Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi hii niweze na mimi kuchangia katika hoja hii muhimu inayogusa maisha ya kila mwananchi katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda niishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo katika hii Awamu ya Tano tumeshuhudia mapinduzi makubwa ambayo na yeye pia amekuwa kiongozi shujaa katika kutatua matatizo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, napenda niwashukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu na wasaidizi wao kwa ujumla katika Wizara ya Maji kwa namna ambavyo wamekuwa wakichapa kazi kwa bidii na pindi wanaposikia matatizo wamekuwa mstari wa mbele kwenda kuangalia kuna matatizo gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kuchangia kabla sijasahau, la kwanza kabisa katika Mfuko wa Maji. Katika hali ya kawaida, mimi nafikiri hata Mheshimiwa Rais anatambua namna gani tulivyo na shida ya maji hasa tunaotoka vijijini. Anatambua kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwa Serikali hii iliyo sikivu tusiwe na kigugumizi, Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wamechangia kwa namna ya pekee, walivyoona umuhimu wa maji, sitaki kurudia michango yao. Naomba Serikali ichukue suala hili na ikalifanyie kazi ili tuone kwa namna yoyote ile ni mahali gani wanapata vyanzo vya mapato ili tuweze kupata maji ya uhakika hasa katika maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, napenda kuishukuru Wizara hii kwa bajeti iliyopita waliweza kunitengea katika Kata yangu ya Ikuba, Vijiji vya Kashishi, Itula ambavyo vyote sasa hivi vina maji. Sasa naomba, Kata hiyo tu ya Ikuba, Kata ya Usevya na Kibaoni ndizo zenye vyanzo vizuri vya maji na wanapata angalau maji safi na salama. Naomba katika Kata ya Chamalendi sina maji kabisa katika vijiji vya Maimba, Mkwajuni na Chamalendi yenyewe, na Mwamapuli katika vijiji vya Lunguya, Centre Pinda na Centre Clara. Mheshimiwa Kalobelo kama yuko hapa, vijiji vyote hivyo ninavyovitaja anavifahamu kwa sababu aliwahi kuwa Mkurugenzi wangu kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaombeni sana, sana, naomba Chamalendi mnipatie maji ya kutosha na visima. Sina maji kabisa kule, watu wanatumia maji yanayoporomoka katika Mto Msabya na yanayotoka katika Mto Kavuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaombeni sana, tupunguze matatizo ya wananchi wangu wa Kata ya Chamalendi, Mwamapuli ambao kila siku wamekuwa wakipigizana kelele na Askari wa TANAPA. Kwa hiyo, nawaomba sana, sana, tuondoe hiyo adha ya wananchi wale kugombana na TANAPA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nikirudi katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 23, mmeongelea uamuzi wa ujenzi wa mabwawa ya kimkakati. Niliwahi kuuliza hapa masuala ya umwagiliaji yako wapi? Hayaongelewi siku hizi huku. Nina umwagiliaji Kirida, nina umwagiliaji Mwamapuli, ambapo Mwamapuli mwaka 2017 mlitutengea hela ya upembuzi yakinifu kupitia Wizara ya Maji, lakini mpaka sasa sioni kinachoendelea. Ni mradi mkubwa na mradi wa Mwamapuli mliuondoa kwenye Halmashauri mkaupeleka kwenye mikakati ya Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa wangu Waziri wa Nchi uko hapa, wananchi wangu wale wana mashine na mitambo mikubwa ambayo takribani ina miaka saba haifanyi kazi kwa sababu hatuwezi kuendelea na kilimo kwa ajili ya mvua zilizoharibu ile mitambo. Nimesema ni umwagiliaji Kirida pamoja na Mwamapuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaongea hivyo najua utanijibu hicho kilimo, lakini ni masuala mtambuka; na utanijibu hicho kilimo kwa kunikwepa tu, lakini katika ukurasa wa 23 mmeandika kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji umeme. Katika kilimo cha umwagiliaji ndiyo nimeweka mradi wa Mwamapuli pamoja na wa Kirida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye uzalishaji umeme, nilimwomba Mheshimiwa Prof. Mbarawa aweze kukutana na Mheshimiwa Dkt. Kalemani waangalie ni namna gani tunaweza tukazalisha umeme katika Kata