Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nawapongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu wake, Mheshimiwa Mary Masanja, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Allan Kijazi, pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa na muhimu wanayofanya ya kusimamia maliasili yetu kwa manufaa ya kizazi cha leo na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, naomba sasa nijielekeze kwenye hoja kwa kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni ushauri kwa Serikali kuhusu haja ya kuinusuru Tasnia ya Uwindaji wa Kitalii katika Taifa letu. Tasnia hii ni moja ya vyanzo vya mapato kwa Taifa letu ambayo kwa muda wa miaka 10 sasa imekuwa katika hali tete na inaendelea kushuka zaidi hasa katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Corona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na takwimu za Chama cha Wawindaji wa Kitalii (Tanzania Hunting Operations Association - TAHOA), idadi ya watalii wa uwindaji wanaokuja nchini kwetu imekuwa ikishuka kwa kasi sana. Idadi imepungua kutoka wawindaji 1,503 mwaka 2010 hadi 519 mwaka 2019. Mapato nayo yameshuka kutoka Dola za Kimarekani milioni 23.5 mwaka 2010 hadi kufikia Dola milioni 11.5 mwaka 2018, sambamba na kushuka kwa umiliki wa vitalu vya uwindaji kwa asilimia 51 kutoka vitalu 157 mwaka 2010 hadi 87 tu ambavyo ndivyo vyenye wawekezaji kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamiliki waliviacha vitalu vyao kwa hiari tangu mwaka 2018 kwa sababu ya kushuka sana kwa faida na ongezeko kubwa la gharama ya ada na kodi wanazotozwa na Serikali, jambo ambalo linalifanya Soko la Tanzania la biashara ya Utalii wa Uwindaji kuwa la bei ya juu zaidi kuliko washindani wetu Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zimbabwe kwa mfano, hupokea wastani wa wawindaji wa kitalii 800 japo wao wana vitalu 16 tu vya Serikali ikilinganishwa na Tanzania yenye zaidi ya vitalu 150. Zambia ambayo ina vitalu 26 tu, kulingana na takwimu za mwaka 2019, ilipokea wawindaji 446 ikilinganishwa na Tanzania ambayo ilipokea wawindaji 541 tu kwenye vitalu vyake 76, na zilizobaki hazikupata wawindaji kabisa. Afrika ya Kusini wao hupokea wastani wa wawindaji 9,000 kwa mwaka ikifuatiwa na Namibia ambayo hupokea watalii wa uwindaji 8,000 kwa mwaka licha ya kuwa maeneo yao ya uwindaji ni machache ukilinganisha na idadi na maeneo tuliyonayo sisi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya tozo zinazolalamikiwa sana na TAHOA kwamba imechangia kuongezeka kwa gharama ya utalii wa uwindaji ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye mauzo yao yote ambayo ilianza kutozwa mwaka 2016; na kufikia mwezi Machi mwaka 2020, pigo kubwa zaidi liliikumba tasnia ya uwindaji baada ya asilimia 80 hadi 100 ya watalii kuahirisha safari zao kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa corona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kufuatia kushuka kwa biashara ya utalii wa uwindaji, nashauri, Serikali iridhie mambo mawili muhimu ambayo yasipozingatiwa, tasnia hii itazidi kuathirika sambamba na kushuka kwa mapato yanayotokana na utalii wa uwindaji pamoja na ulinzi na uhifadhi wa maliasili yetu katika maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba VAT irejeshwe kwenye mfumo wa ugawaji kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2016. Kulingana na taarifa za TAHOA, tangu VAT ianze kutozwa kwa kiwango cha asilimia 100 ya pato lao, Tanzania imeshindwa kushindana na nchi nyingine za Afrika zenye uwindaji kama Zimbabwe, Zambia, Msumbiji, Namibia, Afrika ya Kusini, Botswana, Uganda, Ethiopia, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gabon na Benin. Nchi hizi wao hutoza VAT ya kati ya asilimia 10 hadi 18, lakini ni kwa baadhi ya bidhaa tu kama vyakula, malazi na ada ya uwindaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka 2016, TAHOA ilikuwa inalipa VAT kwenye vyakula na malazi tu na hizi zilikuwa zinahesabiwa kama asilimia10 ya ada za safari na asilimia 90 iliyobaki ilikuwa haihesabiwi ama ilipewa msamaha, kwa sababu TAHOA walikuwa wanatambulika kama wauzaji wa nje (exporters).