Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango na Serikali kwa kuja na mpango huu maana yake sasa tumefanikiwa kuikamilisha mipango yetu mitatu. Mpango wa kwanza, mpango wa pili ambao tunaumaliza sasa na tunakwenda kwenye mpango wa tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napoanza kuchangia narejea kwenye maandiko, lengo kuu la Mpango wa Tatu ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 yaani kuwa na Watanzania wenye kipato (income per capita) Dola 3,000, kuwa na jamii ya Watanzania iliyoelimika na yenye uchu wa kujifunza, kuwa na uchumi shindani wenye uwezo wa kuagiza na kuuza nje, utawala bora lakini eneo ambalo sisi tunalimudu la umoja, mshikamano na amani. Nina imani hapa tunafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla hatujaenda kwenye mapendekezo yangu nipitie kwenye dhima tunayomaliza na dhima tunayokwenda. Uzuri wa kitabu hutangazwa na kichwa cha kitabu (the title). Kwa waandishi wazuri kama Mheshimiwa Dkt. Philipo Mpango unaweza kusoma jina lake la kitabu ukajua uzuri wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya mpango wa pili wa miaka mitano ambao tunamalizia, ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Ni vitu viwili; kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu lakini kujenga uchumi wa viwanda, ni zaidi ya kujenga viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu alikuwa anashangaa muhubiri wa zamani aliyekuwa anahimiza watu kutumia cherehani kumbe ni kujenga uchumi wa viwanda siyo kujenga kiwanda, ni kujenga utamaduni (the culture). Rafiki yangu marehemu Shah wa A to Z alianza na cherehani kimoja wakati anakufa alikuwa ana kiwanda cha A to Z na alikuwa mlipaji mkubwa wa kodi kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, picha kubwa ni ujenzi wa uchumi wa viwanda unaweza kuanza kidogo kidogo halafu unakua. Watanzania ndicho tunapaswa kufanya kwamba ujenge utamaduni wa kitu kusudi mwisho wa siku uweze kufika kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima mpya ni kujenga uchumi shindani (the competitive economy) kwamba katika mawanda yote tuwe na competitive economy. Nakubaliana na jina la kitabu, nakuja kwenye mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma mipango yote mitatu, huu mpango umeandikwa tulidhamiria kuchangamsha productive sectors (sekta za uzalishaji). Mpango tuliomaliza ilikuwa kutengeneza miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi, tumeishaitengeneza, sasa ni kuchangamsha shughuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeandikwa ifikapo 2025 hatutaki uchumi wa kati, tunataka uchumi wa kati uliojumuishi. Ili uweze kupata uchumi wa kati uliojumuishi wale watu wanaohusika lazima uwajumuishe. Unawatoa wapi? Ni kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyie mnaoandika mpango mmesema hii ni rasimu lazima rasimu hii ije na miradi kielelezi (flagship projects) kwenye sekta zitakazotujumuisha. Tunaweza kuvumbua madini na kuyazindua, gesi, helium, mention whatever, tukawa na GDP na income per capita ya Dola 15,000 haina maana yoyote chenye maana ni uchumi jumuishi. Uchumi jumuishi ni kuwachukua Watanzania hawa katika shughuli zao wanazofanya ukazizindua kwa nguvu wakaweza kuzipeleka kwenye shughuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda mfano mmoja wa Singida, block farming, Singida wanachukua watu kwenye ekari 6,000 wanakwambia kulima hapa minimum eka 5 ukiweza eka 20 hauna caterpillar wanakuletea. Wanakuwezesha unalima halafu kwenye kuvuna ndipo wanakukata. Tunataka uwekezaji flagship project kwenye miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika mipango ya Serikali wanazungumza vihenge, wanazungumza