Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nitoe mchango wangu katika hoja ambazo ziko Mezani.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuzipongeza sana Kamati zote ambazo zimewasilisha ripoti zao leo asubuhi. Napongeza ushirikiano mkubwa ambao Serikali inaendelea kutupa katika kufanya kazi yetu ya Uwakilishi hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia mambo machache tu kwa sababu na muda wenyewe ni mfupi sana. La kwanza nianzie hapa alipoishia rafiki yangu Mbunge wa kutoka kule Njombe, ambaye amemaliza kuongea, kwamba katika Wilaya yangu kule Mwanga kuna upungufu mkubwa sana wa Walimu. Leo asubuhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kijijini kwangu kule Kirongaya, ameniambia kuanzia Jumatatu ijayo kutakuwa na Walimu wawili tu katika Shule ya Msingi ya Kamwala ambayo ndiyo shule ya kijijini kwangu.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Mwanga Walimu watatu ndiyo wastani wa Walimu katika Shule za Msingi. Nimepiga kelele hapa kweli kweli, leo niongeze tena kelele hiyo. Nimemwandikia rafiki yangu Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri wa Utumishi, nimemweleza Waziri wa Elimu, nimemweleza Waziri wa TAMISEMI. Sielewi ni kwa sababu gani tatizo hili halijaweza kutatuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Walimu ambao wamepungua ni wale ambao wamestaafu; na kwa sababu hiyo mishahara yao ipo. Sasa inachukuaje mwaka mzima kutatua tatizo dogo namna hiyo wakati Walimu mtaani wako wamejaa tele na shuleni Walimu watoto wako wenyewe hawana Walimu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naendelea kuihimiza Serikali iliangalie jambo hili kwa huruma kabisa ili watoto wasiendelee kupoteza maisha yao wakiwa shuleni wanacheza peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nimeliona huku kwenye mitandao yetu kama Wabunge, kuna mjadala unaendelea, Waheshimiwa Wabunge wanajadili kwamba labda tubadilishe lugha ya kufundisha katika ngazi ya sekondari na ngazi ya Chuo Kikuu, tufundishe kwa Kiswahili. Ukiangalia matokea ya Mtihani wa Form IV wa mwaka 2018 haya yaliyotoka wiki iliyopita, utakuta tatizo kubwa kabisa katika shule zetu ni watoto kutojua Hesabu. Ukienda mbele, ukiangalia vizuri zaidi utakuta watoto wetu hohehahe kabisa katika Kiswahili chenyewe. Wanasema niletee ugari na wari, akuna shida badala ya hakuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watoto wetu wana shida kabisa katika ufahamu wa Kiingereza, anasema I will come yesterday. Watoto wana tatizo kubwa kabisa, ukienda utakuta watoto wetu wana matatizo makubwa sana katika sayansi; biolojia, fizikia na kemia. Sasa huko mbele Madaktari na Wachumi tutapata wapi? Kwa hiyo, tushughulikie tatizo lenyewe, tuwapeleke Walimu ambao wanafundisha masomo haya tuwajengee umahiri wa kufundisha masomo haya ya Hesabu, Kiswahili na Kiingereza sio kubadili lugha ya kufundishia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwapeleke Walimu tuwafundishe kwa sababu huko shuleni hawa watoto ambao wanasema I will come yesterday ndio wanapata degree, wanakwenda kufundisha English na wakiwa wanafundsiha wanafundisha hiyo hiyo I will come yesterday. Kwa hiyo, tufanye juhudi tuwafundishe Walimu wajenge umahiri katika masomo yao, ili tuweze kuacha Taifa ambalo litaweza kushindana katika uchumi wa dunia, litaweza kupambana katika masuala ya utafiti, litaweza kupambana katika kujenga nchi yetu, tusifanye mambo cosmetic yaani tusifanye vitu hivi kama vile mtu unaweka vipodozi mwilini, tusifanye mambo cosmetic. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tufundishe Walimu vizuri ili wapate umahiri wa kufundisha Kiingereza, Hesabu na Kiswahili na watoto waanze kujua zile KKK (Kusoma, Kuandika, Kuhesabu); wajue table na wabebe hata vile vijiti vya kuhesabia ili wajenge kabisa umahiri katika hesabu. Hakuna Taifa ambalo linaweza kuendelea watu hawajui hesabu, wamefika form four wanajua hesabu kwa asilimia 19, mambo magumu haya. Hili ni janga kabisa, kwa hiyo tulichukulie kwa nguvu inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda nirudie jambo ambalo nimelisema tena huko nyuma kwamba, watoto wanaokwenda kwenye vyuo vikuu wanahangaika sana na suala la mikopo. Katika mwezi huu uliopita wa Oktoba watoto wamefungua vyuo vikuu, nilikuwa kule Jimboni kwangu, nimeletewa watoto 15 ambao ni watoto yatima, wengine na mimi nafahamu ni watoto yatima, lakini hawakupewa mkopo. Sio kwamba lile baraza lina shida hapana, mikopo yenyewe haitoshi, kwa hiyo kuna watakaopata na wataokosa; wanafanya kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna siku moja nimekwenda pale, nimeongea na wale vijana wa Bodi ya Mikopo nimeona mazingira ambayo wanafanyia kazi. Serikali katika bajeti iliyopita ilitoa shilingi bilioni 500, jamani shilingi bilioni 500 sio kidogo, ni pesa nyingi sana. Kwa hiyo, Serikali ina dhamira thabiti kabisa ya kusaidia watoto wapate mikopo. Sasa sisi ndio lazima tuwe wabunifu, Serikali ikishatupa shilingi bilioni 500 tuwe wabunifu. Tusifanye mambo business as usual, tuwe wabunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepata bilioni 500, tumewapa watoto hao tuliowapa lakini pia mwaka kesho tutapewa tena labda bilioni 600 kwa sababu watoto wataongezeka, bilioni 700; hivi tunaweza, hatuwezi. Kwa hiyo, lazima tubadilishe gia, tuziambie benki zetu zitoe mikopo ili kila mwanafunzi wa chuo kikuu apate mkopo. Akishaingia chuo kikuu kama anataka mkopo apate mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali kazi yake kuangalia ile mikopo, benki zina…

SPIKA: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, ngoja nimalize kitu kimoja. Benki zinataka riba kiasi gani, Serikali ihangaike na riba na watoto wahangaike na mkopo wakati watakapomaliza shule zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)