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli TAHOA ni exporters kwa sababu hakuna mtalii wa uwindaji atakayekuja Tanzania kuwinda kama hatasafirishiwa nyara zake kwenda nchi aliyotoka aweze kwenda kufurahia. Hata Kimataifa, uwindaji wa kitalii unatambulika kama export industry, na hata Tanzania tuliitambua hivyo mpaka mwaka 2016 VAT ilipoanza kutozwa kwa asilimia 100 ya mauzo na mapato ya makampuni ya uwindaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wetu wa Tasnia ya Utalii wa Uwindaji wanailalamikia Serikali kuwa pamoja na kulipia VAT kwenye mapato yao yote, kampuni hizi pia zinawajibika kubeba gharama kubwa za kudhibiti ujangili, kuendeleza vitalu, kuchangia miradi ya maendeleo ya jamii, kulipa ada za mwaka za vitalu (Block Fees), mambo yote ambayo yanawapunguzia kwa kiwango kikubwa faida wanayopata na wakati mwingine hujikuta zikijiendesha kwa hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kutokana na kudorora kwa utalii wa uwindaji, nashauri Serikali isamehe kampuni za utalii wa uwindaji kwa muda au kupunguziwa Ada ya Vitalu vya Uwindaji. Kwa sasa, kwa mwaka kitalu cha uwindaji hulipiwa Dola za Kimarekani 60,000 kwa vitalu vya daraja la kwanza, USD 30,000 kwa vitalu vya daraja la pili, na USD18,000 kwa vitalu vya daraja la tatu. Katika kipindi hiki cha janga la Corona, wenye vitalu wengi wanashindwa kulipia ada ya vitalu kutokana na kukosekana kwa wateja wa uwindaji. Kwa hiyo, kutokana na hali hii, makampuni ya uwindaji wanashindwa pia kufanya doria na ulinzi wa wanyamapori kudhibiti ujangili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2020, hadi tarehe ya mwisho kulipia ada ya vitalu, ni vitalu 64 tu ndivyo vilivyolipiwa na vitalu 48 hawakuweza kulipia kwa wakati hata baada ya kuongezewa muda wa ziada wa siku 30. Hii inaonyesha hali ilivyo tete kwa sasa katika tasnia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri ili kuinusuru tasnia hii yenye faida kiuchumi na kiuhifadhi, Serikali ifanye mapitio ya sera kuhusiana na tasnia hii na kufanya mabadiliko muhimu ili kuzidi kuboresha mazingira yake ya uwekezaji. Kuna haja ya kufanya marekebisho kwenye viwango vya kodi na ada ya vitalu, pamoja na tozo mbalimbali ikiwemo VAT ya asilimia 18 kwenye huduma na mauzo yote ili kuchochea ukuaji na uwekezaji katika tasnia ya uwindaji na hivyo kuongeza mapato kupitia kuongezeka kwa watalii watakaovutiwa na punguzo la bei kuja kuwinda nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia kubwa ya mapato yanayotokana na uwindaji hayatokani na ada ya vitalu kwani huchangia asilimia 15-20% tu na asilimia 80 - 85 hutokana na ada za nyara pamoja na ada za leseni. Hivyo naishauri Serikali ipunguze kodi ya vitalu ili kampuni ziweze kumudu kupunguza bei kwa wateja wao na hivyo kuvutia idadi kubwa zaidi ya watalii wa uwindaji. Kwa njia hiyo, wataweza kuinua mapato yanayotokana na tasnia hii ambayo kwa sasa yameshuka kwa zaidi ya asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni ushauri kwa Serikali kuhusu kufuta pendekezo la kutaka kuanzisha Pori la Akiba katika katika Wilaya ya Longido Ukanda wa Ziwa Natron.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilijulishe Bunge lako Tukufu na wewe mwenyewe kuhusu mchakato wa Wizara ya Maliasili ulioanzishwa mapema mwaka 2020 wa kutaka kuanzisha Pori la Akiba katika maeneo ya vijiji vya wafugaji wa wilaya ya Longido na ambayo wao wenyewe wameyatenga na kuyahifadhi mahususi kwa ajili ya malisho ya akiba kwa mifugo yao misimu ya kiangazi na nyakati za majanga ya ukame ambayo hutokea mara kwa mara katika wilaya yetu ya Longido.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na hali ya kijiografia na maisha ya wakazi wa Wilaya ya Longido ambao kwa asilimia 95 ni wafugaji, kutakuwa na athari kubwa sana kijamii na kiuchumi endapo Pori la Akiba lililopendekezwa litaanzishwa katika maeneo ya malisho ya mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, naomba niishauri Serikali yetu sikivu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mama yetu jasiri, mpendwa wetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, isitishe mchakato huu kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii ya wafugaji wanaoishi katika eneo husika wanatunza mazingira na tayari eneo