hifadhi. Hoja siyo kuwa na vihenge, tunachotaka kusikia ni uwezo wa taifa wa kuhifadhi bidhaa au chakula kwa kipindi gani. Tuambiwe kwamba tunaweza kuhifadhi mchele wa kulisha nchi hii miaka mitatu, miaka minne ikinyesha mvua likitoka jua hizo ndizo hesabu hoja siyo vihenge. Unaweza kuwa una kihenge ukaita watu 10 wakakila wakakimaliza siku moja. Kwa hiyo, tunataka malengo makubwa mtueleze kwa muda gani. Tunapokwenda kwenye hizi productive sectors kama alivyosema marehemu Ruge, Mungu amrehemu tunaanzia sokoni, mchele una soko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napoipongeza Serikali kwa dhima iliyopita kuna jambo napaswa nilizungumze. Kuna jambo moja la kuangalia na niko tayari kukosolewa, tumeweza kukusanya mapato kwa sababu ya compliance, namna gani watu wali-comply siyo mjadala wa leo, tumepata trilioni 2, niliwahi kusema tunaweza kupata hata 3 hata 4. Compliance ilipatikanaje siyo mjadala tunapaswa tupate mapato makubwa kutokana na ukuaji lakini ukuaji haupo, sekta binafsi inapaswa ikue haikui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, compliance ndiyo imetufikisha hapa, walifanywaje watu kulipa kodi mimi sijui, nisiingie kwenye mjadala huo lakini tunapaswa tukue. Hapa ndipo inapokuja hoja ya kujenga sekta binafsi ya Tanzania. Ili tuweze kufika yale malengo sekta binafsi ya Tanzania inapaswa ijengwe. Wasikudanganye popote duniani sekta binafsi hujengwa na haiendi kwa miaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka miwili unaweza kujenga sekta binafsi, mimi mwenyewe mikononi mwangu nimetengeneza mabilionea naweza nikawazungumza hapa na wengine kaka zao wako humu kwamba Mwijage ndiyo alimtengeneza kaka na msishangae hata Monduli Sajenti ndiyo hutengeneza Brigedia. Kwa hiyo, lazima tutengeneze sekta binafsi, tuwawezeshe. Watu wanachelea kwamba watapoteza pesa, usipochafuka utajifunzaje? Wape wapoteze pesa watoke. Kwa hiyo, kuna haja hiyo ya kuweza kujenga sekta binafsi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliseme hili tunapoingia kwenye Mpango wa Tatu maana yake ni nini? Dira ya Taifa 2025 inakwisha kesho. Kwa hiyo, kuna jukumu la kuhuisha Dira mpya ya Taifa na hapa tujiangalie, kanuni iliyotupa ushindi leo kesho inaweza isifae. Tunaweza kuwa tunajivuna na rasilimali ambazo kesho zitakuwa ni obsolete. Tunazungumza chuma ikaja dunia isiyohitaji chuma, unazungumza petrol yanakuja magari ya hydrogen na umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima leo katika Mpango huu wa Miaka Mitano tutenge kipindi tuzungumze Dira mpya ya Taifa, tuhusishe watu wengi. Hii ni lazima muiweke kwenye mpango kwa sababu tunapanga kesho ijayo, the fourth industrial revolution inazungumza mambo yanatisha watu wanaanza kulima bila kutegemea udongo, watu wanaendesha viwanda vinavyotumia watu wachache lazima tujipange tunajua tunakwenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napomalizia katika mpango wa mwaka mmoja Serikali wanasema watakwenda kumaliza matatizo ya ardhi Kagera kwa kutoa hekari 7,000 kwa JKT SUMA na hekari 22,000 kwa vijiji vya Misenyi. Kagera haigawanyiki, Kagera ni moja. Huwezi kumaliza tatizo la Misenyi bila kumaliza tatizo la Muleba, Karagwe na Bukoba Vijijini. Huu mpango kama unamaliza Misenyi afadhali uachwe, mnapoifuata Kagera muifuate Kagera nzima. Ukimaliza tatizo la Misenyi litahamia Bukoba utakuwa hujatatua tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoweza kumaliza mgogoro wa ardhi Kagera siyo pesa ni ushirikishwaji wa wananchi. Sisi Wabunge ndiyo viongozi wa wananchi mtushirikishe, mnahitaji siku 15 mgogoro umekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja tuendelee kuuchakata. (Makofi)