Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. Sambamba na hilo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Jafo kwa uwasilishaji wake mzuri.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu nitapenda kujikita kwenye upande wa mazingira. Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama tulioridhia wa Mkataba wa Minamata kuhusiana na kemikali za zebaki. Ukisoma mkataba wa Minamata katika Ibara ya 13 imeainisha vyanzo na utaratibu wa upatikanaji wa rasilimali fedha ili kuweza kutekeleza mkataba huo. Baadhi ama sehemu ya vyanzo hivyo ni pamoja na kutenga bajeti ya Serikali, kutumia Mfuko wa Dunia wa Mazingira, washirika wa maendeleo pamoja na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijang’amua kinagaubaga ni kwa namna gani tumetenga fedha za bajeti ya Serikali ili kutekeleza masuala yaliyomo kwenye mkataba wa Minamata. Tunaambiwa tunayo fursa kama nchi wanachama kuweza kupata fedha kutoka Mfuko wa Dunia wa Mazingira ili kuweza ku-deal na matumizi ya kemikali ya zebaki ambayo ni hatari sana na ni sumu kwa maisha ya binadamu. Mheshimiwa Spika, hivyo, nitataka kujua, sisi kama nchi tumeitumiaje fursa hiyo ya kuweza kupata fedha kutoka katika Mfuko huo wa Mazingira ili kuweza kuwajengea uelewa watu wetu sambamba na kupunguza athari ama madhara yanayotokana na kemikali ya zebaki.

Mheshimiwa Spika, ninapoizungumzia zebaki ninapenda Bunge lako lifahamu kwamba hii ni kemikali hatari sana na ni sumu kubwa inayosababisha maradhi kwa binadamu ikiwemo ugonjwa katika mifumo ya nerve za fahamu, uzazi, upumuaji, magonjwa ya figo, moyo na saratani, lakini inadhoofisha viumbe hai majini pamoja na athari za kimazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kemikali hii ya zebaki nimetangulia kusema kwamba ina madhara makubwa sana, nasi kama binadamu tunadhurika na kemikali hii kwa kuishika hususan pale tunapochenjua dhahabu, tunapovuta mvuke wenye zebaki, tunapokunywa au kula vyakula vyenye viambata vya zebaki.

Mheshimiwa Spika, hivyo ni vyema sasa Serikali yako ikatambua na kuona namna bora ya kushughulika na kupunguza matumizi ya kemikali hii. Nitaomba Bunge lako lijue kwamba jamii ya wachimbaji wadogo hususan wenzetu wanaotokea ukanda wa ziwa, hawa ndiyo waathirika wakubwa wa matumizi ya kemikali hii ya zebaki. Wanapofanya shughuli za uchenjuaji wa dhahabu maji yale yanayotiririshwa kwenda kwenye vyanzo vya maji hususan mito na maziwa kuelekea…

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa. Endelea tu wewe mwenye taarifa. Nimeshakuona sasa.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba miongoni mwa waathirika wakubwa sana wa kemikali ya zebaki ni pamoja na wanawake ambao wanashughulika katika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini katika migodi yetu hususan Kanda ya Ziwa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Hawa Mchafu, unapokea taarifa hiyo?

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ninaipokea Taarifa hiyo. Ni kweli kabisa jamii ya wachimbaji wadogo pamoja na watu wanaotokea Ukanda wa Ziwa ndio wanaoathirika na matumizi ya kemikali hiyo ya zebaki.

Mheshimiwa Spika, nimeshasema, wakati wa shughuli ya kuchenjua dhahabu, yale maji yanayotiririka kwenda kwenye vyanzo vya maji, mito na maziwa ndipo pale maji yale yanapokuwa contaminated na kemikali hii ya zebaki…

SPIKA: Kumbe ndiyo maana akina Musukuma hawanenepi, zebaki tupu! (Kicheko)

Endelea Mheshimiwa Hawa. (Kicheko)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ndiyo Ndugu zetu hawa wa Ukanda wa Ziwa, hawa Wanyamwezi, Wasukuma watani zangu, wajuu zangu wanapojiweka katika hatari kubwa ya kupata maradhi ambayo nimeyataja hususan maradhi hayo ya saratani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo shaka; na research ambayo siyo rasmi ni kwamba leo ukienda katika Taasisi…

SPIKA: Mheshimiwa umesimama eh! Endelea Mheshimiwa Hawa.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ipo shaka ama hofu na niseme kwamba hii ni research lakini siyo rasmi kwamba leo ukienda katika Taasisi yetu ya saratani, pale Ocean Road, wagonjwa wengi na Ndugu wa wagonjwa wengi wa pale, lugha na lafudhi inayozungumzwa pale, ni watani zangu Wasukuma.

Kwa maana hiyo, ni dhahiri shahiri, kufuatia shughuli hii, wenzetu wamejaaliwa kupata madini, lakini athari yake au madhara yake ni kujiweka kwenye hatari ya kupata maradhi ambayo nimeshayataja.

SPIKA: Yaani Mheshimiwa Hawa anasema, ukifika Ocean Road pale utasikia tu titiri titiri, unajua hao hao! (Kicheko)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, unasikia tu ng’wadila, ng’wadila, wanakandamiza. Asilimia kubwa ya wagonjwa wa pale ni hawa watani wangu. Tafiti zinaonesha vifo vinavyotokana na ugonjwa wa saratani vimefikia asilimia 15. Asilimia 15 ya vifo, siyo vidogo katika nchi yetu. Hivyo nina mambo mawili ya kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ninapenda kuishauri Serikali kwamba wakati umefika sasa kuja na njia mbadala ya kuchenjulia dhahabu na kuachana na hii kemikali ya zebaki.

Mheshimiwa Spika, ninaomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia…

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia kwamba tunayo teknolojia ama njia mpya ya uchenjuaji dhahabu inayoitwa cyanide. Kwa hiyo, Ndugu zangu na Serikali naomba sana tuanze kutumia hii njia mpya, tuachane na zebaki ambayo ina madhara makubwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo. Ninashukuru, ahsante sana. (Makofi)