Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Naomba niende moja kwa moja kwenye masuala ya mabadiliko ya tabia nchi.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyokumbuka kwamba, Tanzania imeridhia mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi na halikadhalika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi Tanzania mwaka 2000 na kitu Tanzania iliandaa mkakati wa mabadiliko ya tabianchi, lakini kabla ya hapo Tanzania iliandaa mkakati wa kupunguza ongezeko la hewa ukaa kutokana na masuala mazima ya uharibifu na ukataji wa misitu hovyo. Sasa namwomba tu Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje atuambie tu kwa kiasi gani wametekeleza ule mkakati wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2012 na wana mpango gani wa kufanya mapitio ya mkakati ule kwa sababu matatizo bado yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, halafu pia nataka vilevile kumwomba Mheshimiwa Waziri, kama tunavyojua kwamba, hizi documents zimetumia fedha za Watanzania na kwa kiasi kikubwa inaonekana mara nyingi tukishakuzitayarisha zinabaki kwenye ma-shelf na utekelezaji wake unakuwa ni mtihani. Kwa hiyo, naomba tu hili lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, pia kuna suala zima, ambalo wenzangu wameligusia hapa kuhusu fedha za mabadiliko ya tabianchi. Kuna Mifuko hii, Mfuko wa kwanza Mfuko wa Nchi Masikini wa Mabadiliko ya Tabianchi na kuna Mfuko wa GCF wa Green Climate Fund, lakini pia kuna Mfuko wa Adaptation Fund. Mifuko hii yote inasaidia nchi kuweza kutekeleza mikakati yake ya mabadiliko ya tabianchi na kuepukana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Sasa nataka kujua tu kwa kiasi gani Wizara au Ofisi imejitahidi kuweza ku-capitalize hizi fedha na kuweza kutumika. Kwa hiyo, naomba atakapokuja Waziri aje atueleze tu tumepata fedha kiasi gani kwenye Mifuko hii yote mitatu na zimetumika kwa kiwango gani?

Mheshimiwa Spika, kuna sehemu vile vile ambayo ni muhimu pia, niliwahi kuuliza katika swali langu moja hapa Bungeni kwamba, fedha hizi matumizi yake hayako vizuri kimgawanyo baina ya Zanzibar na Tanzania Bara. Imekuwa zaidi ni kama huruma tu kwamba, fedha hizi zitumike Zanzibar na hizi zibaki zitumike Tanzania Bara.

Kwa hiyo naomba Waziri atakapokuja aje atujulishe vilevile kwa kiasi gani fedha hizi zimeweza kutumika upande wa Tanzania Visiwani na upande wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, kuna sehemu moja ambayo ni muhimu kuizingatia. Fedha hizi hasa za Adaptation Fund na fedha za Mfuko wa Nchi Masikini kunakuwa kuna allocation maalum ambayo inagawiwa kwa nchi. Allocation ile kama hukuitumia vizuri, basi inakwenda kwa nchi nyingine ambao wako sharp katika matumizi. Sasa nina wasiwasi kwamba, gawio letu la Tanzania hatulitumii vizuri kwa sababu, mara nyingi utaona ufuatiliaji wetu katika…

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa. Eeh, sawa nimekuona.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba, anayosema ni sahihi na sisi kama Taifa tumeshindwa ku-access hizo fund kwa sababu, kuna qualifications; lazima uwe na taasisi ambazo ziko accredited, wakati nchi kama Kenya ina taasisi kama hizo 18 sisi nadhani tuna taasisi moja tu ambayo ni NEMC. Ndio maana tunakosa hizo fedha pamoja na kuwa fungu limetengwa kwa kila nchi. (Makofi)

SPIKA: Nakushukuru kwa intervention hiyo, lakini pamoja na taasisi hiyo moja hata hizo chache ambazo tumepata zinakwama Wizara ya Fedha. Ndio maana Waziri wa Fedha ajiandae siku ya Wizara yake nitakamata shilingi mimi mwenyewe ya mshahara wa Waziri wa Fedha. (Kicheko/ Makofi)

Kabisa, yaani ni kitu ambacho kila wakati nauliza, hivi hata Spika basi mwambieni ili anyamaze. Kwa nini fedha inaombwa inakuja katika nchi yetu, Wizara ya Fedha mnakalia, eti kisa kamati inayoitwa kamati ya nini sijui, nini sijui inaitwa ile, wala sio ya madeni maana yake hii sio deni, hii ni grant; inaitwa kamati ya, sijui kamati gani, ninyi mnaielewa vizuri zaidi, eti haijakaa. Ni kamati ya wataalam ndani ya Wizara ya Fedha, haijakaa.

