Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nianze kwa kuchangia katika Sera ya Mambo ya Nje na Diplomasia ya Kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, kuna mwanadiplomasia mahiri sana na alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa 38 wa Australia, Julie Bishop ambaye katika moja ya hotuba zake alizungumzia masuala haya; naomba niyanukuu kidogo na alisema; wakati diplomasia ya kizamani ililenga amani diplomasia ya uchumi inalenga ustawi kwa kukuza ustawi wa maisha ya watu, diplomasia ya kiuchumi inakuwa ndio msingi wa kudumisha amani, ikitekelezwa vizuri diplomasia ya kiuchumi ni lazima ilete matokeo ya kukua kwa uchumi, kuongezeka kwa ajira na kufunguka kwa vyanzo vipya vya uwekezaji wa ndani na wa kimataifa kuchochea ubora wa maisha ya watu na nchi husika. Kinyume cha matokeo hayo diplomasia ya kiuchumi itakuwa ni neno tu ambalo tunaweza tukaiga yaani copy and paste.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nazungumza hivi; diplomasia ya uchumi itasaidia sana nchi yetu kuweza kutoka hapa tulipo. Itasaidia sana kuwa na mafanikio makubwa katika nchi yetu kwa sababu tunaposema diplomasia tunahitaji kuwa na wataalamu wazuri, tunahitaji mahitaji ya viongozi wenye maono, tunahitaji watu wenye ushawishi, tunahitaji mikakati madhubuti. Bila kuwa na hivi vitu tutapata changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kupata hii nafasi, najua wewe ni mbobezi na ni mzoefu. Tunakuomba uweze kuifanyia kazi tuweze kuipata hii sera na tuweze kufanyia yale ambayo Watanzania wanahitaji kuyaona katika kutafuta masuala mengi ambayo wameyasema wengine, napenda nisiyarudie. Ajira inatakiwa ipatikane kwa wenzetu ambao ni mabalozi wako kule waangalie fursa zilizopo ni zipi ili waweze kuzileta. Kwa hiyo, tunataka visionary leadership, strong negotiators, tunataka lobbyists na tunataka smart strategies ambazo zitasaidia nchi yetu iweze kutambulika na kupata yale ambayo mengi ambayo tunaweza kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa twende kwenye hadhi za balozi zetu, wamezungumza kuanzia Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje. Hadhi za balozi zetu zinasikitisha, balozi zetu ziko hohehahe, hatupeleki pesa za maendeleo, ndio mwanzo wa haya yote ambayo unayaona. (Makofi)

Kwa hiyo, tunaishauri Serikali, tunamuona Waziri wa Fedha yupo apeleke pesa ili balozi zetu ziendane basi angalau hata na balozi za nchi za Afrika ambazo zipo maeneo hayo, tunatia aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaani balozi zetu unaangalia zina majengo yanavuja, balozi zetu zimechoka huko, majengo ya balozi zetu yanatia uchungu. Kwa hiyo, naomba nisiyaelezee sana haya, kuna maeneo mengi viongozi wetu wakuu walikwenda wakaahidi, lakini bado mpaka leo hatujajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la uraia pacha; mimi nazungumza kwamba uraia pacha ni fursa kimkakati. Tunaangalia nchi za wenzetu wameweza kufanya hivyo, watu wanapata uraia pacha. Tuchukulie mfano tuna wachezaji wanacheza nchi za wenzetu, kuna mchezaji anaitwa Rashford yuko kule anacheza Manchenster United, yule inasemekana wazazi wake ni Wazanzibari, sasa angekuwa na uraia pacha angeweza kurudi akachezea nchi yetu na wengine wengi ambao wako huko wakipata hii fursa kwetu inasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu Wakenya diaspora yao imechangia dola za Kimarekani bilioni 2.7 kwa mwaka 2018 na ambayo ni asilimia tatu ya pato la Taifa ambayo imetokana na uraia huo pacha. Kwa hiyo, sisi tukiweza tusikae kama kisiwa, tuwaangalie wenzetu wanafanya nini na sisi tuangalie pale ambapo italeta tija na sisi tuifanyie kazi hivyo kwa sababu hii tunajikosesha wenyewe mapato kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kuna nchi moja inaitwa Estonia. Hii nchi wana uraia wa kidijitali, kwa hiyo, hapo ulipo unaweza ukapata uraia, unaweza kuomba una kampuni uweze kuwekeza kule na wanaendesha nchi inakwenda, wanakwenda kidijitali, lakini sisi kuna vitu ambavyo tunavifinya. Kwa hiyo, kama kuna mambo ambayo tunataka tuyaweke sawa basi Mheshimiwa Waziri aangalie ni mambo gani ambayo tuyaweke sawa, lakini tuweze kuwafikia wenzetu ili na sisi tuweze kusonga mbele tunyanyue uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatutumii vizuri diaspora zetu. Kwa nini nasema hivi; balozi zetu zikiangalia Watanzania walioko katika nchi ile, tuwe na kanzidata, tujue kabisa kuna wanafunzi wangapi na wanasoma masomo gani na yatasaidiaje kwa nchi yetu? Wapi wanafanya kazi gani? Kama ni watu wa kufanya kazi za majumbani tufahamu, itambulike kabisa na hizi ni fursa wafanyabiashara wangapi? Wanafanya biashara zipi?