ya Majimoto, kwenye chanzo chetu cha Majimoto pale. Kwa hiyo, naomba pamoja na hii mipango mlioyoiandika humu, basi na Majimoto mpafikirie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi katika mradi wa kutoa maji katika Ziwa Tanganyika. Nimeona kabisa kwamba upembuzi yakinifu na tathmini ya athari za kimazingira na kijamii imeshafanyika. Tunasubiri nini sasa kuanza kufanya usanifu wa kina ili tupeleke fedha kule? Kwa sababu haya maji ninaamini yanakuja mpaka kwenye Halmashauri yangu ya Mpimbwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi wangu wa kule tatuwapunguzia adha ya kupata haya maji. Kwa hiyo, naomba tu, ni lini mtaanza kufanya huo usanifu wa kina ili tuweze kuanza mara moja namna ya kutafuta fedha kwa ajili ya kutoa maji Tanganyika kupita Karema, Mpanda, Kavuu na kufika Mpimbwe kabisa kule Jimboni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote, naomba niongelee suala lingine. Pamoja na kwamba nimeshaongea mambo ya Jimboni kwangu sasa naomba niongee kama mwananchi ninayetoka Mkoa wa Katavi. Naomba niongelee kuboresha mfumo wa maji katika Mji wa Mpanda, nimeona kuna fedha pale imetengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mradi wa Ikorongo, una miaka kadhaa, maji Mpanda ni tatizo. Ni mji pale, ni tatizo, ni tatizo ni tatizo, naomba litatuliwe. Wananchi wamekuwa hawataki kulipa bill kwa sababu tu maji wanapata mara moja kwa wiki; kwa sababu tu maji yanatoka mara moja kwa wiki. Huyo mtu akifanya mahesabu yake kwa bill na lita alizotumia, lazima atakukatalia kulipa bill. Mtaanza kuwakatia maji, mtagombana bila sababu za msingi. Kwa hiyo, naomba hilo pia mliangalie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala moja ambalo kwa mimi binafsi naona kama ni kero; ankara kutolewa kwa njia ya kielektroniki, yaani kwenye simu. Kwanini tusitoe karatasi pamoja na meseji kwenye simu? Kama mimi mwenye simu nimesafiri, basi nyumbani pale inabaki karatasi wale watu wanalipa bill, na siyo muda wote mtu atakuwa na simu mkononi kuangalia bill yangu imeingia ya maji ya mwezi huu, kwa hiyo lazima niende nikalipie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naowaomba mfanye utaratibu; na hizi ni Kanuni, siyo kwamba ni amri za Mungu. Hizi ni Kanuni tu tunatunga. Kwa hiyo, huo utaratibu mimi nimeona una malalamiko na una matatizo. Kwa hiyo, ni vema sasa mkatoa karatasi na pia mkatumia hiyo njia ya kielektroniki. Siyo muda wote watu wana simu kama hizo na nimekuwa nikisema kila wakati, kwa hiyo, nilikuwa nawaomba pia mwangalie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Oman ambayo imeleta mradi wa kuchimba visima 100 kwa shule za sekondari. Mimi kwangu sijaona hata shule moja. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri, nipatie sekondari hata mbili tu; au shule za msingi hata tano tu ili wale watoto kule wapate maji. Sina maji katika shule hizi. Sina maji katika shule za msingi wala za sekondari. Kwa hiyo, nawaomba, nipatieni hata visima viwili tu vya sekondari, vitano nipe vya shule ya msingi; vingine nitakuwa naomba pole pole angalau wanafunzi wangu wapate kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe ni mwalimu, nikienda naingia darasani kufundisha. Nikitoka natafuta kidumu cha mwanafunzi kiko wapi ndiyo ninawe maji chaki. Sasa hii siyo nzuri, naomba tupate angalau usawa. Kwa nini maeneo mengine yapelekewe hivi visima, maeneo mengine hayapati? Nataka tujue, mtakapokuja nawaomba kabisa katika hili mwangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la miundombinu. Wakandarasi wamekuwa wakinunua vifaa ambavyo siyo vizuri ni vibovu. Mpira badala ya class C, sijui mnatuletea mpira gani. Mwananchi au Mwenyekiti wa Kamati ya Maji Kijijini anajua huu mpira ni class C? Hiyo nayo iangaliwe.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia, malizia Mheshimiwa.

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Maombi yangu naomba yachukuliwe kama nilivyoyaleta kwako Mheshimiwa Waziri na ninaunga mkono hoja ili nipate maji. (Makofi)