Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kutoa mchango wangu. Lakini kwa namna ya juu kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufaya kazi hii; na ninawapongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na timu yenu nzima, hongereni kwa kazi mnayofanya.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani, miongoni mwa mambo ambayo iliyafanya kwa nguvu kubwa kabisa ni kuweka amri ambazo zilisaidia kwenye utekelezaji wa sheria kwenye mambo ya hifadhi ambayo ilihusiana na mifugo, kwa sababu ilikuwa inaingia kule, lakini pia na habari ya uvuvi. Ni jambo zuri, kwa sababu sheria ni namna tu mlivyokubaliana namna ya kuishi na namna ya kuhusiana lakini amri ndiyo lile karipio linalotoka kwenda kuhakikisha watu wanafuata sharia; kwa hiyo hilo nalipongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, mimi ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba sasa tumepata muda wa kutosha wa kuweka amri ili sheria zitekelezwe na ushahidi uko wazi, kwamba sasa amri zinaanza kuzaa matunda. Nitatoa mfano wa Biharamulo; Biharamulo ni Wilaya ambayo asilimia 46 ya eneo lake ni eneo lililohifadhiwa; kwa maana ya Burigi, Biharamulo na Kimisi; kwa hiyo asilimia 54 ya eneo iliyobaki ndiyo kwa ajili ya shughuli nyingine za uchumi, nasema nyingine kwa sababu uhifadhi nao ni shughuli ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu hiyo, kwa sababu ya kitovu hicho cha hizo hifadhi tatu, wakati wa zile vurugu za kuondoa mifugo kutoka kwenye hifadhi ili habari ya uhifadhi iende vizuri Biharamulo ilikuwa ni kitovu cha mapambano kati ya hifadhi na wafugaji, ilikuwa vurugu kubwa sana. Lakini sasa mimi ni mmoja wa mashahidi kwamba ni kweli kuondoa wale ng’ombe hifadhini kumeanza kuleta tija.

Mheshimiwa Spika, juzi hapa mmeona kuna picha ilikuwa inatembea kwenye mitandao, kuna ndovu mmoja amegongwa na gari barabarani, nafikiri ni upande wa Karagwe, hiyo ni ishara kwamba wanyama hawa tunaowahifadhi wameanza sasa kuwa wengi na sasa wanaanza kuonekana hata kwa ngazi hiyo. Lakini faida hiyo tunayoipata upande wa hifadhi hebu twende na upande wa pili, upande wa wafugaji nako tutafute sasa kwenda hatua ya zaidi baada ya amri sasa tuanze kuwekeza kwenye mambo ambayo yataongeza tija.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka kabla ya zile vurugu za hifadhi na wafugaji mimi nilikuwa nimepata fursa ya kuongea na mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii; walikuwa tayari kuja kukaa na Chama cha Wafugaji Ukanda ule wa Wilaya za Biharamulo, Ngara, Karagwe, Chato, Muleba, ili kuona ni namna gani eneo dogo tulilonalo la asilimia 54; kwa sababu tunafanana wilaya hizo; litatumika kwa tija.

Mheshimiwa Spika, unakuta mkulima ana eka kumi, analima tatu, eka saba hazitumii lakini anasema hizi ni za kwangu. Lakini hapo kuna fursa ya kuweka uwekezaji ambapo utapata zile nyasi nzuri za ng’ombe kutumia, kwa hiyo kwanza ukaongeza mahusiano mazuri kati ya mfugaji na mkulima, lakini ukaweka namna ambapo hata wote wawili wanaweza kushiriki kwenye ushuru na kodi kwa mfumo ambao ni rasmi.

