Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

MHE. DKT. RITHA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kuhusu Azimio la Bunge Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Kuhusu Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Kilimo na watendaji wote kwa kuwasilisha Azimio hili ili tuweze kulijadili. Nimpongeze pia Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Kilimo na Wajumbe wa Kamati ya Kilimo kwa maoni na ushirikiano wao walioutoa kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa mmojawapo wa wajumbe wa Kamati, kama Kamati tuliweza kukutana na wataalamu mbalimbali ili kuhoji na kujiridhisha. Pia, tuliweza kupitia na kuchambua na kuona faida na hasara za kupitisha Itifaki hii. Zipo baadhi ya faida tuliona kama kukuza na kuimarisha biashara ya chakula na mazao ya kilimo na mifugo; kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha mipakani; kuongeza hamasa miongoni mwa wakulima katika kuongeza viwango vya ubora wa bidhaa na mengine mengi ambayo Mheshimiwa Mwenyekiti wetu amewasilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uridhiwaji wa Itifaki hii, Kamati ilibaini upungufu katika mifumo ya usimamizi wa taasisi mbalimbali zinazohusika na afya ya mimea. Ni vyema Serikali ikazingatia ushauri uliotolewa na Kamati ili kuondoa upungufu huo. Pia, kuandaa sera mahsusi inayosimamia usalama wa chakula na kuhuisha sheria mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kuhuisha sheria mara kwa mara kwa sababu kuna wakati tulifanya ziara Kanda ya Ziwa na yapo mapungufu ya kisheria ambayo tuliyaona mfano katika Ziwa Viktoria, kulikuwa kuna sheria ambazo zimewekwa kwa ajili ya nchi wanachama lakini tuliona zile sheria kwa upande wetu zilikuwa hazihuishwi mara kwa mara na kusababisha kwamba nchi yetu pamoja na kuwa nchi yetu ndiyo inamiliki eneo kubwa katika Ziwa Viktoria lakini wenzetu walikuwa wanapata faida kutokana na zile sheria ambazo zilikuwa zinawabana wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hasara iliyokuwa inapatikana ni kwamba wafanyabiashara wengi walifunga viwanda na kwenda kufungua viwanda Uganda na Kenya. Kwa hiyo, ilikuwa inasababisha nchi yetu kukosa viwanda na ajira kwa sababu kufungwa kwa viwanda vijana wetu wengi walikuwa wanakosa ajira. Kwa hiyo, naomba tunaporidhia Itifaki hii Serikali ijipange kuhuisha sheria mara kwa mara na iwe flexible ili wenzetu wanapohuisha sheria zao na sisi tuhuishe za kwetu kwa ajili ya manufaa ya nchi yetu na wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Itifaki hii imezingatia maslahi mapana ya Taifa na nchi yetu ikiwa ni mnufaika mkubwa wa Itifaki hii kutokana na kuwa ndiye mzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na mifugo miongoni mwa nchi wanachama. Pamoja na kuwa tulikaa miaka nane bila kuidhinisha Itifaki hii, sasa imefika wakati muafaka nchi yetu iweze kuidhinisha itifaki hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)