Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia kwenye sekta ya elimu. Nami niungane na Wabunge waliozungumza tangu jana kupongeza juhudi za Wizara ya Elimu katika kuimarisha na kuboresha elimu kwa ajili ya vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze ushirikiano unaoimarishwa kati yao na TAMISEMI maana Wizara ya Elimu imebaki na sera, TAMISEMI imebaki na utekelezaji lakini tunaona jinsi wanavyoendelea kushirikiana. Wizara inatafuta resources inazipeleka TAMISEMI na TAMISEMI wanatekeleza miradi. Wizara inabuni maandiko yanakwenda kutelezwa na TAMISEMI kwa maslahi ya maendeleo ya nchi yetu. Hata huu Mpango wa Elimu bila Malipo najua uliandaliwa na Wizara ya Elimu na ikatoa miongozo na TAMISEMI ikaingia kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitajikita kwenye maeneo machache. Bahati nzuri mimi ni mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii lakini ukiisikiliza jamii yote imekuwa ikizungumza juu ya kutoridhishwa na mwenendo wa elimu kwa ajili ya maendeleo ya vijana wetu. Wakati mwingine tusipokuwa waangalifu tunaweza tukajikuta lawama hizi zinaelekezwa kwa Waziri na Waziri na wataalam wake wakaona kama ni watuhumiwa wa kushusha elimu yetu. Mimi naomba niwashauri kwamba viongozi wa Wizara na wataalam walioko Wizarani ni wawakilishi wetu tu katika kusimamia sekta ya elimu. Hivyo, ni vema watusikilize sisi wawakilishi wa wananchi na wadau wengine wanapozungumza mambo haya then wapange mikakati ya utekelezaji na uboreshaji kwa kuwahusisha wadau hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naungana na wasemaje wote waliopita wanaosema elimu yetu ina changamoto. Sote tuna watoto na tunaona wakitoka vyuoni au shuleni hali zao huwaje. Wakati fulani nikiwa mmoja wa watendaji wa Serikali wataalam wanapoandika hata ile ku-draft barua Mtendaji Mkuu unakuwa na kazi ya ziada kurekebisha barua ile. Hii zote ni indicators kwamba uwezo wa vijana wetu ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, ni vizuri tukishauriwa kwamba pana changamoto tuisikie na tuone namna ya kui-address. Kama mtu anamaliza chuo kikuu hawezi kuandika barua nzuri ya kuomba kazi inayoshawishi lazima tujue kwamba kwenye elimu yetu lipo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, naomba nijikite kwenye Jimbo la Butiama, nimkumbushe Waziri, najua nililisema hili kwenye Kamati na nikajibiwa lakini nina maoni kwamba ni vizuri tukasikiliza na tuone namna ya kutanzua. Katika dhamira ya kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa letu, Serikali ilikubali kuanzisha Chuo cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu (Mwalimu Julius Nyerere University of Agriculture and Technology) ni zaidi ya miaka kumi sasa hakijaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chuo hiki kipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi yam waka 2010-2015 lakini kiko kwenye Five Years Development Plan I ya mwaka 2010/2011 - 2015/2016 lakini pia kiko kwenye Five Years Development Plan II ya mwaka 2016/2017 - 2021/2022. Kwa kuanzia Mkoa wa Mara na Wilaya ya Butiama walifanya mambo mengi; moja ni kukubali ku-sacrifices iliyokuwa Shule ya Sekondari O-Level na A- Level iitwayo Oswald Mang’ombe High School yenye ekari 86 yawe majengo ya kuanzia chuo kikuu hiki, lakini Butiama ilitoa ekari 573 kama eneo la kujenga campus kuu na eneo la Baiki. Pia tulikubaliana kwamba viwepo vitivo kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Mara na kule Rorya Kinesi walioa jumla ya ekari 75; Serengeti eneo la Kisangula walitoa ekari 136 na maeneo yote yalipewa hati miliki kwa jina la chuo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa upande wake ilitekeleza wajibu wake ambapo ni pamoja na kukubali kuanzisha mitaala 35; 26 ya shahada na 9 stashahada, miongozo na sera mbalimbali zaidi ya 25 ilitayarishwa na kuidhinishwa na mamlaka husika kwa maana Ofisi ya Rais, Utumishi na Msajili wa Hazina. Wizara pia ilitoa wataalam 79; academic staff 42 lakini watumishi mwega ambao ni administrative staff 37.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachohuzunisha tangu watumishi hawa wapelekwe zaidi ya miaka saba iliyopita chuo hakijaanza lakini wanalipwa mishahara. Kinachotuuma zaidi ni kwamba shule ile ilijengwa ili itumike lakini sasa haitumiki kwa ajili ya wanafunzi wa sekondari pia haitumiki kama chuo. Sasa watu wa Butiama na Mkoa wa Mara wanauliza chuo hiki kitaanza lini? Anayetakiwa kusajili chuo hiki ni TCU ambayo iko chini ya Wizara. Wizara chini ya Mheshimiwa Prof. Ndalichako ilikubali chuo kianze na wakapeleka wataalam including Deputy Vice Chancellors lakini hadi leo hakuna kinachoendelea. Wananchi wanauliza hivi lengo la Serikali lilikuwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi wananchi wa Butiama wanataka chuo kianze kama ilivyodhamiriwa awali. Wamechoka kusubiri, wanaomba majibu ya Serikali. Kwa kweli katika mazingira haya majibu yasipokuwa ya kuridhisha najiuliza hivi nitaachaje kuing’ang’ania shilingi ya Mheshimiwa Waziri wangu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imegonga.

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja lakini naomba swali langu hili lijibiwe vizuri. Ahsante sana. (Makofi)