Fedha zina miaka miwili, zina miaka mitatu, zina mwaka. Hata Mheshimiwa Jafo tunamwonea tu maana hata yeye hazikwami kwake, zinakwama Wizara ya Fedha. Sasa Wizara ya Fedha waipate kabisa mapema, katika jambo hili tunataka badiliko, kwamba mifuko iko, mapesa yako duniani ya kutusaidia mambo ya mazingira, halafu hizo chache zinazokuja kwanza hatupati za kutosha, hizo chache zinazokuja zinakwama Wizara ya Fedha kwa nini? (Makofi)

Tunataka wenzetu wataalam muandike zaidi tupate hizo fedha, hizo fedha ni za dunia nzima ni za mazingira. Tuweze kufaidika na sisi tuna shida kubwa ya mazingira, miti kukatwa hovyo, makorongo kila mahali na matatizo ya fukwe, mmeeleza ninyi wenyewe matatizo mengi sana, tufaidike na hizo fedha. Sio fedha ikifika Wizara ya Fedha, basi ina wenyewe pale Wizara ya Fedha, haiwezekani! Haiwezekani Bunge hili likakubali mambo ya namna hii. (Makofi)

Endelea Mheshimiwa, alikuwa anakuunga mkono kwenye mchango wako. Malizia dakika zako kama bado una ya kusema.

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza naikubali Taarifa na Wizara ya Fedha walianza mchakato wa accreditation karibu sasa hivi mwaka wa kumi na mpaka leo hawajafanikiwa kupata accreditation.

Kwa hiyo, ningeomba tu sijui kama hili Mheshimiwa Waziri atakuwa na nafasi nalo, lakini tulikuwa tunataka tupate vilevile ufafanuzi wa Wizara ya Fedha wamekwama wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, wenzetu nchi mbalimbali…

SPIKA: Wizara ya Fedha au Ofisi ya Makamu wa Rais?

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha wameanza mchakato wa accreditation wa kuweza ku-access fedha za GCF, huu ni mwaka wa kumi na imeshindikana. Tunashukuru Mungu angalau…

SPIKA: Miaka kumi hatujapata hela za Global Climate Facility.

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, hatujawahi kupata hata siku moja, labda kupitia kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo, hili nafikiri Wizara ya Fedha au Waziri wa Muungano, kwa sababu, yeye ndio answerable kwa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, basi ni vizuri wakaja wakatueleza wana mchakato gani kwa sababu, kama alivyozungumza mtoaji taarifa kwamba, kuna nchi zina karibu taasisi zaidi ya tano, sita, ambazo tayari zimeshakuwa accredited na zinaweza ku-access hizi funds, lakini sisi ndio kwanza CRDB na CRDB ilivyo kwa utaratibu wa benki watakopesha hawatatoa msaada moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, wale ambao watakuwa na uwezo wa kuweza kutoa grant moja kwa moja ingekuwa kama Wizara ya Fedha na kule Zanzibar walianza mchakato, lakini mpaka leo nako bado hawajafanikisha. Kwa hiyo, kwa ufupi Tanzania capacity yetu imekuwa ni ndogo na hizi fedha tutakuwa tukiona tu wenzetu wakizitumia, nchi nyingine, lakini sisi tutakuwa hatuna faida nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie mchango wangu katika mchango wa CSOs asasi za kiraia. Kama unavyojua kwamba, asasi za kiraia na asasi za kikanda na za kimataifa nazo zina mchango wa kuweza kutupatia fedha kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Kuna tatizo ambalo limekuwa likijitokeza kuna asasi ambazo zina wataalam kutoka nje ambao wamekuwa wakisaidia ku-raise hizi funds, lakini hawa wamekuwa wakipata matatizo ya kuzuiliwa vibali na wengine wameondoshwa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeomba tukazisaidie hizi asasi kuzijengea uwezo na hawa wataalam kutoka nje wakija basi tuwape nafasi kuweza kusaidia kuchangia na ku-raise hizi funds.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)