Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Martha Nehemia Gwau

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii uliyonipa nami niweze kuchangia Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kuja na Mpango huu wa Elimu bila Malipo. Naomba nipongeze sana kwa sababu Mpango huu umesaidia vijana wetu wengi, watoto wetu wengi kuweza kumaliza Kidato cha Nne tofauti na awali ilivyokuwa elimu yenye malipo. Kwa hiyo, kwa hili kwa kweli naomba niipongeze sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine naomba nijikite sana kwenye mitaala yetu au mtaala wetu uliopo kwa sasa hivi, naomba tuufanyie marekebisho au maboresho ili uendane na dunia inavyotaka au mahitaji ya dunia sasa hivi yanavyotaka, wanafunzi wawe na nini au wahitimu wawe na nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tujikite sana na kuwafundisha hawa watoto ubunifu na skills ili wakimaliza hapo wajiajiri na waweze kuajiriwa. NI tofauti na sasa hivi ambapo wakimaliza wengi wanajikita sana kusubiri ajira na hizo ajira hazipatikani kwa urahisi na siyo nyingi za kutosheleza. Katika hilo, nina ushauri wa vitu vitatu kwenye kuboresha mitaala yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, tungeanzisha somo la technical subject katika elimu ya msingi mpaka sekondari. Kwa nini nasema hivyo? Hawa wanafunzi wanapomaliza Form Four kuna makundi matatu yanapatikana baada ya kuwa wamehitimu. Kuna kundi la kwanza watakwenda Form Five; kuna kundi la pili watakaokuwa wazazi wao wanaweza kuwalipia shule za VETA na ufundi na kadhalika; na kundi la tatu ambalo hilo halitaenda VETA, halitaenda Form Five; wanafanya nini na ndiyo kundi kubwa kuliko haya mawili niliyoyataja mwanzoni?

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwajengea uwezo kutoka primary wakamaliza Form Four na skills za kutosha, wakitoka hapo wataweza kwenda kwenye Halmashauri zetu, wakapata mikopo wakaweza kujiajiri, wakaunda vikundi, wakakopesheka, wakajiajiri na tukasaidia kutatua tatizo la ajira. Tofauti na sasa akimaliza Form Four anabaki nyumbani. Sasa atafanya nini na wakati tumempa elimu bure? Kwa hiyo, akimaliza na ujuzi itamsababisha yeye kujiajiri mwenyewe na kukopesheka kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, program ya pili tungeanzisha sports and games katika shule zetu ambapo awali zilikuwepo na tukapata wachezaji na watu wazuri tu, lakini naona zimefifia kwa muda uliopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, michezo inaibua vipaji shuleni, inaibua wachezaji bora, wanamichezo bora kutoka utotoni na kutoka umri mdogo. Hatuwezi kusema mtu akienda kwenye degree ndiyo anaweza akawa mchezaji mzuri, hapana. Kuanzia level ya primary mpaka hapo Form Four atakuwa mchezaji mzuri, ndiyo tutakuwa na wachezaji wazuri. Kwa mfano, wachezaji wa nje kama akina Morisson, Chama, nasi tutapata wa kwetu hapa Tanzania. Nadhani wana-Simba wenzangu watakuwa wamenielewa. Kwa hiyo, tuanzishe hizo sports ambazo zitawasaidia watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, tuanzishe environmental subjects. Nina maana gani hapa? Tuna bahati ya kuwa na kanda tofauti tofauti na katika kila kanda kuna kitu wanajivunia. Kuna kanda wanafanya uvuvi, kuna kanda wanafanya kilimo, kuna kanda madini, kuna kanda wanafanya uvuvi na ufugaji na kadhalika. Tutakapowapa wanafunzi wetu mafunzo ya environmental studies, ataamua, mimi nataka kuwa mkulima. Atakuwa na mwalimu mkulima anamfundisha. Kuanzia level ya primary mpaka hiyo ya sekondari. Akitoka hapo anaweza akajiajiri mwenyewe kwa kufuga, kulima au kuchunga. Hayo tunamfundisha kutokana na mazingira alipo. Watu wa kanda ya kati tunajua tunafanya nini, watu wa kanda ya kaskazini na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya tukiyaongeza yatatusababishia vijana wetu wanaomaliza form four kwa kuwapa hii elimu bila malipo, lile kundi la tatu lililobakia, litapata kitu cha kufanya mtaani, badala ya sasa hivi wakimaliza wanakuwa wamekaa bila kazi yoyote, lakini hili lote itatusaidia sisi kama Serikali kupunguza suala la ajira kwa sababu, tutawakopesha kwenye halmashauri zetu na watajiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho, naomba Serikali iongeze bajeti kwenye Wizara ya Elimu kwa sababu, Wizara ya Elimu inapaswa kuwapa Walimu mafunzo. Nimeongelea upande wa wanafunzi, lakini watoa huduma je, ambao ni Walimu. Naomba wapatiwe semina mbalimbali hata mara mbili kwa mwaka kwa sababu, unapompa Mwalimu semina ni kama motisha. Semina yenyewe hata iwe ya malipo, akipata semina yake anapata malipo yake inamsaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine motisha, kwamba, wanapopata zile semina basi kunakuwa na shule iliyofanya vizuri inapewa zawadi, kuna Mwalimu bora aliyefanya vizuri anapewa zawadi. Hii una-motivate Walimu wengine waliobakia au shule nyingine zilizobakia na wao kufanya vizuri zaidi, ili wapate hizo zawadi na recognition. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na uzuri zawadi sio lazima pesa. Mtu atakapopata certificate kutoka kwa Mkuu wa Mkoa au kwa Mkurugenzi wa Halmashauri anajisikia yuko well valuable, yaani anajisikia kwamba, ameheshimika na mchango wake umechukuliwa. Hii itasaidia Walimu wetu kuwa motivated na wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine pia ni reviews. Unapokaa na Walimu wa halmashauri moja wakasema kwa nini mimi nafaulisha zaidi kuliko wewe? Wata-exchange ideas, watapeana mbinu na mikakati mbadala ambayo itasababisha na yeye akirudi afanye vizuri kwenye shule yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndio ulikuwa mchango wangu kwa siku ya leo. Nashukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)