Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. OSCAR R. MUKASA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI:
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwa mara nyingine na kwa uendelevu, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii tena, lakini nakushuru pia kwa kutuongoza vizuri hapa na kwenye kazi zetu zote za kila siku.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wachangiaji wote waliochangia taarifa yetu. Wachangiaji kwa ujumla walikuwa 35 lakini waliogusia taarifa yetu ni wachangiaji 10 ambao ni utashi mkubwa kabisa wa kisiasa kuonyesha kwamba Bunge letu wanatoa kipaumbele kabisa kwenye masuala ya UKIMWI ndiyo maana wametoa michango kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee pia nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri ambao wamezungumza; wamezungumza vizuri sana, unaona kabisa utashi wa kupokea kwa kufanyia kazi mapendekezo yetu mara pale ambapo yatakuwa yamepokelewa na Bunge lako Tukufu kwamba ni maazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwa namna nyingine tena naishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya. Tunaposema Serikali, tunamshukuru Mheshimiwa Rais na timu yake nzima, kwa sababu takwimu zinasema, preverence ya kwanza kabisa ya masuala ya UKIMWI nchi hii nafikiri ni mwaka 1992 au 1995, utanirekebisha, ilikuwa ni asilimia 7.2, lakini leo tunaongelea asilimia 4.7. Maana yake ni kwamba, pamoja na kwamba kazi bado ni kubwa mbele yetu, lakini kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliochangia, lakini kuna jambo moja ambalo ni vizuri tuliweke sawa ili tuwe na uelewa wa pamoja. Kuna Wabunge wamechangia vizuri sana kuhusu Mfuko wa Taifa wa UKIMWI, lakini unasikia kwenye maneno yao kuna mwelekeo wa uelewa kwamba kazi ya mfuko wa UKIMWI ni kwenda kuwalinda tu wale ambao wameambukizwa, lakini kumbe kuna Majimbo mawili hapa kwenye habari ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni asilimia 4.7 ambao wameshaambukizwa; hawa tunataka tuhakikishe maisha yao yanaendelea kuwa mazuri kiafya, kiuchumi na kijamii, lakini kuna asilimia 95 ambayo haijaambukizwa, hawa tuna kazi ya kuwalinda wasiambukizwe. Kwa hiyo, kuna hizi constituency zote mbili. Kwa hiyo, mtazamo wetu wa mapambano ya UKIMWI ni vizuri ukaenda kwenye Majimbo yote hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nilitaka nigusie Sheria ya UKIMWI kwa ufupi tu. Wamesema vizuri Mheshimiwa Waziri na unaona utashi wa kushughulika na hilo jambo la marekebisho, lakini niseme kwamba msingi wa kwa nini Kamati na sauti ya jamii inaomba marekebisho haya, misingi ni miwili mikubwa. Msingi wa kwanza ni takwimu kwamba maambukizi mapya ya UKIMWI kwa sasa kwa mujibu wa takwimu zetu wenyewe asilimia 40 iko kwa vijana wa miaka 15 mpaka 24 na miongoni mwa hao, asilimia 80 ni vijana wa kike. Kwa hiyo, huko ndiko maambukizi yapo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bila kujali kwamba kuna habari ya migongano ya sheria, wameolewa na nini, lakini ukweli ni kwamba asilimia kubwa ya maambukizi yako kwa vijana wa umri ule. Kwa hiyo, ni muhimu sana twende kutazama kule kuna nini? Kwa hiyo, huo ni msukumo wa kwanza wa marekebisho ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msukumo wa pili ni msukumo wa dunia kwa ujumla. Sasa hivi wanasema 90, 90, 90 na Tanzania pamoja na kazi nzuri ya kutoka preference ya asilimia 7.2 mpaka 4.7 sasa, lakini bado kwenye 90 ya kwanza hatufanyi vizuri, tuko asilimia 52. Kuna uwezekano ikafika 62 kwa sababu ya mambo ya kitakwimu yanafanyika, tutapara report hivi karibuni. Kwa hiyo, asilimia 52 bado haitoshi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, duniani huko watu wamechukua measure mbili kubwa; umri, kwamba watu wenye umri ambao maambukizi ni makubwa waingizwe kwenye kupima kwa hiari, lakini na self testing. Kwa hiyo, tuna misukumo miwili mikubwa ambayo ni muhimu tukaenda nayo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, misukumo hii inakuja na jambo lingine kwamba tuna kazi ya kuhakikisha kwamba Mfuko wa Taifa wa UKIMWI unaanza kusimama wenyewe. Ni kweli ni kazi ambayo haiwezi kukamilika ndani ya miaka michache lakini ni muhimu kazi hiyo ianze. Mfano, ni kwamba kuna taarifa zisizo rasmi lakini kwa bahati nzuri zitakuwa rasmi hivi karibuni; hivi tunavyozungumza wafadhili wanakwenda kupunguza asilimia 23 ya pesa ya UKIMWI inayokuja nchi hii kwa sababu yoyote ile, lakini ni kwamba zinakwenda kupungua. Kwa hiyo, huu ni msukumo ambao unatufanya tunahitaji Mfuko wa ATF upate tozo maalum uweze kusimama wenyewe, vinginevyo tutapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano hapa; duniani huko, kuna watu wanafanya endowment fund. Sasa hivi pesa yote ya UKIMWI inayokuja nchi hii, asilimia 60 inakwenda kununua supplies. Unavyosema supplies ni sindano, gloves, na kadhalika. Yaani vifaa vya kusaidia mapambano dhidi ya UKIMWI. Asilimia kubwa ya vifaa hivyo ni vile ambavyo tukiwekeza wenyewe vinaweza vikatengenezwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukitengeneza endowment fund, utashirikisha sekta binafsi, utatafuta hizo pesa za UKIMWI, zinatingia kwenye mfumo wa kiuchumi, kwa hiyo, zitajibu haja ya uchumi na haja ya masuala ya UKIMWI. Kwa hiyo, tunaomba tusisitize sana kwenye ATF na endowment fund ili tuweze kusimama wenyewe.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Utumishi; Mzee Mkuchika namwomba kwa dhati kabisa, Wizara hii ndiyo ina dhamana ya kusimamia Sheria ya UKIMWI mahali pa kazi. Kuna baadhi ya Wizara tumezungumza nazo, unaona kabisa kwamba mtazamo wa kwamba ni jukumu lao, upo mbali sana, wanadhani ni jukumu la TACAIDS. Kwa hiyo, hapa naoimba tuweke msukumo kwenye Wizara ya Utumishi kuzisimamia Wizara nyingine kwa kazi hiyo, lakini tuboreshe kitengo cha ndani ya TACAIDS ambacho kinapaswa kutazama hizo Wizar nyingine ili waweze kuwasimamia kwa nguvu zaidi.

Mheshimiwa Spika, Sera ya Madawa ya Kulevya ni muhimu sana. Sheria inafanya kazi vizuri, tumesikia mifano hapa, ni mfano Tanzania kwa maana ya utekelezaji wa sheria, lakini sheria ambayo inafanya kazi nje ya sera ni wazi itakuwa na upungufu. Tunaomba ile kasi iongezwe ili jambo hilo lifanyike mara moja halafu tumalizane nalo na kasi iwe kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako Tukufu likubali maazimio yetu kwamba ni maazimio ya Bunge ili baada ya hapa sasa Serikali ipate maelekezo ya kufanya kazi kwa kasi na nguvu zaidi kwa ajili ya kupiga hatua.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, naafiki.