Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwanza kwa kumshukuuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya hatimaye nimeweza kusimama katika Bunge lako Tukufu kutoa mchango wangu. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mwigulu Nchemba na Naibu wake kwa kazi nzuri ambazo wamezifanya katika Wizara hii ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kwa kazi nzuri ambazo amezifanya toka amechukua madaraka ya kuongoza nchi yetu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia nimpongeze kwa namna ambavyo tumeona ana nia ya dhati kabisa ya kuhakikisha miradi ya kimkakati ambayo walianzisha pamoja na Mheshimiwa Hayati, ana nia ya kuimaliza lakini pia na kuanzisha miradi mipya ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na suala la Madiwani. Naomba pia ku-declare interest, mimi nilikuwa Diwani kwa miaka 10 na nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa miaka 10. Moja ya changamoto ambayo Madiwani walikuwa wanapata ni suala la posho hizi za mwezi. Serikali kwa kuamua sasa kuwalipa moja kwa moja Waheshimiwa Madiwani, kwa kweli watakuwa wamewasaidia sana. Wakurugenzi walikuwa wana-take advantage ya kuwalipa Waheshimiwa Madiwani kwa namna wanavyotaka wao na kama kuna mambo ambayo yanataka kujadiliwa kwenye vikao, Madiwani hawana sababu ya kupinga maamuzi ya Mkurugenzi kwa sababu wanajua mwisho wa siku Mkurugenzi hatatulipa posho zetu. Sasa kwa kuwalipa moja kwa moja, wataenda kutenda haki kwenye vikao bila kumwogopa mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo kubwa hapa ni kuongezewa posho. Madiwani wanalipwa shilingi 350,000. Kazi kubwa ambazo wanazifanya Waheshimiwa Madiwani kwenye Kata kule ni kuhakikisha wanasimamia miradi ya fedha nyingi ambazo ndizo tunazipitisha hapa Bungeni, wao ndio wanakwenda kuzisimamia, lakini kwa mwezi Diwani analipwa shilingi 350,000. Hata mtendaji wake wa Kijiji anapata fedha nyingi kuliko Mheshimiwa Diwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri hebu endeleeni kuwaangalia Waheshimiwa Madiwani, angalau na wenyewe hata wakiongezwa shilingi 100,000 au shilingi 200,000 posho za kujikimu, ikafika kwenye shilingi 400,000 na kitu au shilingi 500,000, tutakuwa tumewasaidia sana. Mwisho wa siku na wenyewe wapande hadhi sasa walipwe mishahara. Wanafanya kazi kubwa, nasi Wabunge tunawategemea sana Waheshimiwa Madiwani watusaidie tukiwa huku Dodoma. Wao ndio wanafanya kazi kule usiku na mchana kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine sasa, Wakurugenzi waache visingizio vya kukosa pesa za vikao. Wameshapunguziwa mzigo mkubwa sana kwenye hii shilingi 350,000/=, wafanye vikao kwa wakati. Kamati ya Fedha inatakiwa kukaa kabla ya tarehe 15 kila mwezi, lakini baadhi ya Halmashauri wanakaa miezi mitatu halafu wanapitisha miezi miwili yote kwa pamoja kwa siku moja. Au miezi mitatu wanapitisha kikao cha siku moja, lakini kisingizio ni nini? Mkurugenzi anasema hana pesa. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri hili nalo mliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wako kwa kututengea shilingi milioni 600 kwa kila Jimbo kwa ajili ya sekondari ya kata. Nina ushauri kidogo hapa Mheshimiwa Waziri. Mfano kwangu tuna upungufu katika Kata ya Kweuma, Mkindo, Lubungo, Kikeo, Msongozi na Homboza. Nina upungufu wa kata sita hazina sekondari ya kata. Kwa hii shilingi milioni 600 kila mwaka itabidi nikae miaka sita ndiyo jimbo langu zima liwe limepata sekondari za kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, hii shilingi milioni 600 kama inawezekana, kama mtaona mnaweza mkaigawanya na Halmashauri wenyewe kwa kushirikiana na Mbunge na Waheshimiwa Madiwani wakaweza kuhamasisha wananchi wakachangia fursa, hii shilingi milioni 300 ikanunua vitu vya madukani; mabati, nondo, cement na kulipa fundi, tunaweza tukajenga sekondari mbili kwa shilingi milioni 600. