Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo niweze kutoa mchango katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wote kwa hotuba nzuri ambayo hakika inaonyesha matumaini makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali kwa ku-respond timely kuhusiana na suala zima la Bima ya Afya kwa Watanzania wote. Walikuwa wamekusudia kwamba wangeweza kuleta Muswada mwezi Septemba lakini wamekiri kwamba kutokana na unyeti wa suala hili, basi ndani ya Bunge hili la bajeti wataweza kuleta Muswada huo ambao hakika sisi kama Wabunge tutakuwa na nafasi ya kufanya maboresho ili kile ambacho tunakikusudia kwa ajili ya Watanzania kiweze kufikiwa. Naomba Serikali isiishie hapo, tumeanza vizuri hivyo ni vema mlango huu tukautumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo nitachangia maeneo mawili nikipata nafasi na eneo la tatu. Eneo la kwanza ambalo naomba nishauri ni kuhusiana na hifadhi ya jamii kwa ujumla wake. Kama tumeanza kutambua umuhimu wa afya za watu wetu ni vizuri sasa in a holistic manner tukatizana ustawi wa Watanzania kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mfuko unasoma ni hifadhi ya jamii lakini ukienda kufuatilia ndani unakuta kwamba hiyo hifadhi ya jamii zaidi inawalenga watu ambao wameajiriwa Serikalini na zile sekta za kuajiriwa ambazo zinajulikana. Hata hivyo, sekta ya Watanzania walio wengi, zaidi ya 65% ambayo inaajiri wakulima, wavuvi na wafugaji huoni dirisha ambalo limewekwa ili baada ya kuwa wamefanyakazi nzuri ya kujenga uchumi katika taifa hili waweze kuhudumiwa. Kila mtu ni mzee mtarajiwa watu hawa tunawasaidiaje ili baada ya kwamba wamefanyakazi nzuri waweze kuishi maisha ambayo ni decent, ambayo kila mtu anatamani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunakuwa tuna-refer Biblia ambavyo siyo sahihi kwamba kwa mwanadamu ambaye amezaliwa na mwanamke miaka yake ya kuishi si mingi akiwa na nguvu 70 au 80 lakini mbona tukitizama wenzetu wanafika miaka 99 wao Biblia yao ikoje? Ukija kutizama kwa ujumla unakuta ni namna ambavyo maandalizi yanafanywa ili mtu huyu baada ya kwamba amefanyakazi kubwa ya kujenga uchumi aishi maisha ambayo ni decent. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunasingizia kwamba unajua kwa culture yetu sisi Waafrika isingependeza mtu akishakuwa mzee atunzwe sehemu ambayo siyo pale alipozaliwa. Hii dhana nadhani imepitwa na wakati. Sisi ni mashuhuda pale ambapo tunakuwa na wazazi wetu na sisi tuko kwenye shughuli zingine jinsi wanavyopata taabu. Ni vizuri ifike wakati muafaka hawa watu ambao wamefanya kazi nzuri na kwa bahati nzuri kuna makundi ambayo vipato vyao viko tofauti tofauti, kuna wakulima ambapo kuna misimu ambayo wanapata fedha wanaweza wakachangia kwa utaratibu ambao utakuwa umewekwa, wavuvi wanaweza wakachangia katika utaratibu ambao utakuwa umewekwa na wafugaji halikadhalika ili pale ambapo umri ukishafika pale anapohitaji kutunzwa awe na option yake kwamba katika kile ambacho amekuwa akichangia apate pesa au a-opt kwamba naomba niende katika maeneo ambayo yametunzwa maalum kwa ajili ya kutunza wazee. Maeneo hayo kutakuwa na madaktari na huduma zote ambazo ni muhimu ili wengine waonekane kwamba kazi waliyoifanya hawakupoteza juhudi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali watutafutie fomula itakuwa ni sahihi ili kuwasaidia Watanzania hawa wengine ambao hawako kwenye kada ya utumishi Serikalini ili nao wafaidike ili tupate Watanzania ambao wanaishi miaka 99. Kama huko kwingine inawezekana kwa nini sisi isiwezekane? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo naomba kuchangia kwa siku ya leo ni kuhusiana na maendeleo kutofautiana kati ya mkoa na mkoa na halmashauri na halmashauri. Yapo mengine ni kwa sababu ya kihistoria hatuna wa kumlaumu imetokea hivyo na maeneo mengine yana uchumi mzuri kutokana na rasilimali zinazopatikana katika maeneo hayo. Sasa wengine wamefanyaje? Ili Taifa kwa ujumla wake kila eneo katika nchi hii liwe ni sehemu salama na ya kuvutia kuishi ni vizuri tukaja na Development Equalization Fund ambayo wale ambao wanazalisha in excess na wale ambao watakuwa willing na mtu yoyote yule aweze kuchangia ili sasa kama Taifa tutizame maeneo ambayo yanahitaji kusaidiwa kutokana na mfuko huo wasaidiwe ili kila sehemu ya Tanzania iwe sehemu salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu ulivyo sasa hivi ukamchukua Mkurugenzi ambaye yuko kwenye Jiji ambalo lina vyanzo vingi vya mapato ataonekana anafanya vizuri sana lakini ukampeleka katika halmashauri ambavyo vyanzo vyake ni kidogo huyo huyo ambaye alikuwa anaonekana anafanya vizuri sana mtaishi kumfukuza kwa sababu inaonekana kwamba ha-perform. Lazima tuje na fomula ya kusaidia wale ambao wanahitaji kusaidiwa ili tunyanyuke kwa ujumla kama Taifa. Mwananchi ambaye anaishi Newala atamani kuendelea kuishi Newala kulikoni kutamani kwenda Dar es Salaam kwa sababu inaonekana iko vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)