Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchnago wangu wa maoni kwenye mapendekezo ya Mpango na muongozo wa Mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa jinsi ambavyo wameleta mapendekezo haya na hasa hasa jinsi ambavyo amewasilisha kwa ufasaha mapendekezo haya na niseme tu kwamba bahati nzuri sisi katika Nchi yetu tumebahatika sana kuwa na nguli wa mipango tangu wakati wa uhuru mpaka leo. Nchi nyingine zimekuwa zinakuja kujifunza uandaaji wa mipango katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka tangu enzi za wakina Dkt. Justina Rweyemamu, wakina Profesa Kigoma Malima na sasa Dkt. Mpango, mipango yote imekuwa ni mizuri, kwa kweli ni mizuri sana hata ukiitaza, ukisoma mpangilio wake, malengo, shabaha imekuwa ni mipango ambayo kwa kweli inalenga kumkwamua Mtanzania kutoka kwenye umasikini na kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mipango yetu kuanzia mwaka 2000 tulipoanza kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa, ule mpango wa kupunguza umasikini ambao ulilenga huduma za jamii, uje kwenye MKUKUTA wa kwanza, uje kwenye MKUKUTA wa pili ambao uliunganishwa na mpango wa kwanza wa miaka mitano kwa kweli mipango yote imekuwa ni mizuri sana na leo hii tunakaribia kuhitimisha Awamu ya II au mpango wa pili wa miaka mitano kuelekea kwenye mpango wa tatu wa miaka mitano ili tuendelee kusaidia uchumi wa Nchi hii ufike katika ngazi ya kati ya uchumi Kidunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuko katika mwaka wa nne wa utekelezaji na mpango ambao unapendekezwa leo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha unatupeleka kwenye maandalizi ya mpango wa mwisho wa miaka mitano. Kwa kweli hili ni jambo ambalo tunatakiwa tujipongeze kama Taifa, tunakwenda vizuri. Nchi nyingine huwa wanaishia katikati, wanakuwa na mpango wa miaka 15 (long term) wakifika baada ya miaka mitano wanaacha wanaingia katika kutatua mipango mingine lakini sisi tunakwneda sequentially. Baada ya miaka mitano tunaingia Awamu ya II tunaingia Awamu ya III. Hilo ni jambo ambalo tunatakiwa tujipongeze kama Taifa. Kwa kweli kama nilivyosema mwanzo mipango yetu ni mizuri sana na kazi zinazopangwa kwenye mipango ni nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo au maoteo ya makusanyo huwa ni mazuri sana yanalenga kuhakikisha wkamba mpango unatekelezwa, matarajio ya Watanzania ni mazuri tatizo ambalo ninaliona katika utekelezaji ni dogo sana. Kwa mfano, hadi sasa katika utekelezaji wetu tumekaribia kutekeleza malengo mengi kwenye mpango. Ukiangalia mipango mikubwa, ufufuaji wa Shirika la Ndege, ujenzi wa miundombinu, ukiangalia utekelezaji kwenye sekta ya umeme, ujenzi wa reli, ujenzi wa minara ya mawasiliano na maeneo mengi sana, vituo vya afya, hospitali mpya, ujenzi wa madarasa, mabwalo na mabweni kwenye shule za msingi na sekondari na kwa kweli katika maeneo mengi tumefanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji, jambo ambalo naipa heko serikali yetu ni jinsi ambavyo tumebadilika kutoka zamani ambako wenzetu walipokuwa wanatufanyia tathmini. Kwa mfano, nirejee taarifa ya maendeleo ya Dunia (World development report) ya mwaka 2004 ambayo ilisema kwa sababu ilifanyika Tanzania hapa, ilisema fedha haziendi kwa watu masikini lakini ukiangalia utekelezaji wetu wa leo chini hasa ya Awamu ya Tano hii, fedha nyingi zimekuwa zinakwenda kwa watu masikini katika sekta ambazo zimezitaja. Walisema kwamba kuna matatizo ya nidhamu makazini, kulikuwa na absenteeism leo hii nidhamu kazini kwa kweli imeongezeka na mambo mengi ambayo waliyaona kipindi kile yamebadilika. Kwa hiyo, kwa kweli napenda sana kuipongeza sana Serikali yetu kwa kufanya kazi kubwa sana ambayo inalenga kumkwamua Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto bado zipo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha amezitaja changamoto, kwa mfano, changamoto kwenye ukusanyaji wa mapato kwamba bado kuna mianya, mapato yanapotea na ndiyo maana hatujawahi kufikia asilimia 100 ya makadirio ya makusanyo na sababu zilizotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni pamoja na uwepo wa njia za panya yaani Bandari bubu, ukwepaji mwingine wa kodi, wahisani kutotimiza ahadi kwa kweli haya mimi nilikuwa naomba sana Serikali yetu iyavalie njuga kuhakikisha kwamba hizi changamoto zinaondoka. Tufanye kila mbinu kuhakikisha wkamba changamoto hizo zinaondoka ili tuendelee kufanya vizuri zaidi katika kumuhudumia Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine iko kwenye ufuatiliaji na tathimini, hapo nataka nisisitize kidogo; kuna tofauti kati ya kutembelea mradi na kufuatilia mradi hasa kwa wataalam. Kiongozi anaweza akatembelea mradi kwa maana ya kuona kama ni ujenzi unaondelea lakini mtaalam anapotembelea mradi hapo ndiyo naona ni kioja. Mtaalam hatakiwi kutembelea mradi, mtaalam anatakiwa afuatilie utekelezaji wa mradi, kwa maana gani?

