Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii, la kwanza, mchango wangu utajikita kwa Taarifa ya Kamati ya Katiba na Sheria, kuhusiana na Hifadhi ya Jamii na niipongeze sana kamati kwa kufanya kazi nzuri na nitaongezea hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi imeanzishwa sababu moja kubwa, ni kuangalia mustakabali wa wafanyakazi wetu pale wanapokuwa watu wazima na kustaafu na kulinda maslahi yao baada ya umri wa kustaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini mifuko hii iliwekwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kutambua nafasi ya Waziri Mkuu mwenyewe na unyeti wa mifuko hii na ikitarajiwa, Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake waweze kusimama kidete, ili kulinda mifuko kwasababu ukilinda mifuko, umelinda watumishi wa Taifa hili. Tunavyozungumza Hifadhi ya Jamii na hii Mifuko maana yake tunazungumzia watumishi wa sekta ya umma na tunazungumzia watumishi wa sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mifuko huwa inafanya uwekezaji, na mifuko duniani kote inawajibu wa msingi wa kuisaidia Serikali kuweza kushiriki katika shughuli za maendeleo. Hilo halina ubishi duniani kote, lakini, changamoto iliyokuwa hapa kwetu Tanzania na ambayo ninaomba sana, Mheshimiwa Jenista utujibu sio umjibu Halima hapana, jibu wafanyakazi wa Taifa hili ili wapate matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninasema hivi kwanini? Mifuko inawekeza katika mazingira mawili, zingira la kwanza kuikopesha Serikali na Taasisi zake kwa riba. Serikali inakopa kwa ajili ya kuingiza kwenye shughuli za maendeleo inadhamini Taasisi zake zinakopa, inatakiwa ilipe kwa riba. Lakini la pili, inashiriki katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali ya ujenzi ama wao binafsi ama kwa kushirikiana na Sekta Binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mdudu mkubwa, donda ndugu, zito, ilililo sugu kabisa ni upande wa Serikali. Pesa inazokopa, inazotakiwa ilipe kwa riba, pesa ambazo Serikali inadhamini taasisi zake zikope kwenye Mifuko ya Hifadhi ambayo inatakiwa ilipe, hailipi! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018, mtanisahihisha kama nimekosea, tuliunganisha mifuko tukaambiwa kwamba hii mifuko inaunganishwa ili ufanisi uwe bora zaidi. Nimeona hotuba ya Waziri Mkuu imesema wamepunguza gharama za uendeshaji, yes! Lazima ipungue kwa sababu watu wamekuwa wachache, mifuko ni miwili lakini usugu upo! Zile fedha mlizokopa mna kigugumizi gani kurudisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ester Bulaya amezungumza juzi, kwamba madeni yale ya kawaida kwa taarifa zenu wenyewe kupitia Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni 2.7 trilioni. Pia mnafahamu kuna fedha zingine shilingi trilioni 7.1 ambazo pia PSPF walipewa jukumu kulipa wastaafu ambao walikuwa wamekidhi umri lakini hawajachangiwa, almost ten trillion! Kwenye mifuko hatulipi. Kama Serikali ina uwezo kila Mwaka wa Fedha kutenga shilingi trilioni 8 mpaka 10 kulipa madeni ya nje ya Serikali ama ya mabenki, tuna ugonjwa gani kushindwa kutenga hata shilingi trilioni moja moja basi kila mwaka tuisaidie mifuko yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana na inauma madeni mengine yalikuwa yameiva toka 2007, 2008, 2010, 2014 Serikali inatoa ahadi hapa, haitekelezi! PSPF ikachoka, ikafilisika, tukaunganisha ili kuziba mashimo. Hatuwezi kwenda hivi!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niombe…

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Kimei.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, mimi ningeshukuru au ningemuomba Mbunge anayezungumza aelewe kwamba Serikali ni mdhamini wa mifuko hii. Serikali ina namna nyingi ya kupata fedha wakati wowote, hawezi kusema kwamba hii mifuko imefilisika. Haiwezi kufilisika kwa sababu Serikali ina uwezo wa kutengeneza fedha saa yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie kwamba deni analosema yeye hamna tofauti na deni ambalo linalipwa kwa wakati na Serikali ina namna yake kwa sababu inaweza ikatu-tax sisi saa yoyote ile. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kuogopa kwamba iko siku Serikali itashindwa kulipa hiyo mifuko. Hivyo ndivyo ilivyo duniani kote kwamba fedha ya mifuko inatumika na njia salama kabisa kutumia fedha ya mifuko ni kwa Serikali kutumia zile fedha kwa kufanya miradi ya muda mrefu.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, niseme kwamba Serikali haikosei chochote.

SPIKA: Ahsante sana. Taarifa hiyo ipokee Mheshimiwa Halima.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, ninamheshimu sana Mheshimiwa Kimei na ametumikia nchi hii muda mrefu sana. Sitaki kumjibu kwa sababu nikimjibu naweza, ngoja niendelee. (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Msamehe.