Mheshimiwa Spika, wakati mifugo ipo hifadhini ilikuwa ni kukimbizana tu, wanakimbizana, wanatoa rushwa, wanaleta kesi na nini. Mimi nimezungumza sana na hiki chama cha wafugaji; pesa iliyokuwa inazunguka kwenye kesi na rushwa, hiyohiyo ukiigeuza ikawa kodi ni uchumi mkubwa sana. Sasa nakuomba Mheshimiwa Mpina, hebu tuanze na ukanda ule kama mfano, njoo tukuelekeze, tunaongea vizuri na chama cha wafugaji. Bahati nzuri wakishakuwa na chama ni fursa kwamba wana sauti moja, njoo tuzungumze tuondoke kwenye hiyo hatua, tumeshafanya vizuri kwenye hatua ya sheria na amri, sasa twende kwenye hatua ya tija ya hizo sheria na amri zianze kuchangia kwenye uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimefurahi, kwenye hotuba yako, sikumbuki ni ukurasa wa ngapi, umezungumzia namna ambavyo sasa nyama tunayoleta kutoka nje ya nchi imeanza kupungua, na ninadhani huo ndiyo uwe mwelekeo. Juzi mimi nimemsikia Mheshimiwa Rais anatoa maelekezo kwamba baadhi ya watu, hasa viongozi wa Serikali, pamoja na kuwa na laini nyingine za simu;nataka nitumie kama mfano; lakini lazima wawe na laini za TTCL kwa sababu wao ndiyo wadau wakubwa wa hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuna mtu mmoja akawa anaona kwamba ni jambo limekaa vibaya, lakini mimi nikajiuliza; nina ndugu yangu aliwahi kufanya kazi Airtel, alikuwa ananiambia wao kwa mwezi Airtel wanawapa airtime kwa ajili ya mawasiliano. Na jana nikamuuliza hivi ilitokea siku moja Airtel wakakupa airtime ya Tigo wakati wewe unafanya kazi Airtel? Akasema hapana. Kwa hiyo hiki kinachofanyika mimi nafikiri ndio mwelekeo. Hebu tutafute kuinua mambo ambayo kwanza ni ya Umma halafu twende upande wa pili, siyo kwamba Private Sector tuiue.

Mheshimiwa Spika, sasa niilete kwenye muktadha wa ufugaji. Ukiangalia viatu, mikanda, mabegi tunayotumia hapa Watanzania ni uchumi mkubwa sana unazunguka. Jana nimemsikia Mheshimiwa Mbunge mmoja anasema tutafute soko nje, lakini mimi nasema tuanze na soko la hapa, hebu starve yale mambo ya nje weka nje huko, tuhakikishe hapa mikanda, viatu, mabegi tunatumia hapa. Tuki-starve supply kutoka nje, hapa soko liki-starve wawekezaji watafanya kazi nzuri, na muwape support, itafikia hatua hata ng’ombe wako akipotea unakuta ameshachunwa watu wanakwenda kutengeneza mikanda kwa sababu mikanda haitoshi, utakuwa umetengeneza soko la hapa.

Mheshimiwa Spika, lakini tuwasaidie na wafugaji sasa; jambo lingine katika ile niliyosema kuongeza ubora; hebu tuondoke kwenye habari ya ng’ombe, kuna mtaalam mmoja alikuwa ananiambia hapa kwamba sio kila ng’ombe ambaye nyama yake itakuwa nzuri, nyama inawekwa inavutwa hivi kama mkanda, ng’ombe anafugwa miezi 18, 16 ni nyama. Sasa sisi hapa unakuta ng’ombe ana miaka tisa, yaani tangu azaliwe anakuja kuchinjwa siku ya graduation ya Form Four ya binti au kijana aliyezaliwa wakati ng’ombe ananunuliwa. Kwa hiyo tutafute namna ya kuanza ku-transform ili habari ya nyama iwe ya kiwango hicho. Utaacha kununua nyama kutoka nje kuleta Serena na kwingine na mambo mengine kama hayo.

Mheshimiwa Spika, nimeskia hapa, kwenye ukurasa fulani hapa, sikumbuki, tutaona, inasema asilimia 20 ya wafugaji wa nchi hii ndio wana access na extension services (huduma za ugani); lakini hata miongoni mwa hao asilimia 20 ni tija ndogo sana inayopatikana pamoja na huduma za ugani. Na hii inaashiria kwamba mambo aliyokuwa anasema Mheshimiwa Dkt. Nagu kama mfano, kwamba mara kuna dawa feki na vitu kama hivyo, inawezekana kweli yapo. Kwa sababu hata katika hiyo asilimia 20 ambayo wanapata huduma za ugani bado tija haipatikani, na hii nimeipata kwenye ripoti ambayo ni ya Serikali inaitwa Tanzania Livestock Modernization Initiative.

Mheshimiwa Spika, tumeona idadi ya ng’ombe inaongezeka, kwenye hotuba wanasema milioni 30 mpaka 32; mbuzi milioni 18, nadhani ni milioni, nafikiri niko sahihi; kondoo wanaongezeka. Lakini twende hatua ya zaidi, kutoka kwenye idadi kwenda sasa kwenye tija ya hiyo idadi. Namna gani sasa; hebu tuingize wawekezaji waende watengeneze ranchi ndogondogo kwenye maeneo ambayo wakulima…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Oscar Mukasa.

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)