Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia taarifa ambayo imewasilishwa na Kamati yetu nikiwa kama Mjumbe wa Kamati. (Makofi)

Kwanza naunga mkono hoja hiyo na ninaliomba Bunge lako tukufu kwa namna ambavyo tumefafanua na kulielezea Bunge lako kuridhia nyongeza inayoombwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, najisikia fahari kusimama ndani ya Bunge hili na mimi kuendelea kuunga mkono taarifa hii ya Serikali kwa mkopo ambao uliwasilishwa kwa ruhusa yako kwenye Kamati yetu. Kwa mara ya kwanza tulipata fursa ya kujadiliana vizuri na Serikali naipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuridhia pia mapendekezo yaliyowasilishwa na kamati yetu na hatimaye leo tunaona kazi ambayo imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa weledi kwa maono yake kwa kujenga hoja hatimaye tumefanikiwa kupata mkopo huu ambao kwa hakika ninaamini kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha muda mrefu Bunge lako linapata fursa ya kujadili mapendekezo ya nyongeza ambayo kazi tumeshaanza kuiona katika maeneo yetu na kwa kuzingatia mkopo huu hauna riba na utalipwa baada ya miaka kumi kwa kweli tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais na tunamtakia kheri na tunamuomba aendelee kusafiri maeneo mbalimbali ili tuweze kupata mikopo ya aina hii ichochee uchumi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaposimama kuunga mkono hoja iliyowasilishwa leo nitatambua Watanzania wengi kupitia kwa mfano makundi mbalimbali, mama ntilie, mafundi ujenzi katika maeneo yetu yalikojengwa madarasa 15,000, walipata faida na pesa hizi walienda kuchochea uchumi. Ninaposimama leo hapa ninawakilisha wanawake ambao watakwenda kutuliwa ndoo kichwani kwa miradi zaidi ya 172 ya maji vijijini ikiwemo miradi tisa ya Mkoa wetu wa Pwani na kiasi cha shilingi bilioni 3.7 ambazo tumezipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaposimama hapa ninasimama kwa niaba ya Wazazi wa Wanafunzi waliopelekwa madarasa 15,000 wamepunguza msongamano, lakini hata hivyo umeinua kiwango cha taaluma kwa sababu wanafunzi hawa walipokuwa wanachaguliwa awamu kwa awamu ni wazi kwamba wengine walikuwa wanaachwa nyuma kwa kiwango cha taaluma. Lakini ninaposimama hapa ninafurahi mkopo huu umekwenda kuchochea huduma za afya kwa kupitia wodi za dharura zitakazojengwa zaidi ya 113, itawezesha kupunguza vifo pia vya kinamama wajawazito, vitawawezesha pia kuokoa vifo vitakavyotokana na ugonjwa wa Covid. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninaposimama hapa pia ninafurahi kwa hatua ya mara ya kwanza kwa hospitali zetu za rufaa zinaenda kupatiwa CT-Scan zaidi ya 29 jambo ambalo haijapata kutokea. Ninaposimama hapa ninatambua kwa dhati namna ambavyo hospitali zetu nyingi zilikuwa hazina x-ray za kisasa, lakini leo hata Mkoa wa Pwani tumepata x-ray mbili kwa Wilaya ya Kibiti na Halmashauri ya Chalinze, lakini kanakwamba haitoshi watoto wetu wa kundi maalumu wenye ulemavu wamepata mabweni zaidi ya 50; lakini ninaposimama hapa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutimiza ahadi yake ya kuendeleza miradi iliyoazishwa Awamu ya Tano kwa kuliomba Bunge liidhinishe mkopo wa bilioni 693 kwa ajili ya kuendeleza kipande cha Reli cha Manyoni - Tabora, niwazi kwa kweli ni nia ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita ndani ya miezi 10, shilingi trilioni 1.3 zitakwenda kuchangia uchumi wa Taifa letu na kwa kweli tumeona kwa hatua ya Mheshimiwa Rais za kukubali nchi yetu ipambane na UVIKO kwa mbinu za ndani, lakini kwa mbinu ambazo mataifa mengine yametumia tumeona faida yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naliomba Bunge lako tukufu kwa heshima na taadhima liridhie nyongeza hii ya Serikali, napongeza Wizara ya Fedha chini ya Waziri Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu, lakini kipekee Gavana wa Benki Kuu kwa tuzo aliyoipata ambayo imeitangaza nchi yetu namna ilivyochukua hatua mbalimbali kulinda uchumi wetu na tumeona pamoja umekua kwa kiwango cha 4.8 lakini ni juu ya lengo ambayo ya kimataifa, walidhani ungekuwa kwa asilimia 2.5. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza sana kwa kazi nzuri, umetengeneza leo historia ya kuidhinisha nyongeza hii ambayo kwa miaka mingi ya Bunge haijapata kutokea nyongeza ambayo kazi yake imeonekana na naiomba Serikali ishungulikie zile changamoto, mfano VAT hizo na masuala mbalimbali ya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninaliomba Bunge lako tukufu tuidhinishe nyongeza hii. Ahsante sana. (Makofi)