Mradi wowote ambao kwa mfano, unajengwa na Mkandarasi una mkataba sasa mtalaam anapokwenda kufuatilia mradi mkataba hajausoma huu, hana mkataba hapo ndiyo unapoona kioja. Lazima wataalam wetu wabadilike, kazima wanapokwenda kukagua miradi au kufuatilia miradi wawe na nyenzo za ukaguzi au nyenzo za ufuatiliaji ambao ni pamoja na mkataba, ambao ni pamoja na makadirio ya ujenzi au BOQ, ambayo ni pamoja na michoro ili ajionee je, huu mradi unaotekelezwa unafuata makubaliano ambayo yako kwenye mkabata na yaliyopo kwenye michoro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu jambo la pili ni tathmini; tathmini ambayo tumeizoea sana Serikalini na nchini kwa ujumla ni tathmini ile ya kila mwaka ambayo inafanyika kupitia bajeti kila Wizara inafanya tathmini yake na Mheshimiwa Waziri wa Fedha akija hapa huwa anahitimisha ile inaitwa budget review au mapitio au tathmini ya Mwaka ya utekelezaji wa Mpango wa Mwaka wakati anasoma bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mipango hii lazima kuwe na tathmini ya nusu mwaka au medium review, tathmini ya nusu muhula au midterm review. Kama kuna mpango wa miaka mitano inapofika nusu lazima ifanyike tathmini ya nusu ya utekelezaji wa muda wa ule mpango halafu mwishoni mwa muhula yaani kama ni miaka mitano, mwishoni mwa miaka mitano ifanyike tathmini ya kina ambayo itasaidia sasa maandalizi ya mpango wa miaka mitano inayofuata. Kwa kweli hapa tumekuwa kidogo tunatatizo ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwasababu analifahamu ningependa alipe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa tumekuwa tukipata vipaumbele vingi, lakini nikitazama kwa undani, tumekuwa tuna upungufu kwenye eneo la ardhi. Sekta ya Ardhi kwa upande wangu ndiyo sekta mama ya uchumi. Hakuna mtu atafanya ujenzi wa aina yoyote bila kugusa Sekta ya Ardhi. Watu wa kilimo wanafanya shughuli zao kwenye ardhi, mifugo, uvuvi, maliasili na utalii ni kwenye ardhi; madini yako kwenye ardhi. Sasa Sekta ya Ardhi kama hatujaipa kipaumbele, kwa mfano kwenye eneo dogo tu la maeneo ya uwekezaji, hilo litakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuipe kipaumbele Sekta ya Ardhi na Mheshimiwa Doctor, Mwalimu wangu anajua vizuri sana. Naomba sana, tunapoendelea kupanga vipaumbele vyetu tuikumbuke Sekta ya Ardhi. Huyu Waziri wa Ardhi tumsaidie aweze kutimiza matarajio ya Watanzania. Haiwezekani tuendelee kupima Dodoma na Dar es Salaam peke yake, lazima tupime miji yote ikae vizuri, makazi yakae vizuri. Halafu kule vijijini kuna miji ambayo inaibuka kwenye vijiji, ina ujenzi holela. Lazima tumsaidie Waziri wa Ardhi aweze kuratibu miji ambayo inaibuka vijijini iwe na makazi mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kila kipande cha ardhi Tanzania kikipimwa tutapata maendeleo ya kutosha kwa sababu ardhi itakuwa na thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani yangu ni hayo. Naunga mkono hoja, Ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)