Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mungu sana kunipa wasaa huu wa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake, Waheshimiwa Mawaziri Mheshimiwa Jenista pamoja na Mheshimiwa Angela Kairuki; Manaibu, Mheshimiwa Ikupa pamoja na Mheshimiwa Mavunde, lakini Makatibu Wakuu Ndugu Nzunda, Ndugu Massawe pamoja na Dada Doroth. Tunawapongeza sana kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Chama Cha Mapinduzi ni kweli kinalea watu vizuri. Ukitazama wakati ule anatoka Mheshimiwa Mizengo Pinda na anaingia Mheshimiwa Majaliwa alikuwa mtu mpole, mtulivu, mwanamichezo tena alikutwa uwanjani; watu wengi hatukufikiri kwamba, Mheshimiwa Majaliwa angeweza kukimudu kiatu cha Mzee Pinda, lakini leo ninapochangia hotuba ya mwisho ya Mheshimiwa Waziri Mkuu nataka nichukue fursa hii kukupongeza sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kiatu umekivaa kimetosha, lakini umekuwa Mheshimiwa Majaliwa yuleyule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtakubaliana nami kwamba, Mheshimiwa Majaliwa cheo hakijamvaa, amebaki kuwa Mheshimiwa Majaliwa, mtu mpole, mtu anayeheshimu kila mtu, mtu anayefanya kazi zake kwa utaratibu mzuri. Mheshimiwa Majaliwa tunakupongeza sana na kweli Chama Cha Mapinduzi ni msitu, kinatoa viongozi wakutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mengine unayowasikia watu wanajaribu kuamsha tu moral ya wapiganaji ili waingie kwenye uchaguzi walao wakiwa na moral, lakini nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Rais timu aliyoipanga, hili Baraza la Mawaziri linalofanya kazi wakati mwingine mpaka usiku wa manane limeiweka CCM katika hali nzuri ya kuingia kwenye uchaguzi tukiwa na ushindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chama chetu kingepwaya kama ninyi msingepambana, lakini Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Mawaziri mmepambana katika sekta zote; sekta ya afya, sekta ya ardhi, sekta ya madini, sekta ya uwekezaji, yaani mmetuweka katika mazingira mazuri ambayo wapinzani wetu sasa hoja hawana wanakimbilia kwenye vitu vidogovidogo kama kutafuta refa awe huru, refa awe nini, ukishaona timu inakimbilia kwa refa, jua jiyo timu tayari iko taabani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba, uchaguzi tu joto la uchaguzi ndio linalosababisha unaona tume sasa inaitwa sio huru. Sijui utawapata wapi, juzi tumeona kiongozi mkubwa kabisa tena anayeongoza upinzani Bungeni akiteuwa watu anasema nimekuteuwa kuwa Katibu Mkuu na watu wanapiga makofi. Anasema nimekuteuwa Mheshimiwa Heche kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na mziki unafuata, “Mbowe tubebe”, wala hakukuwa na tume, alikuwa mwanaume mmoja anafanya uteuzi na watu wote wanapata nafasi. Aah! Sasa leo hii wanazungumza kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana tumeona. Maana hivi vitu sio siri unaona wazi…

