Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani. Kipekee nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema. Nitajielekeza moja kwa moja kuchangia zao la alizeti pamoja na kitunguuu endapo muda utatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Singida ni Mkoa unaoongoza kwa kuzalisha zao la alizeti. Serikali imekuwa ikisema kwamba zao hili ni la kimkakati lakini mkakati huu upo katika maandishi na wala si kwa vitendo. Niiombe sana Serikali mkakati huu wa kuzalisha zao la alizeti uwepo kwa vitendo ili wananchi wa Mkoa wa Singida waweze kunufaika na ukulima wenye tija wa zao hili la alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mkoa wa Singida wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi katika kulima zao hili la alizeti. Hivi majuzi kulikuwa na uhaba mkubwa wa mafuta ambayo yanatokana na zao la alizeti. Kama Serikali ingetoa kipaumbele basi nina uhakika kabisa zao hili la alizeti lingeweza kumaliza changamoto kubwa ya uzalishaji wa mafuta lakini pia lingeweza kukuza uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Singida ndiyo inayoongoza kwa kulima alizeti bora kabisa Afrika ya Mashariki na Afrika ya Kati lakini kilimo hiki cha alizeti kimekuwa hakipewi umuhimu. Niiombe sana Serikali iweze kufungua milango kwa wakulima wetu kwani wakulima wengi wamekata tamaa na hata kwa msimu uliopita, alizeti hii imezalishwa kwa kiwango cha chini sana. Kwa kuwa, Serikali inayo dhamira nzuri ya kuanzisha mashamba ya kimkakati, basi itenge maeneo ambayo sasa yatakwenda kufungua fursa za uzalishaji wa kilimo hiki cha alizeti katika halmashauri zetu kwani halmashauri za Mkoa wa Singida zote zinalima zao hili la alizeti, zikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Mkalama, Ikungi, Manyoni pamoja na Iramba. Naishauri sana Serikali iweze kufungua milango kwa wawekezaji waje kuwekeza katika zao hili la alizeti ili sasa tija iweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa katika zao letu hili la alizeti ni uzalishaji wa mbegu. Niiombe sana Serikali iweze kutoa kipaumbele kwa taasisi zetu hizi za ASA pamoja na TARI, ambazo zimekuwa zikizalisha mbegu aina ya records ziweze kupewa bajeti ya kutosha ili ziweze kuzalisha mbegu hizi na kuweza kumaliza changamoto hii. Wakulima wetu wamekuwa wakinunua mbegu hii kwa Sh.3,500 kwa kilo lakini imekuwa ikizalishwa tu kwa tani 500 kwa mwaka wakati viwanda vyetu vinaweza kuzalisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Aysharose Mattembe.

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 100.