Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipatia. Lakini namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ambayo nimeipata ya kuzungumza ndani ya Bunge hili siku ya leo katika Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nikupongeze sana kwamba vinasaba hivi vimezungumziwa sana, lakini nafikiri umekwenda kwenye conclusion kwamba sheria ije sasa ili twende kwenye maamuzi TBS wapate kihalali kutokana na sheria.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, naomba nisijielekeze sana huko, nijielekeze kwenye umeme hapa. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, kwamba katika bajeti hii, nimeona bajeti za mwaka jana na mwaka huu, wao kila wanapotenga fedha za maendeleo zinakuwa karibia asilimia 98, ikionesha kabisa kwamba kuna kazi inakwenda kufanyika. Kwa hiyo, vitabu vyao vyote vinaonesha asilimia 98 huwa inakwenda kwenye maendeleo. Na haya tunayaona kwenye miaka mitano, sasa tuna vijiji zaidi ya 9,000 vilivyoongezeka kuanzia mwaka 2015 ambavyo vimepata umeme.

Mheshimiwa Spika, mwaka huu inaonekana bajeti imeongezeka kwa asilimia nane, kwa hiyo ninaamini kazi inayokwenda kufanyika itakuwa ni kubwa kuliko hata iliyofanyika mwanzo.

Mheshimiwa Spika, niseme tu, umeme wetu huu ambao ninauona umewekwa kwenye vijiji vyetu, pamoja na miradi mingi ambayo imefunguliwa hapa katikati, bado tuna kazi kubwa ya kupeleka kwenye vitongoji vyetu, huko kwenye senta tu za vijiji na wananchi wamefurahi sasa kupata umeme, kila mmoja ambaye hana umeme sasa anajuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe sana Wizara wajitahidi na wakandarasi ambao wametupatia simu hawa tunaendelea kuwasiliana nao umeme uwezo kuwafikia wnanachi kwa ajili ya kuchachua maendeleo ambayo yalikuwa yamesimama kwa sababu ya kukosekana kwa umeme.

Mheshimiwa Spika, tuna vijiji 1,956 havijapata umeme, jimboni kwangu katika vijiji 83 nina vijiji 26 tu ambavyo vina umeme, vijiji 57 havijapata umeme. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, mkandarasi ambaye nimeongea naye jana – nilipata namba yake – ameniambia bado anashughulikia performance bond CRDB, kwa hiyo, bado hajaweza kwenda kwenye eneo la tukio kwa ajili ya kutupatia umeme.

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana; katika miaka miwili ambayo tumeambiwa Desemba, 2022 kutakuwa na umeme nchi nzima, tuhakikishe kwamba umeme huu unaosemwa uweze kufika kwenye vitongoji ili wananchi waweze kuona maendeleo ambayo tunayasema.

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo moja, nimeona wanasema kuna densification. Hii densification kuna mahali ambapo watu wameshafanya wiring muda mrefu tu, lakini walivyokuwa wanafanyiwa survey maelezo yanasema kunatakiwa nguzo mbili, hawezi kuwekewa umeme ule, anatakiwa tena aingie kwenye hii densification kwa sababu anaonekana yeye hapo alipo siyo kijiji, ni sehemu tu ya mtaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yako maeneo mengi ambayo yanakaribiana na miji midogo hii yana tatizo hili; watu wengi wamefanya wiring na hawana umeme, na malalamiko yao ni makubwa. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri, hawa wakandarasi wanaokwenda, pamoja na miradi hii ambayo tumeisema, uweze kuwasaidia wananchi hawa waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, kwenye umeme hapo; pamoja na kujenga miundombinu ambayo tunaisema, kuna tatizo kila ninapokwenda ninalikuta mahali kwenye miji yetu. Umeme unapowekwa kati ya nguzo na nguzo kuna kitu wanaita clearance, clearance ni mahali ambapo nikisimama natakiwa nione wire ukiwa juu yangu. Lakini bahati mbaya kwenye miji yetu hii unaweza ukasimama ukaona wire umepita tu karibu nusu mita kutoka kwako ulipo.