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde na hapa Bungeni wanashukuru kuteuliwa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, naona kabisa na uteuzi umekuwa mzuri kwa sababu Wabunge wanaume hawaaminiki sasa Mheshimiwa Mbowe karudi kwa wanawake ambao naamini kwamba, hawa wanaaminika kuliko hawa wanaume walioachwa kwa hiyo, amefanya vizuri kwa kweli. Nakubaliananaye kwamba, hawaaminiki kwa sababu, hata kwenye chai ukikutananao kuna wengine wana mpango wa kuhama mwishoni kwa hiyo, Mheshimiwa Mbowe yuko sawa kabisa kuwaacha hawa wanaume na kufuata akinamama, yuko sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasema kwamba, jambo zuri wangelifanya baadhi ya Wabunge wa upinzani kama alivyofanya Profesa. Profesa ameonesha, unajua kama unaona maji mazito aga, jamani tumieni Bunge hili kuaga kuweni wastaarabu; hivi saa hizi unaomba lami kweli jamani, Bunge hili unaomba lami? Hiyo game imeisha hiyo, game imeshaisha hapa tunajadili uchaguzi, keshokutwa Rais anakuja anasema Bunge limevunjwa, wewe unaomba lami kilometa 70, taabani hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwashauri tutumie haki ya kidemokrasia wakati mwingine kuaga. Ukiona maji yamezidi unasema jamani eeh!, kama alivyosema mama kwamba, jamani naomba niwashukuruni safari ijayo sitakuwepo na wewe tumia zile dakika tatu ambazo umemuachia nina hakika huyo Mbunge atatumia kuaga badala ya kuendelea hata kuzungumza mambo mengine.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mama Anna, Profesa Tibaijuka.

T A A R I F A

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, asante sana, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Lusinde kwamba, mimi sikuaga kwa kuwa maji ni marefu, kule Muleba Kusini niko imara kabisa, nimeaga kwa sababu ninang’atuka, naomba kuwasilisha. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mhshimiwa Spika, mama maji kule mazuri si tuko CCM mama, nazungumza ambao hawako kwenye chama hicho ndio ambao maji yanazama mama yangu, sizungumzii wewe Profesa. Wewe ungepita bila kupingwa. (Makofi/kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimeona hapa Wabunge wanazungumza kwamba, ooh, magereza wanapiga wanawake. Jamani magereza hawawezi kupiga wanawake, Jeshi letu la Magereza haliwezi kupiga wanawake hata siku moja, Jeshi la Magereza linashughulika na wahalifu sio jinsia, halishughuliki na jinsia ya mtu. Kwa hiyo, akiwa mhalifu mwanamke wanachukua, akiwa mhalifu mwanaume wanachukua, yaani wao hawashughuliki na jinsia wanashughulika na matatizo kwa hiyo, nataka niwapongeze sana Serikali hii kwa kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeona namna ambavyo mwaka huu mvua imekuwa kubwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ndio inashughulikia maafa. Barabara nyingi za Wabunge, hasa zile za vijijini, barabara zimegeuka mito kwa hiyo, tunaomba muiwezeshe TARURA kwa haraka ili itengeneze barabara za kwenda kukusanya kura maana hizi kura tutazifuata vijijini kwa hiyo, barabara zitengenezwe ili watu waweze kufika, wafike Manda, wafike kule Mvumi Mission lile daraja litengenezwe, wafike kule chini Loje kule tukusanye kura za Mzee Magufuli, habari ya uchaguzi na hoja mnaziona hapa hazipo.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya matumizi ya fedha, maana kukusanya kitu kingine, lakini nidhamu jambo jingine. Tumeona namna ambavyo kwa kutumia pesa zetu za ndani kila kijiji kinapata umeme kwa sababu, ya nidhamu ya mapato na nidhamu ya matumizi. Tumeona namna ambavyo migogoro ya ardhi inashughulikiwa na Mawaziri mpaka usiku wa manane kwa sababu ya nidhamu ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa watu waliofanya, nataka niseme, CCM haiwezi kujisifu kwamba, inapendwa ila vitendo vinavyofanywa na viongozi wa Serikali vinaonesha chama hiki kinapendwa. Chama Cha Mapinduzi kadiri mtakavyotenda mema ninyi Mawaziri mnaturahisishia kazi, tunakaa kwenye mserereko wa kuingia moja kwa moja, yaani kama ni meli iko kwenye chetezo inaingia tu baharini. Sasa hapa tunashindana na nani jamani hii hali mnavyoiona hivi? Hamna kitu na ninataka niwaambie wakati mwingine watu wasiseme tunafuta demkrasia, hatufuti, timu ya mpira wa miguu inajifuta yenyewe kwa kufungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na timu hapa inaitwa Zimanimoto, iko wapi? Tulikuwa na timu inaitwa CDA, imefungwa na ndivyo ambavyo hawa mwezi wa 10 tunakwenda kuwafungilia kwa mbali na kuwashusha daraja, wala sio kwamba, kwa kufuta demokrasia ni nguvu tu; kazi imefanyika Watanzania wameamini, wamekiamini Chama Cha Mapinduzi wanakwenda kukichagua Chama Cha Mpinduzi, sio suala, lazima tuwambie hapa wazungu. Hatufuti…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Lusinde nafikiri tutakubaliana kwamba, mkimuona ile suti yake ilivyokaa kwa kweli, ni kiwango. (Makofi/kicheko)