Mheshimiwa Spika, sasa tukitambua hivyo mabalozi hawa watatusaidia kuona fursa ziko wapi. Tuna watu wako kule wanasoma nini? Wanafanya nini? Kwa hiyo, sisi kama nchi itatusaidia kutambua kwamba tuwekeze wapi kwa zaidi kwa sababu tunakuwa tuna data kamili ya watu ambao wako nje ya nchi ambao tunaweza kuwa-supervise na kuona nini ambacho wanaweza wakakifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwa mabalozi; mabalozi wana wajibu mkubwa sana wa kutafuta fursa za ajira kwa nchi yetu. Fursa za ajira watatutafutia mabalozi wetu, kama kweli tutawachukua wale ambao wamefuzu, wamesoma diplomasia, wanaelewa ni kitu gani wafanye katika nchi hizo.

Kwa hiyo, wanapokuwa pale wanaweza wakaziona fursa, amesema Mheshimiwa Balozi Pindi Chana hapa. Watu tuna mazao mengi yako kule tunakosa masoko, lakini balozi ambayo itaona kwamba hapa pana fursa hii ndio kazi yao kubwa ya kuhakikisha inashirikiana na nchi hii kujua kwamba mkoa fulani wazalishe hiki ni fursa huku na tunaweza tukaipelekaje hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia sisi tunakuwa hatuangalii, wenzetu wa Kenya wana-market strategies ambazo wanatangaza utalii. Unakuta wanatangaza kabisa kwamba pengine Mlima Kilimanjaro uko kule kwa sababu sisi tuna vitu ambavyo ni vikwazo. Mimi kuna jamaa yangu alikuwa yuko huko Sweden, lakini ametaka kuja, kwenda kwenye ubalozi wetu wanasema hawatoi visa ya East Africa. Sasa anakwenda kwenye ubalozi wa Kenya na nchi nyingine anapata visa, anakuja kupitia Kenya, kule anatoa pesa inabaki kule, sisi tumezuwia, lakini atafika Tanzania kapitia Kenya. (Makofi)

Kwa hiyo, kuna fursa kama hizo zipo sisi tunazizuia kwa vikwazo ambavyo kwa kweli kama kuna msingi mkubwa ambao tunauona hauna manufaa basi turekebishe ili na sisi tuweze kupata pesa kutoka kwa watalii wengi wanaotaka kuja kwetu. Kwa hiyo, hayo ndio mambo ambayo ninaya-insist.

Mheshimiwa Spika, wenzetu kule kuna lugha ya Kiswahili, lugha ya Kiswahili nje wanaofundisha wengi ni Wakenya wanafundisha Kiswahili, sisi tupo na ndio waanzilishi na wenye Kiswahili hapa, hatufanyi hivyo. Ukiangalia kwenye mtandao unakuta kuna translation za Kiswahili wamefanya Wakenya, wameingia mkataba na google, wanapata fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi tuzione hizo kama ni fursa na sisi tuweze kutumia mabalozi wetu na wengine kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaitendea haki Wizara hii, tunaitendea haki nchi yetu ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini cha mwisho sio kwa umuhimu, basi angalau hawa mabalozi wabakiziwe maduhuli yale ambayo badala ya kupeleka Serikalini wabaki nayo mabalozi yawasaidie kwa ajili ya ujenzi wa balozi zao, ahsante sana. (Makofi)