Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia hoja hii katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, mgawo wa bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Ujenzi mwaka 2016/2017 ulikuwa shilingi trilioni 4.8, mwaka 2017/2018 shilingi trilioni 4.9, mwaka 2018/2019 shilingi trilioni 4.1 ambayo ni 34.5% ya bajeti yote ya maendeleo. Mpaka mwaka huu wa fedha unaisha Bunge litakuwa limeidhinisha jumla ya shilingi trilioni 13.8 kwa miaka mitatu.

Mheshimiwa Spika, napenda kujua ni sekta zipi nyingine za uchumi zimechochewa kutokana na uwekezaji huu kama viwanda, ni vingapi vimeanzishwa? Watanzania wangapi wameondokana na umasikini? Pato la Taifa limeongezeka kwa kiasi gani kutokana na uwekezaji huu?

Mheshimiwa Spika, sekta ya ujenzi. Kumekuwa na changamoto kwa wakandarasi Watanzania kutopata kazi za kufanya ndani hata nje ya nchi. Serikali ina mkakati gani wa kufanya wakandarasi hawa waweze kupata angalau asilimia 50 ya kazi za ndani ya nchi na hata za nje ya nchi?

Mheshimiwa Spika, TBA wanapewa kandarasi za Serikali na mara nyingi hawashindanishwi. Hii imefanya kazi zao kuwa chini ya kiwango na malalamiko yamekuwa mengi, Serikali ifanyie kazi suala hili.

Mheshimiwa Spika, barabara nyingi zimekuwa hazikamiliki kwa sababu fedha nyingi zinaenda kwenye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao unachukua muda mrefu sana. Wananchi wanaathirika kwa kutosafirisha mazao yao kwa wakati na uchumi kusuasua.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna ahadi za Mheshimiwa Rais kutekeleza ujenzi wa barabara za Mkoa wa Iringa, nikitaja chache barabara ya Rujewa – Madibira, Iringa Mjini – Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (kilometa 14) na Ipogolo - Kilolo (kilometa 133). Barabara zote hizi fedha za ujenzi bado hazijafika, kinachofanyika ni usanifu tu. Pamoja na utengaji huu wa fedha mnaouainisha, naitaka Serikali hii itekeleze ahadi hizi mapema ili wananchi wasipate adha.

Mheshimiwa Spika, bado nasisitiza uendeshaji wa Shirika la Ndege la ATCL ni wa hasara. Serikali iangalie suala hili kwa makini kwani kodi za wananchi zinazidi kuteketea.

Mheshimiwa Spika, mradi wa SGR vifaa vinavyotumika vinatoka nje ya nchi. Nashauri Serikali itumie malighafi kutoka hapa nchini. Kwa mfano, makaa ya mawe ambayo yapo Mchuchuma yangetumika katika mradi huu.