Ilikuwa ni kengele ya kwanza tu Mheshimiwa bado unaendelea na dakika zako, malizia. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, tunakushukuru wewe kwa kuongoza Bunge vizuri, Bunge limeongozwa kisayansi. Ule upinzani wakukurupukia hoja ndogondogo hizi oooh! Ufisadi, haupo sasa kwa sababu, nidhamu iko Serikalini kwa hiyo, maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, maana yake Watanzania sasa wanakwenda kufanya uchaguzi mwepesi ndio maana mnaona sasa inalalamikiwa tume. Hoja iliyopo sasa sio CCM mafisadi, hoja iliyoko sasa sio CCM kuna wizi wa fedha, hoja iliyoko sasa sio CCM wameshindwa kumaliza migogoro, aah aa, hoja iliyoko ya refa, wanataka refa, sasa huyu refa anatoka wapi? Atatoka nchi gani refa atakayesimamia uchaguzi? Mbona kwenye chama chao hawatuoneshi namna ambavyo wanafanya uchaguzi? Tunaona tu mwanaume mmoja kwenye clip anasema nimekuteuwa kuwa Katibu Mkuu, nimekuteuwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, nimekuteuwa, halafu na kanyimbo kanamsindikiza; mbona hawabishi kule wanakujaje kubisha huku?

Mheshimiwa Spika, Tena huku hakuna uteuzi, huku ni shughuli tu. Unaenda kuomba kura, unapewa kura shughuli zinaisha. Kwa hiyo, nataka nikuombe Bunge lako hili tujipange kuhakikisha kwamba, mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, habari ya corona imezungumzwa hapa, ninachotaka mtusaidie tu, maana mnaposema kila mnayemuhisi ana corona mnampeleka kwenye kambi na wagonjwa wako kwenye kambi. Sasa hapa watusaidie maana kuhisiwa sio kuugua, unaweza ukahisiwa una corona halafu ukapelekwa kwenye kambi yenye wagonjwa wa corona, sasa pale unakuwa tena umepelekwa kupata corona au umepelekwa kusaidiwa?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ingekuwa vizuri Serikali ikatuonesha kambi tofauti kwamba, kambi fulani iwe kwa ajili ya wanaohisiwa tu, haina mgonjwa. Kambi fulani hii ni kwa ajili ya wagonjwa tu, haina mtu anayehisiwa na kambi fulani wanapelekwa hotelini wale waliotoka nje, lakini mkisema tu kila mnayemuhisi, Mloganzila, wagonjwa Mloganzila, eeh ee!

Mheshimiwa Spika, sasa tunapata shida hapa. Ni lazima kuwe na tofauti ya mtu anayehisiwa na mtu anayeugua, ili tusije tukachukua watu tunaowahisi tukawapeleka kwenda kuugua badala ya kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la mwisho nakushukuru sana, umefanya kazi kubwa, umeliongoza Bunge kisayansi. Na hata wale ambao walikuwa na mashaka na wewe wakati unaingia mashaka wameondoa, wamegundua kwamba, Mzee Ndugai ni mzee wa viwango. Anaweza kulibadilisha Bunge hata akina Lusinde sasa tunabofya tu, maana mwanzoni tulikuwa tunaonekana mimi na Bwege labda tutapata shida katika kubofya, lakini watu wako wametusaidia mpaka mimi na Bwege sasa tunabofya na tunaingia humu ndani na mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)