Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kidogo katika huu Mpango wa Miaka Mitano. Kwanza kabisa kabla sijaendelea, napenda niunge mkono hoja Mpango huu. Pia napenda kuwapongeza Wizara ya Fedha kwa Mpango huu, tunaamini miaka mitano hii, haya mambo yote yaliyoandikwa humu yakitekelezwa tutakuwa tuko sehemu nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu napenda kujielekeza katika mambo mawili. Katika hayo mambo mawili, napenda kuongelea mambo ya uzalishaji wa bidhaa muhimu za ndani; mfano sukari, chumvi, mafuta ya kula ambayo iko katika page ya tano na ya sita kwenye mambo ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuongelea kwenye ukuzaji wa soko la ndani. katika kukuza uchumi wa nchi, tunajua kabisa nchi yetu na Mataifa mengine yameathiriwa sana na suala la Corona. Tukisema kwamba tunaweza kuongeza fedha kutoka nje, siyo jambo jepesi, lakini lazima tujitathmini. Soko la ndani tulilonalo kwa bidhaa zile za msingi ambazo kila Mtanzania lazima atatumia, tumejidhatiti vipi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kuchangia hayo, nilitaka nirudi kule kwetu Songwe, Wilaya ya Momba katika Kata ya Ivuna ambapo tuna mradi wa chumvi. Huu mradi upo na tafiti zilishafanyika na ikaonekana kabisa chumvi iliyopo pale ni ya kiwango kikubwa sana ambacho hakiishi leo, lakini siioni ile dhamira ya Serikali kuwekeza pale pesa ya kutosha ili chumvi ile iweze kuhudumia angalau Kanda ya Chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapoongelea chumvi, ni kitu ambacho mtu anaweza asitumie sukari, lakini chumvi akaitumia. Kwa hiyo, katika Wizara hii nilitamani tuongezee kipengele cha chumvi, kwa sababu mpaka sasa hivi sielewi kama chumvi iko Wizara ya Madini au iko sehemu gani? Kwa sababu kwenye Madini haijawekwa na sioni popote chumvi ambapo inasoma katika Mpango huu.

Mheshimiwa Spika, katika Mradi huu wa Chumvi, tunaishukuru Serikali, ilitenga shilingi milioni 535, lakini ikaweza kutupatia shilingi milioni 120, si haba, lakini kiwango cha pesa kinachohitajika ili uzalishaji uwe mkubwa ni karibu shilingi bilioni nane. Kwa Serikali hii ya Tanzania ambayo ni Tajiri, siamini kama inashindwa kweli kujikita kuweka fedha kiasi cha shilingi bilioni nane izalishe chumvi ambayo ni lazima itauzika na ikizidi tunaweza tuka-export nje.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka nijikite hapo. Otherwise ningependa pia kuchangia kwenye kipengele cha mafuta kidogo. Tunaamini kabisa kwamba Watanzania wengi ni wakuliwa na wangeweza kupata fedha kupitia hii fursa ambayo ipo kwenye mafuta kwa kujielekeza kuzalisha mbegu za alizeti, chikichi na hata kuzalisha ufuta wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba kama kweli tuna dhamira ya kukuza uchumi, lazima tuwatazame hawa watu ambao wanaitwa wakulima; watu wa chini kabisa ambao ndio wanatufanya wote tuwe na amani hapa, maana bila chakula tunaamini kabisa hakuna mtu ambaye angekuwa yupo comfortable kukaa hapa kama chakula kisingekuwepo. Kwa hiyo, kabla haujatokea mgomo wa wakulima, napenda kuona kabisa wakulima wanapewa kipaumbele, kwa mambo yao yale ya msingi mfano hiyo fursa ambayo ipo ya kuzalisha mafuta, mahindi na kadhalika, yangekuwa yanachukuliwa kwa uzito. Kama ni viwanda vya uchakachuaji wa hizo bidhaa, viwekwe vile ambavyo vina ubora vitafanya finishing nzuri na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nisiseme mengi sana, naomba niishie hapo. Otherwise naunga mkono hoja. (Makofi)