Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kutuchagulia Mkaguzi na Mdhibiti kuu wa Hesabu za Serikali mpya na mchapa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwape udhibitisho; Ofisi ya CAG haikuwa safi kama walivyokuwa wanaifikiria. Nataka niwape mfano; mfumo wetu wa ukaguzi katika halmashauri zetu ukaguzi wa miradi unafanyika kwa sampling, yaani katika miradi kumi unakaguliwa miradi mitatu, ile miradi mitatu ndiyo inatoa remarks ya ile miradi kumi; sasa pale ndipo mianya ya rushwa inapopitia. Inatolewa pesa inakaguliwa miradi mizuri mibovu inaachwa, hatimaye remarks inatoka hati safi lakini vitu vinakuwa hovyo. Kwahiyo naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutuchagulia CAG mpya; na napenda nimuambie kuwa aendelee kufanya reform katika ofisi ya CAG ili wananchi wapate haki zao na huduma wanazostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili nataka niongelee elimu. Tanzania ina idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kuwa milioni 55 na watu wazima wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 25, lakini production iliyoko katika nchi yetu haiendani na idadi ya watu waliopo; kwanini idadi ya watu haiendani na production iliyopo? ni kwasababu kubwa ya elimu ambayo wanaipata; yaani mitaala yetu ya elimu hai-fit nchi yetu ya Tanzania na nje. Kwa mfano shule ya msingi wanafunzi wanafundishwa darasa la kwanza mpaka form four lakini akienda mtaani hawezi hakafanya kitu kwa sababu mitaala ya elimu haimuruhusu yeye kwenda kuwa productive katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napendekeza mwanafunzi wa darasa la kwanza mpaka form four ukiacha masomo ya msingi anayosoma awe anapewa elimu ya msingi ambayo itamwezesha kutumia rasilimali inayozunguka maeneo yake. Kwa mfano, maeneo ya Kanda ya Ziwa wanafunzi wa elimu ya msingi wafundishwe uvuvi na uchimbaji wa madini ya dhahabu; maeneo ya Lindi wafundishwe kilimo bora kama cha korosho; maeneo ya Mara na Singida wafundishwe uvuvi wa kisasa; Dodoma wafundishwe uvuvi wa kisasa katika elimu ya msingi ili asipoendelea chuo aweze kupambana na maisha; maeneo kama Rukwa wafundishwe tiba asili. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa chuo kikuu, leo hii tumeshuhudia wanafunzi wanaomaliza chuo kikuu ni zaidi ya laki tano kwa mwaka lakini hawa wanafunzi wanapokwenda mtaani…

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, mnacheka lakini tiba asili inalipa kwelikweli.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo.

MWENYEKITI: Worldwide inalipa sana.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Sawasawa.

MWENYEKITI: Kabisa, angalieni dawa za Mchina ziko dunia yote. Endelea Mheshimiwa Mlinga, walikuwa wanacheka dawa za asili kwa Rukwa lakini mimi nawaambia ile ni mtaji mkubwa. Ukienda Nairobi unakuta mabango yameandikwa mganga maarufu kutoka Tanzania (Rukwa). Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hata wale wenye shida ya nguvu za nanihii tiba asili ndiyo imekuwa mtatuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa chuo kikuu, leo hii tumeshuhudia utitiri wa vyuo vikuu lakini kozi ambazo wanaziweka katika vyuo hivyo haziko productive katika nchi yetu. Leo hii tunasikia Wizara ya Elimu wanatangaza walimu wa arts hatuwahitaji tena lakini vyuo bado vinazalisha wanafunzi wa arts na bado vinakwenda kudahili wanafunzi tena wanapewa mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza mitaala yetu ya elimu ya chuo kikuu iwe inatolewa kulingana na mahitaji ya nchi yetu. Kwa mfano, mtu anamaliza Business Administration hawezi kuanzisha hata genge la nyanya; mtu anamaliza Public Administration hata uongozi wa familia yake hawezi, watoto wanavuta bangi. Wanasheria, tumeshuhudia wako Wabunge wanasheria lakini wanaongoza kwa kufanya makosa, kila siku wako mahakamani.

Kwa hiyo, napendekeza hata vyuo vikuu mitaala iendane na mahitaji ya nchi yetu yaani watu wanapotoka hapo wawe productive na siyo kuvunja sheria na mambo mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la mapato napendekeza kwenye kipengele kimoja tu, tunapoteza mapato mengi sana katika nchi yetu. Nitolee mfano, tuna madereva wengi sana katika nchi yetu zaidi ya laki tano, lakini wengi wameajiriwa katika ajira ambazo siyo rasmi. Kwa mfano, madereva teksi wako zaidi ya 4,000 hawalipii kodi, NSSF wala matibabu. Madereva wa daladala zaidi ya 20,000 hawalipi kodi. Madereva wa mabasi makubwa zaidi ya 5,000; madereva wa mabasi ya kati zaidi ya 5,000 na madereva wa Noah zaidi ya 16,000 lakini hawalipi kodi. Napendekeza kwa mfano vile vitambulisho tulivyowapa Wamachinga tungewapa na madereva ili wawe wanalipia hata laki moja kwa mwaka ili iwe kwa ajili Pay As You Earn, NHIF na NSSF ambayo itawasaidia hata wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nataka nipendekeze kwenye utafiti. Benki yetu Kuu ya Tanzania tuna Kitengo cha Utafiti lakini wanafanya tafiti matokeo yake ripoti wanazifungia kwenye makabati. Tumeshuhudia tuna mazao kama tumbaku ni crisis katika soko; tuna korosho ni crisis katika soko; tuna pamba crisis ni katika soko, lakini BoT tangu imeanzishwa kuna Kitengo cha Utafiti, sasa tuwaulize wanafanya nini zaidi ya kupokea mishahara tu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza tafiti wanazozifanya BoT katika mambo mbalimbali ya mining, kilimo, biashara, hizo ripoti wawe wanaziweka wazi. Tuna matajiri katika nchi yetu; ikusanye matajiri na benki, iweke ripoti katikati itoe ushauri watu wakopeshwe hela matokeo yake wafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda EPZA nikakuta wanaagiza nyuzi kutoka India wakasema wao pamba inayozalishwa Tanzania yote zingekuwa zinatengenezwa nyuzi wana uwezo wa kuzinunua zote. Sasa waulize BoT wanashindwa kumshauri hata Mohamed Dewji akapewa mkopo akatengeneza kiwanda cha nyuzi akanunua pamba zote za Wasukuma zikatengenezwa nyuzi akapeleka EPZA wakaenda kuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunategemea nyuzi kutoka India wakati Wasukuma kule na watu wengine hawana sehemu ya kuuza pamba zao. Kwa hiyo, napendekeza hiki Kitengo cha Utafiti cha BoT wafanye kazi yao, waache kupokea mishahara waweke ripoti wazi matajiri tunao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono. (Makofi)