Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Kabula Enock Shitobela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na uhai na leo nipo katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa kwenye ushuru wa vitenge vinavyotoka nje ya nchi, ukilinganisha na nchi za jirani zinazotuzunguka. Hapo awali vitenge vilitozwa kodi ya 0.28 kwa yadi moja ambayo nadhani sijui ni mita moja, ambapo tulipata wateja wengi sana kutoka nchi mbalimbali za jirani kama vile Zambia, Comoro, Msumbiji, Kongo, Malawi na Zimbabwe, Kenya na Uganda, kwa sababu kodi hiyo ilikuwa ni Rafiki, ilikuwa inaweza kulipika na hata vile vitenge vikaweza kuuzwa kwa bei nafuu. Baada ya muda nchi yetu au Serikali iliongeza kodi kufikia 0.4 per yard ambapo sasa tulikosa tena wanunuzi kutoka nje tukawa na wanunuzi wa kutoka hapa hapa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia kuhusu uchumi, uchumi tunauchangia kwa namna nyingi ambapo huyu M-Comoro alipokuwa akija kuanzia anaposhuka Airport au Bandarini au stendi ya basi, anapochukua taxi, mnufaika pale ni dereva taxi au bodaboda au mwenye bajaji. Akifika hotelini atachukua hoteli atalala, lakini asubuhi akiamka anaweza kula kwa mama ntilie, mama ntilie naye akapata kipato chake. Vile vile anapokuja hapa, atahitaji mawasiliano atanunua labda ni vocha, atatumia. Kwa hiyo Kampuni zetu za simu zitapata mapato na vile vile Serikali itapata kodi pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wateja walivyokuwa wakija, hawanunui vitenge peke yake, bali wameweza kununua na bidhaa nyingine muhimu nyingi. Kwa hiyo ilikuwa ni faida kubwa kwa wao kuja hapa Tanzania. Sasa naona kodi mwaka jana ilipandishwa mpaka kufikia dola moja kwa yadi moja lakini katika bajeti hii nimeona wameshusha percent kufikia 0.5 kwa kitenge cha polyester na cotton wameweka ushuru kuanzia 0.6 hadi 0.8 ambayo kodi hii haitawezekana kabisa kulipika. Matokeo yake tutaongeza wafanyabiashara ambao watakuwa wanakwepa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wanunuzi watakwenda kununua nchi jirani, kwa sababu sasa hivi changamoto iliyopo, nchi hizi jirani zote zilizozitaja hapo awali, sasa hivi zinauza vitenge bei rahisi zaidi kuliko Tanzania kwa sababu ushuru wake ni reasonable. Kinachotokea sasa wafanyabiashara wanakwenda kununua nchi jirani vitenge, wanatafuta njia za panya, wanaingiza ili waweze kuuza bei nafuu, lakini vile vile kupata faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu Tukufu inayoongozwa na Mama yetu mpendwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, najua mama yetu ni mwema na ni mwelewa aangalie katika hili suala zima la vitenge, kwa sababu vitenge hivi mvaaji wa mwisho ni mama, ni kitenge kama hiki nilichokivaa mimi leo na Waheshimiwa wengi walioko humu wamevaa vitenge hivi. Vile vile wauzaji wakubwa wa vitenge hivi ni akinamama, ndiyo wanaouza vitenge, kwa hiyo naomba waangalie kwa jicho lingine kwa kum-support mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie kwa kusema kwamba…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nilitaka nimpe taarifa mchangiajia anayeendelea kuchangia sasa kwamba kuhusiana na suala la kodi ya vitenge, imepanda kwa asilimia 100. Ilipokuwa asilimia 0.4 vitenge vilikuwa vinalipiwa kwa container la 40 feet shilingi milioni 128. Sasa hivi imepanda kwa asilimia 100 ina maana Watanzania wataenda kutoa container hilo la 40 feet kwa shilingi milioni 400 jambo ambalo biashara hii inakwenda kufa pale Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kabula.

MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo nimeipokea kwa mikono miwili. Ni kweli kabisa. Labda niongeze tena kidogo kusema kwamba, pamoja na kwamba tunalinda viwanda vya ndani lakini viwanda vyetu vya ndani kwanza haviwezi kutosheleza soko lililopo. Soko ni kubwa sana na viwanda vya ndani bado havina hiyo capacity kubwa kiasi hicho, lakini pia kwenye ubora, tukubali tu kwamba bado ndiyo tunaanza, siyo vibaya, lakini ni vizuri tuwe na varieties, yaani tuwe na vitu vingi; vitenge vya aina tofauti. Atakayependa kununua cha Tanzania anunue, atakayependa kununua cha China anunue, atakayependa kununua cha Burundi anunue. Kwa hiyo, naona ni vyema tukaacha soko huria, kila mtu akaweza kuingiza na kuuza; na kila mtu awe na choice yake anayotaka kununua.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ehe, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba sera ya nchi yetu ni kulinda viwanda vyetu vya ndani. Suala la kwamba vitenge vyetu labda havina ubora, aishauri Serikali kuboresha na suala la kwamba uzalishaji ni mdogo, aishauri Serikali namna ya kuongeza uzalishaji na siyo ku-entertain bidhaa kutoka nje. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa unapokea taarifa?

MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana, siipokei kabisa kwa sababu hivi vitenge vya kutoka nje siyo kwamba vimezuia au vitamaliza hili soko la vitenge vinavyotengenezwa nchini. Bado nafasi ya kuuza vile vitenge ipo. Kila vitenge vina watu wake wanaoweza kununua. Siyo kwamba kile kitenge cha Tanzania; labda nitoe mfano mmoja. Mheshimiwa Msongozi anaweza akakinunua kwa sababu wanawake wa Kitanzania au wa Kiafrika kwanza wamejaaliwa, ni mashallah, wana miili mikubwa na maumbo makubwa, vitenge hivi ni vidogo, havitoshi. Hata kwa kufunga mama wa kisukuma aliyepanda kule kijijini, hakiwezi kumtosha, labda achukue vipande viwili. (Vicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa kitenge nimeshamaliza, meseji imeshafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu biashara ya mahoteli. Naomba ni-declare interest; nami ni mdau katika hoteli. Hali ya mahoteli nchini hasa Dar es Salaam na Arusha ni mbaya sana, lakini sijawahi kusikia Mbunge hata mmoja humu anaongelea. Nimekaa kimya, lakini leo nimeona ni vyema niongee kwa sababu hata mimi niko kwenye hiyo sekta. Kwa hiyo, ninaelewa hali halisi, wafanyabiashara wa mahoteli au mahotelia wanachokipitia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hakuna biashara tena kwenye mahoteli hasa hoteli zilizopo Dar es Salaam na Arusha kama nilivyoongea awali, lakini sababu siyo Covid 19 kama watu wanavyotafsiri. Hili tatizo limekuwepo muda mrefu kabla ya Covid 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu Tukufu kurudisha tena biashara kwenye sekta binafsi hasa kwenye hoteli. Wajaribu kutuletea tena zile semina, wafanye kazi mbalimbali katika mahoteli yetu ili nasi tuweze kuchangia ushuru katika nchi yetu. Kwa mfano hoteli moja sitaitaja, walikuwa na wafanyakazi 80, lakini hivi ninavyoongea na wewe wana wafanyakazi 15; na waathirika wakubwa waliopunguzwa kwenye kazi hiyo ni wanawake, kwa sababu mahotelia wengi huwa ni wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali hii ijaribu kuangalia ni jinsi gani ita-rescue huu upande wa mahoteli. Kwa kweli hali ni ngumu sana na hatujui hatima yetu ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)