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sekondari ambazo tumezijenga wenyewe, Serikali imekuja kumalizia kwa fedha ndogo sana. Sasa shilingi milioni 600 ni fedha ambazo tunaishukuru sana Serikali kutupatia, lakini kwa sekondari ambazo ni nyingi kama kwangu mimi; sekondari sita, hatutaweza kumaliza kwa muda mfupi, itahitaji miaka sita ili tuweza kuzimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru Serikali, kwa kipindi chote, bajeti ya TARURA katika Wilaya ya Mvomero haizidi shilingi milioni 600. Sasa hivi kwa mwaka huu wa fedha mmetenga shilingi milioni 815. Nina imani tutakwenda kutengeneza barabara hizi za TARURA vizuri zaidi na hasa barabara za pembezoni mfano Kata ya Maskat, Kata ya Kinda, Kibati Pemba, Kikeo, Nyandila na maeneo mengine, hizi barabara za TARURA ziweze kupitika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, tulilalamika hapa wakati tunachangia bajeti ya TAMISEMI kuhusu suala zima la TARURA na mmesikia kilio chetu, mmeweza kutuongezea shilingi milioni 500 nje ya bajeti. Hizi zitakwenda kufanya kazi kubwa na nzuri katika Jimbo letu. Nami nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri kama kila mwaka tutaendelea kupata hizi shilingi milioni 500 basi miji ile yote ambayo iko ndani ya Wilaya yetu ya Mvomero tunakwenda kuipa vipande vidogo vidogo vya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hii faini ya boda boda. Faini ya Boda boda ilikuwa ni shilingi 30,000/=. Mama yetu amesikia kilio, mmepunguza mpaka shilingi 10,000/=. Tatizo kwenye hizi faini sasa, Askari wanapokamata pikipiki, badala ya kulipa lile kosa moja shilingi 10,000/= sasa watalipa makosa nane, tisa mpaka 10. Ile shilingi 30,000/= itarudi na zaidi ya ile 30,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi na bahati nzuri Waziri wa Mambo ya Ndani uko hapa, hawa Askari wakikamata hizi pikipiki, anaweza akawa amekamata kwa kosa moja pengine la kutokuvaa helmet, yule dereva wa bodaboda hana ile hela, anachukua pikipiki wanaipeleka kwenye Kituo cha Polisi. Wakati pikipiki iko pale, anapoenda kuitafuta shilingi 10,000 au ile shilingi 30,000 ya zamani ili aende akagomboe ila pikipiki, akirudi pale anaambiwa hii pikipiki ilifanya mauaji, ilibeba mtu ambaye amekwenda kushiriki mauaji. Yule dereva wa bodaboda anakimbia anaitelekeza pikipiki na yule mwenye pikipiki hakanyagi kwa sababu anajua dereva wake alishakwenda kufanya mauaji na ile pikipiki. Mwisho wake ile pikipiki inakwenda kuuzwa kwa Askari wenyewe, wanauziana ile pikipiki. Baadhi ya vituo wamefanya hivyo, hata Mheshimiwa Waziri ukitaka ushahidi nitakupa. Wamekusanya pikipiki, wameshindwa kuzigomboa, wamewapa kesi za kutisha za mauaji, wamezitelekeza, wameuziana wenyewe maaskari hizi pikipiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii shilingi 10,000/= hii ambayo mama ametaka kuwalenga hawa vijana, kama hamtakuwa makini, watakwenda kutengenezewa kesi na pikipiki watazisahau kule kwenye vituo vya polisi. Kama ni faini, hatalipa shilingi 10,000/=, atalipa kuanzia makosa Matano, sita na kuendelea kama ambavyo walikuwa wanafanya. Kwa hiyo, Mheshimwa Waziri naomba hili nalo mliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mpango wa bima nchi nzima. Hili ni jambo jema sana, lakini hizi zahanati zetu hazina madawa na wala hazina vifaatiba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)