Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza nikupongeze kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri; Katibu Mkuu, Dkt. Allan Kijazi; na watendaji wote wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Vile vile niwapongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kuweza kusaini Mkataba wa REGROW. Pia tunawashukuru sisi Nyanda za Juu Kusini kwa kutupatia magari 12 kwa ajili ya operesheni za mbuga ambazo ziko Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri pia kwa kusaini GN. Najua huu ni mwanzo mzuri wa kuanza ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu kwa ajili ya kutangaza utalii Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua REGROW Phase I imechukua Mikumi National Park, Nyerere National Park, Udzungwa pamoja na Ruaha. Ni matumaini yangu kwamba Phase II mtachukua Kitulo National Park pamoja na hifadhi nyingine za Taifa zilizopo Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ni hifadhi nzuri sana; ina maua mazuri ya kila aina. Ni hifadhi ambayo hakuna ulimwenguni inayofanana na Kitulo National Park. Ina maua mazuri pamoja na ndege wa ajabu ambao wanakuja kila mwaka mara moja; wanatoka Australia moja kwa moja mpaka Kitulo, hawasimami sehemu yoyote. Kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba Phase II ya REGROW, Kitulo National Park ambayo iko Wilaya ya Makete ndani ya Mkoa wa Njombe inaingizwa kuwa sehemu ya mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo nilishawahi kuwauliza watu wa Utalii, hivi kwa nini hawakuiingiza Kitulo National Park katika huu Mradi wa REGROW? Wakaniambia, unajua barabara kule haziko rafiki na nini; lakini nitumie nafasi hii kusema kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutengeneza ile barabara ya Njombe – Makete. Hivi sasa nina habari njema; Mheshimiwa Rais Samia ameshatuingizia pesa za kilometa 25 kutoka Makete kupitia Hifadhi ya Kitulo kutokea Mbeya. Kwa hiyo, sitategemea tena kuwe na sababu ambazo zinahusiana na masuala ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi hapa Mheshimiwa Mrisho Gambo amejinasibu sana akasema kwamba asilimia 80 ya pesa zinazotokana na utalii zinatoka Kaskazini. Niwakumbushe basi Wizara, sasa hivi mwangalie maeneo mengine. Mje Nyanda za Juu Kusini, kuna vivutio vingi vya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Nyanda za Juu Kusini mfanye ile mnaita package tourism (utalii wa vifurushi). Mtalii anatua Iringa, anaenda Ruaha National Park, anaenda kuangalia historia ya Mkwawa, anakwenda Sao Hill kufanya utalii wa picha, akitoka hapo anakwenda Njombe, anakwenda Kitulo National Park, anapita pale Kipengele, anatoka anaenda Songwe kuangalia kimondo pamoja na maji moto; anaweza akatoka hapo akaenda Mbeya kuangalia zile waterfalls na mambo mengine ambayo yanavutia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile anaweza akaamua kwenda kwa Mheshimiwa Waziri kule Ruvuma kuangalia historia ya wamisionari kwenye Jimbo la Mheshimiwa Jenista. Kuna njia ambayo wamepita watumwa zamani; na huo ndiyo mwanzo wa umisionari kule Ruvuma. Yote hayo mnaweza mkayaweka kwa pamoja mkafanya hiyo package tourism. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia msisahau kule Njombe kuna mashamba mazuri ya chai, kuna mashamba mazuri ya miti, mnaweza mkafanya farm tourism. Hivyo vyote ni vivutio. Sisi hatujajaliwa wanyama wengi sana kule Southern Highland, lakini tuna utalii ambao wanaita wa ikolojia, mnaweza mkafanya vizuri na tukaweza kuiingizia nchi yetu mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya vivutio ambavyo wananchi na Waheshimiwa Wabunge wa kutoka Nyanda za Juu Kusini waliweza kuviainisha. Ni kazi sasa ya Wizara kuvifanyia kazi ili vithibitishwe rasmi. Kwa mfano, kuna Gereza hili la Kihesa Mgagao Iringa; Wabunge wa Iringa hapa miaka mitano wamezungumza. Lile gereza lina wafungwa 17 tu, yaani wafanyakazi ni wengi kuliko idadi ya wafungwa. Lile gereza, Nelson Mandela alipita pale akalala. Kile chumba ni historia nzuri, nayo ikaingia katika package ya utalii kwa Iringa na Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla. (Makofi)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.


MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Neema Mgaya, kuhusiana na hilo gereza. Ni kwamba aliwahi kuja Balozi wa South Africa hapa nchini, alipokuta kuwa ni gereza, akakataa kuingia pale kuona kile chumba ambacho mzee Mandela alilala pale. Kwa hiyo, unaweza kuona kwa namna gani tunapunguza watalii, maana yule angeweza pia kuwa balozi wetu wa utalii kule South Africa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema Mgaya, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili. Hapo sasa ndiyo Wizara iangalie namna gani tunapoteza mvuto katika suala hili la utalii kwa vitu vidogo vidogo lakini vyenye msingi na ambavyo vinaweza vikatuongezea pia mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Ogidivai, kule Wanging’ombe, kuna lile jiwe linaitwa Ogidivaa, lina ramani ya Afrika na jiwe lingine hapo hapo pembeni lina ramani ya South America. Vitu kama hivyo mvichukue. Pia kuna Msitu wa Nyumbanitu. Huo msitu uko Wanging’ombe, una kuku Weusi mbao hawajawahi kufugwa na mtu na wanazidi kuongezeka siku hadi siku. Ukienda pale unawakuta, hawafi, wapo tu. Kwa hiyo, vitu kama hivyo ni vya kuviongeza katika hiyo package tourism. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishasema kule Iyangweni na Matuhu, unajua majina ya huku Songea ni magumu magumu; hiyo nayo mnaweza mkaiingiza pia ikawa kwenye sehemu ya package tourism. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nizungumzie suala la migogoro ya ardhi kati ya hifadhi za TANAPA pamoja na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mgaya.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwende mkatatue mgogoro wa Hifadhi ya Mpanga Kipengele inayozungukwa na Vijiji vya Malangali, Mlangali, Mpanga, Iyai, Igando na Ruduga. Migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na wananchi imekuwa mingi. Mheshimiwa Waziri nendeni mkashughulikie mmalize migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)