Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Justin Joseph Monko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuanza kuchangia bajeti kuu ya Serikali katika siku ya leo. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nami fursa ya kuweza kusema leo mbele ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara kwa namna ambavyo wametuletea bajeti ambayo kwa kweli imekidhi mambo mengi ambayo Wabunge tumekuwa tukiyatafuta kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ambaye ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali hapa Bungeni, kwa namna ambavyo wamesimamia Wizara na kuweza kuleta bajeti ambayo kwa kweli imegusa kwenye maeneo mengi ya muhimu hasa katika Sekta za Miundombinu ambayo ni chachu kubwa sana ya maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais, kwa kitendo chake cha kukutana na wafanyabishara na makundi mbalimbali ambayo ni muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Taifa letu la Tanzania. Amefanya jambo jema. Ombi langu na wito wangu kwa viongozi wengine, wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri walioko hapa, Wakuu wa Mikoa na baadhi ya viongozi wengine huko, wasisubiri tena Mheshimiwa Rais aendelee kuwaita watu Ikulu na kuzungumza nao kusikiliza kero zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo kero nyingi, leo kaongea na wafanyabiashara, kesho na kesho kutwa walimu watakuwa na kero, wakulima wanzo kero zao, hatuwezi kusubiri Mheshimiwa Rais aweze kuita makundi yote haya na viongozi wapo. Kwa hiyo, wachukue hatua ili waende kutatua kero za wananchi kwa kuwasikiliza na siyo kutoa tu maelekezo peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ya mwaka huu imegusa kwenye maeneo mengi. Mimi nitazungumzia kidogo upande wa Sekta ya Kilimo. Waheshimiwa Wabunge, waliotangulia wamesema bajeti kwa upande wa kilimo kwa kweli ni ndogo. Nami niseme, sitaki kuzungumza sana, mwaka 2018 nilisema sana kuhusiana na takwimu za bajeti ya kilimo, lakini naomba sana, kilimo ndugu zangu kinahitaji kuongezewa bajeti kwa sababu kinachukua zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania. Ni muhimu sana tukaona namna ambayo tunaweza tukaboresha kilimo chetu sambamba na viwanda ambavyo tunavifungua sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda ambavyo tunavianzisha haviwezi kuwa na tija, kwa sababu mwelekeo wote ni wa viwanda ambavyo vitatumia malighafi za mashambani au malighafi za kilimo. Kwa hiyo, naomba sana, tuboreshe kilimo chetu na hasa kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wetu bado wanateseka. Tanzania yetu, wakulima wengi ambao tunawategemea ni wakulima wadogo wadogo, sio wakulima wakubwa. Hawa ndio wanahitaji kuangaliwa namna ya kuweza kuboresha mazingira yao, wanahitaji kusaidiwa ili waweze kupata pembejeo, wasaidiwe waweze kupata mbegu na vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumekuwa hata na uvamizi wa ndege ambao baadaye wanavamia mazao. Serikali inapaswa kuchukua jukumu la kuweza kuwasaidia wananchi hao kwa sababu hawana uwezo wa kupambana na wadudu waliokuwepo pamoja na ndege wanaoshambulia mashamba yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie zao la alizeti ambalo kwa kweli ni zao kubwa kwa Mkoa wetu wa Singida na hususan Jimboni kwangu. Zao hili la alizeti bado linazo kero kadhaa ambazo naomba sana Mheshimiwa Waziri mtusaidie kuziondoa. Tunawapongeza sana, mmeondoa kero zaidi ya 54 katika bajeti ya mwaka huu ambazo zinawasaidia sana wananchi. Hata hivyo, katika zao la alizeti, kwa mfano mashudu sasa hivi bado yanakuwa na ushuru wa mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mashudu siyo mazao, ni byproduct ya alizeti. Kwa hiyo, sasa mtu anapokuwa amenunua alizeti, amelipa ushuru wa mazao, halafu baadaye tena kwenye mashudu, anakuja kuchajiwa ushuru wa mazao, nadhani hizi zinakuwa ni kero. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye mashudu, tunayo pia tozo ya shilingi 20,000/= ambayo inatolewa na Wizara ya Mifugo. Pale ambapo unataka ku-export mashudu, wanapotaka ku-export mashudu kuna tozo ya shilingi 20,000/= kwenye Wizara ya Mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye Tume ya Atomic, pia iko tozo kwa ajili ya radiation, lakini tozo hii siyo requirement ya wanunuzi kule nje. Kinachofanya sasa, matokeo yake sasa, bidhaa yetu hii ambayo ni byproduct ya alizeti inakuwa siyo competitive kwenye masoko ya nje. Tumeona hapa tumeongeza sana ushuru kwenye bidhaa zinazotoka nje, lakini tuone kwa sababu watakaokwenda kuzitumia bidhaa hizo ni Watanzania hawa hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna nia na lengo zuri sana la kuweza kulinda viwanda vyetu vya ndani, lakini tukumbuke Kenya watafanya hivyo, Uganda watafanya hivyo na nchi nyingine zitafanya hivyo, nasi pia tunataka tuuze nje. Jambo kubwa ambalo tunatakiwa kufanya ni kuona namna ya kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa zetu, siyo kuongeza zaidi tozo kwa bidhaa zinazotoka nje, lakini tukiweza kupunguza gharama za uzalishaji, tutaweza kushindana kwenye soko..

Mheshimiwa Naibu Spika, Soko hili ni huru. Kwa hiyo, moja ya vitu ambavyo vinafanya gharama zetu zinakuwa kubwa, ni hizi tozo ambazo sisi tunaona kwa kweli hazisaidii na hazina tija kwa wananchi na pengine hata kwa Serikali. Sidhani kama zina ongezeko kubwa sana zinaweza zikawa zinaongeza mapato, lakini zinawafanya wafanyabishara wanaanza kukwepa na kinakuwa ni chanzo pia hata cha kushawishi kwenye masuala rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Wizara kuziangalia tozo hizi ili iweze kuziondoa ili ikishaziondoa wananchi wetu, wakulima, kwa sababu mashudu yakipata bei, alizeti itapata bei. Alizeti ikipata bei, wananchi wetu watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wameanza kukimbia zao la alizeti sasa. Hata Mheshimiwa Kiula hapa, yeye ni mkulima mzuri, sasa ameanza kulima dengu. Wanaogopa kwa sababu limekuwa ni tatizo. Mbegu ni gharama kubwa, halafu ukishalima pembejeo ni tatizo, ndege wanashambulia, lakini bei yake inakuwa ni ndogo mno. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ijaribu kuangalia, vyanzo vingine na kufuta tozo hizi ambazo kiukweli hazina tija sana kwa ajili ya wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, naunga mkono hoja, bajeti hii ya mwaka huu ambayo iewasilishwa, lakini naomba sana Wizara ifanye marekebisho ambayo nimeyaomba kwa niaba ya Watanzania, ili kusudi kuweza kulinda kweli viwanda vyetu na kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanaweza wakanufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)