ya kuwaingiza katika program mbalimbali waweze kupata mikopo na fursa mbalimbali ili mwisho wa siku waweze kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya maeneo tumeenda tumewakuta hawa vijana ambao wameacha kutumia madawa ya kulevya na wameanzisha familia zao; na wamekuwa ni raia wema kabisa, lakini hawana miradi ya kufanya. Kwa hiyo, naiomba Serikali ione namna ya kuwabaini na kuweza kuwasiadia ili mwisho wa siku waweze kurudi katika mazingira yao ya kawaida, kwa sababu hawa vijana wengine wanaingia kwenye uraibu kwa sababu ya kukosa kazi au kukosa shughuli ya kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuhusu hawa waraibu, wale ambao wamezidi miaka 15, tunaona kabisa kwamba kama ni kundi la vijana, wao wana fursa; wanawake wana fursa, vijana wana fursa, lakini wale waraibu wanaume ambao wana zaidi ya miaka 35, bado naomba Serikali ione namna bora ya kuweza kuwasaidia ili kusudi na wao waweze kufaidi hizi fursa ambazo ziko hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, niliomba pia nizungumzie kuhusiana na suala la UKIMWI; hasa nilipenda kuzungumzia kuhusu tohara ya kitabibu. Inaonyesha kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)