hilo ni Pori Tengefu (Game Control Area – GCA) na linatumika kwa uwindaji wa kitalii tangu miaka ya 1950. Sambamba na shughuli ya ufugaji kwa Jamii ya Kimasai ambayo ndiyo wakazi Wakuu wa Wilaya ya Longido, kuna azma ya Serikali yetu kuongeza maeneo ya wafugaji na siyo kuyapunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lililopendekezwa la Ukanda wa Ziwa Natron, milima ya Gelao, Ketumbeine, Matale na nyanda za malisho ya vijiji zaidi ya 17 za Tarafa ya Ketumbeine na Engarenaibor ambazo zitamezwa na Pori hilo la Akiba, linategemewa sana na wafugaji ambao ni asilimia 95 ya wakazi wa Longido na mifugo ndiyo njia kuu ya uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kufanya eneo husika Pori la Akiba litaleta mgogoro kati ya wananchi na hifadhi na itaongeza migogoro ndani ya Wilaya ya Longido na maeneo ya jirani Wilayani Ngorongoro ambako tayari hali ya uhifadhi na jamii imekuwa tete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wake, walizirudishia zaidi ya vijiji 900 ardhi ya hifadhi ili wananchi wapate maeneo ya kuishi na kufanyia shughuli za kiuchumi; na kwa Vijiji vya Wilaya ya Longido, hazikuwa kwenye orodha yoyote ya vijiji vyenye mgogoro na hifadhi. Hivyo, siyo vizuri sasa kuongeza tena eneo la hifadhi kwa wananchi ambao tayari wanaishi vizuri na wanyamapori na bila kuwa na migogoro na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Akiba linalopendekezwa litaathiri vijiji vyote 19 vya Tarafa ya Ketumbeine; Vijiji 11 vya Tarafa ya Engarenibor na Kijiji kimoja cha Kiserian katika Tarafa ya Longido. Hili ni eneo lenye zaidi ya watu 90,000. Vilevile Pori hilo litaathiri baadhi ya vjiji vya Wilaya ya Ngorongoro na ikizingatiwa kuwa eneo la Ngorongoro tayari kwa sehemu kubwa ni hifadhi na hivyo ikifanyika hivi wananchi hawatakuwa na mahali pa kuishi na kufuga; hivyo kuongeza migogoro katika wilaya husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Longido tuna kiwanda kikubwa na cha kisasa chenye uwezo wa kuchakata nyama ya mifugo zaidi ya ng’ombe 1,000 kwa siku, mbuzi na kondoo 4,000 kwa siku; na hivyo eneo kubwa zaidi ya hili tulilonalo kwa sasa linahitajika kwa ajili ya kufuga na kunenepesha mifugo yetu kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani. Hivyo pendekezo la kumegua sehemu ya ardhi ya Longido haliendani na azma ya Serikali ya kuongeza maeneo ya malisho ili kuinua sekta ya mifugo na kukuza uchumi unaotokana na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya kwanza ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Bunge letu ya tarehe 22 Aprili, 2021 Dodoma, alikazia dira ya Taifa letu la kuendelea kuongeza maeneo ya ufugaji. Wilaya ya Longido ni moja ya wilaya kame sana nchini na ambayo hukabiliwa na majanga ya ukame mara kwa mara, hivyo milima inayotaka kutwaliwa pamoja na eneo la nyanda za Ziwa Natron ndiyo huwa kimbilio la kupatia malisho na maji wakati wa majanga ya ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii katika ngazi zote (Kijiji, Kata kupitia WDC, Halmashauri ya Wilaya kupitia Baraza la Madiwani, wala DCC na RCC) hawakuwahi kushirikishwa katika mchakato wa pendekezo la kuanzishwa kwa Pori hili ili kupata mawazo yao. Hivyo jambo hili siyo shirikishi. Pori linaloonekana kama liko wazi kwa wageni ni maeneo ya asili ya wafugaji waliyopangilia matumizi ya malisho na maji kwa misimu tofauti ya mwaka ili kutunza ekolojia na upatikanaji wa malisho bora ya mifugo kwa majira ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya milimani ndiyo hunusuru mifugo kwa malisho na maji wakati wa kiangazi na nyanda za chini hufaa nyakati za mvua na masika tu kutokana na ukosefu wa vyanzo vya maji misimu ya kiangazi katika Wilaya ya Longido. Hivyo kuyatwaa maeneo hayo ni sawa na kuwaangamiza wafugaji wa Wilaya ya Longido.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, naomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii isikilize kilio cha wananchi wa Jimbo langu la Longido na ichukue hatua sahihi bila kusita kusitisha na kulifutilia mbali pendekezo la kutaka kutwaa eneo hili la wafugaji na kulifanya kuwa Pori la Akiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja na ahsante kwa kupokea mchango wangu.