Mheshimiwa Spika, sasa huu ujenzi wa miundombinu ya aina hiyo udhibitiwe sana kwa sababu wanaita mawimbi (magnetic feed), yale mawimbi yanapopita karibu na mwanadamu yana athari, na hizo athari inawezekana zisitokee kesho au keshokutwa, zikaja baada ya muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapojenga laini zetu hizi tuhakikishe kwamba ile clearance ya mwnadamu kwenda kwenye wire iwe ni ile iliyokuwa-recommended, iliyosemwa. Ukienda kwenye miji mbalimbali unapita unakuta wire unapita tu jirani, maana yake ni kwamba ujenzi uliofanyika ulikuwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niishauri Serikali kwamba ujenzi wa laini zinazojengwa wahakikishe kwamba hicho kinachojengwa kama clearance kwenye ile sag kati ya nguzo na nguzo kiwe ni kile ambacho kiko recommended kwa ajili ya mwanadamu ili mawimbi yale, magnetic feed, isimletee madhara kwa namna yoyote ile. Kuna mahali inaoneshwa hata kwenye mitandao mtu anapita karibu anagusa wire. Ni hatari sana kwa maisha yetu.

Mheshimiwa Spika, nihame kwenye umeme niende kwenye EACOP (Bomba la Mafuta). Hili bomba la mafuta limesemwa muda mrefu na wananchi wetu wamekuwa wanajiandaa wanajua watauza mchicha, mayai na kuku. Lakini hivi vitu kama alivyosema jirani yangu hapa, Mheshimiwa Zedi, havijana defined. Havijajulikana ni vitu gani vitafanyika kwenye biashara ya bomba la mafuta, sasa vingesemwa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kupitia Taasisi ya Uwezeshaji, kwamba ingewezekana wananchi ambao tunao wako wengi wanaotaka kufanya biashara kwenye bomba la mafuta lakini uwezo wao ni mdogo. Hii Taasisi ya Uwezeshaji ambayo ninaamini ipo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, waangalie uwezekano wa kuwa na fedha ambayo itapitishwa kwenye benki yoyote ili iweze kuwasaidia hawa wafanyabiashara wadogo na wakiweza kukopeshwa kwa utaratibu wa benki wataweza kufanya biashara hizo. Ili isifike biashara hii ikavamiwa na wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusipofanya hivyo wako watu wamejiandaa kufanya biashara na bomba la mafuta, wataonekana kama ni Watanzania lakini itakuwa ni hela kutoka kwa watu wengine wenye uwezo mkubwa na siyo wale Watanzania wenyewe. Kwa hiyo, hii Taasisi ya Uwezeshaji iangalie inaweza kupita mahali gani kwenye benki zetu ikawawezesha hawa waweze kufanya kazi katika miaka hii.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mtu atahitaji labda kuku 1,000, tukiuliza kuku 1,000 nani anao ili aweze ku-supply, utaona mwananchi anaanza kuhangaika, anakusanya huku na huku. Lakini kama wamewezeshwa watakuwa wameandaliwa kwa ajili ya kuvuna hiki ambacho tunakisema ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikumbushe suala la mwisho kwa Mheshimiwa Waziri; kuna mradi kutoka Geita, Mpomvu kwenda Nyakanazi, ambao ndugu yangu, Mheshimiwa Ezra, aliusema pale. Huu mradi umesemwa muda mrefu sana lakini haukamiliki. Kwa hiyo, ni ombi langu Mheshimiwa Waziri, hawa wakandarasi wanaokuja sasa wahakikishe kwamba mradi huu unakamilika, vijiji vingi sana vinapitiwa na mradi ule na kama haukamiliki maana yake wale wananchi hawawezi kupata umeme kwa sababu ndiyo laini pekee kwenye backborn inayoweza kuwapelekea umeme.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)