MHE. HALIMA J. MDEE: Namsamehe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niseme hivi, Serikali imekopa fedha, iliingia makubaliano na mifuko, tutakopa hizi fedha, tutarudisha ndani ya muda fulani, tutakopa hizi fedha kwa kuzidhamini taasisi tutarudisha ndani ya muda fulani tena kwa riba. Navyozungumza Mkurugenzi mstaafu mpaka sasa
Serikali inadaiwa zaidi ya shilingi trilioni 10 kwa vitabu vyenu wenyewe! Sasa hiyo shilingi trilioni 10 basi hata lipa kidogo kidogo watu wapate matumaini, hulipi unakauka tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajenga nyumba moja, yaani wala tusigombee fito. Tunawakilisha wastaafu wa nchi hii. Leo Mbunge aniambie kwenye Jimbo lake sasa hivi kutokana na Serikali kutokurudisha fedha, kuna matatizo makubwa sana kwa wastaafu kulipwa ndani ya muda. Zamani ilikuwa mtu anastaafu, ndani ya miezi sita pesa zimeshaingia. Sasa hivi kuna wengine wanastaafu mpaka wanakufa fedha hazijaingia. Hii mifuko ingekuwa ina hela mambo yangeenda mswano. Nashauri Mheshimiwa Kimei akasome…

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mzee naomba utulie basi. Please!

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, Taarifa tena. Hilo analosema lote ni sehemu ya Deni la Taifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kimei sijakuruhusu bado. (Kicheko/ Makofi)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nachoshauri…

SPIKA: Sasa nakuruhusu Mheshimiwa Kimei.

WABUNGE FULANI: Aaaaa. (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka nimuelimishe kwamba hilo analosema kwamba Serikali haijalipa ni sehemu ya Deni la Taifa ambalo kila siku tunasema linakua. Ukweli ni kwamba Deni la Taifa ni kidogo sana kwa sababu ya assets Serikali ilizoweka. Net worth ya Serikali ni kubwa hasa ukiangalia miradi hii ya muda mrefu ya kujenga reli, kununua ndege na kadhalika hizo ni assets zipo. Ukweli ni kwamba ukiondoa liability na assets tulizonazo ni kama zina-balance. Kwa hiyo, hakuna tatizo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Halima pokea Taarifa hiyo, hakuna tatizo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, napokeaje? Tatizo lipo kwa sababu yeye anasema haya madeni ni sehemu ya Deni la Taifa, si ndiyo? Deni la Taifa hapa kila mwaka na mtaona kwenye bajeti ya mwaka huu maana naye ni mpya, sitaki kutumia lile jina lingine, utaona katika bajeti ya mwaka huu tunatenga shilingi trilioni 8 mpaka 10 lakini ujiulize…

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri nimekuona, Taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika,
nilikuwa nafikiri kwamba ningesubiri wakati wa kujibu hoja na nilikuwa nimejipanga kutoa maelezo ambayo yangeweza kusaidia Bunge lako Tukufu na wafanyakazi kuendelea kuwa na matumaini na usimamizi wa sekta kiujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa ufupi lakini nitakuja kutoa maelezo baadaye, tunakubaliana na utaratibu wa Kiserikali wa CAG (Mdhibiti wa Fedha za Serikali) kufanya ukaguzi na kutoa taarifa ya hali ya sekta zote ikiwemo sekta hii ya Hifadhi ya Jamii. Hayo madeni anayoyasema Mheshimiwa Halima, yako madeni ambayo yana uhalali, yanajionesha wazi lakini anapoongeza yale madeni mengine yanayofika karibu kama shilingi trilioni kama saba anazozisema nadhani angerudi akafanye uhakiki vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini nachotaka kusema hapa tulipoamua kufanya merging ya mifuko ilikuwa ni kazi ya Serikali kwa sababu iligundua kuna tatizo kwenye sekta na ndiyo maana ikaamua kufanya merging ya mifuko. Kama Serikali iliona kuna tatizo na kufanya merging nadhani ilikuwa ni hatua mojawapo ya kusaidia na anachokizungumza Halima ni ile pre 99 ili isiue sekta nzima ya hifadhi ya jamii.

Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie sasa hivi tumeamua kutekeleza takwa la kisheria la kufanya actuarial ili kupata taarifa sahihi za hali ya mifuko jinsi ilivyo. Actuarial ndiyo itakayotusaidia kujua hali ya mifuko na nini kifanyike kwenye madai, madeni na kuboresha sekta ili iweze kuwa sustainable.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya haraka haraka tu, wastaafu wa PSSF ambao ni takriban kama 132,670 wamekwishakulipwa mafao na tulitoa taarifa kwenye Kamati. Tunabakiwa na hayo madeni ya nyuma ya wastaafu kama 6,793. Kwa hiyo, hao sasa ndiyo tunaendelea nao. Juzi Hazina wametupa shilingi billioni moja ili tuweze ku-clear hawa wengine waliobakia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo matatizo yapo lakini yako manageable kwa sababu Serikali inasimamia na kuhakikisha kwamba inatafuta suluhu.

SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Halima, pokea Taarifa hiyo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jenista amesema anakubaliana na lile la shilingi trilioni 2.7, hili la shilingi trilioni 7.1 ana mashaka nalo. Namshauri mambo yafuatayo, nenda kasome Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya mwaka 2013/2014 labda nirejee. Ukurasa wa 96, inasema hivi; kwa mujibu wa Ripoti ya Kikosi Kazi na Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali TK/02/Januari 2015 ya mwaka unaoishia tarehe Juni 2013, Deni la Serikali ni shilingi za Kitanzania, kwa kipindi hicho kabla halijafika sasa hivi shilingi trilioni 2.7 lilikuwa shilingi trilioni 1.8. Anasema deni hilo halijajumuisha jumla ya shilingi za Kitanzania trilioni 7.1 ambalo ni deni la Serikali linalodaiwa na PSPF tangu 1999 ambapo PSPF iliwalipa mafao wastaafu waliokuwa hawachangii lakini wanatakiwa kulipwa mafao kwa mujibu wa sheria. Hii ni kwa mujibu wa Taarifa ya Mkaguzi Mkuu na hizi shilingi trilioni 7.1 hamjawahi kuzilipa. Mimi ni mkongwe nimekuwa kwenye hili Bunge na ripoti hizi za CAG ni endelevu. Hamuwezi kutuambia ripoti ya mwaka huu inaziba ile nyingine wakati hamkutekeleza ile nyingine. (Makofi)

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, Taarifa ndogo.

SPIKA: Mheshimiwa Halima, Mheshimiwa Waziri amesimama tena.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika,
nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Halima kwamba hiyo ripoti amesema ni ya mwaka 2013/2014. Ndiyo maana tuliamua mwaka 2016, 2017 na 2018 ili kuhakikisha kwamba tunaondoa tatizo la pre 99 hiyo anayoizungumza kwa kufanya merging. Unapofanya merging unaunganisha mifuko, assets zote na kila kitu. Ukishaunganisha hiyo mifuko inakusaidia sasa ku-treat yale matatizo ambayo yalikuwa siku za nyuma. Mheshimiwa Halima essence ya kufanya merging ilikuwa ni sustainability ya sekta kwa kuzingatia hiyo pre 99 ambayo umesema ni Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachotaka kumshauri, aache tufanye hiyo actuarial valuation, itatusaidia kujua hayo yote yameshafanyika kiasi gani? Naomba niliambie Bunge lako Tukufu tayari PSSF imeshafanyiwa utathmini na ripoti sasa hivi ndiyo inaletwa Serikalini ili iweze kusomwa na kuona hayo mawanda yote na namna sasa ya kuweza kuitendea kazi ripoti hiyo.

SPIKA: Mheshimiwa pokea taarifa hiyo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri kukiri kwamba ile shilingi trilioni 7.1 ilikuwepo lakini yeye anafikiria kwa ku-merge ndiyo unaondoa tatizo. Unapo- merge kitu unachukua zile assets na liabilities. Sasa moja kati ya liabilities zilikuwa ni madeni ya shilingi trilioni 7.1. Jamani, kiroho safi tu, yaani mimi hapa wala sina beef na mtu, nachotaka ni tuangalie kwa namna gani mifuko yetu hii, nakiri kwamba Serikali haiwezi kulipa kwa mkupuo lakini basi turudishe kidogo kidogo ili kuifanya iwe sustainable. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, leo Kamati inatuambia, kuna miradi ya ujenzi zaidi ya minne ya Tungi, Tuangoma, Kijichi, Mzizima I na II ambayo inagharimu shilingi bilioni 495 za wastaafu wetu watarajiwa zimekuwa injected ile miradi imeshindwa kuonesha multiplier effect. Nyumba zimejengwa, hakuna nyumba iliyouzwa tunaishia kupangisha tena tunapangisha bila mikataba ambapo haikuwa lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kaka yangu Wakili kapendekeza tunaomba kuja na mkakati tufanye mortgage financing, tushirikiane na BoT ambayo ndiyo ina jukumu la kusimamia masuala ya uwekezaji kwa kushauriana na hii mifuko. Tushirikiane na BoT na mabenki, uzuri Tanzania tuna sheria ya mortgage financing, tufanye huo utaratibu, wananchi waweze kukopeshwa na mabenki kununua zile nyumba, zile nyumba zitumike kama collateral. Jambo limeshatokea kama tulivyosema juzi kwenye ATCL, zimeshakuja hatuwezi kuzichoma lazima tupange utaratibu wa kufanya mambo yaboreke zaidi. Kwa hili naomba tuangalie utaratibu wa mortgage financing, tushirikiane na BoT kwa sababu inasimamia mabenki yetu, wananchi wapate nyumba kwa sababu sekta ya nyumba kwa Tanzania bado iko chini sana; Serikali ipate na mashirika yetu yaweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tupate majibu, siyo kwa sababu Halima amezungumza bali tupate majibu wa nini muelekeo wa mifuko yetu kwa mustakabali wa Taifa na watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho lakini sio kwa umuhimu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)