Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Supplementary Questions
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka nenda, miaka rudi tofauti na kada nyingine za watumishi, kero imekuwa madeni ya walimu, madeni ya walimu. Leo hii mnatuambia kwamba madeni ya walimu yamefikia takribani shilingi bilioni 34 plus. Walimu hawa wanaidai Serikali wengine kama matibabu, likizo, kwa miaka zaidi ya mmoja hadi miwili. Walimu waliopandishwa mishahara miezi 12 iliyopita hadi leo hawajalipwa huo mshahara wanausikia harufu tu. Walimu wengine wamestaafu zaidi ya miezi sita hawajapata mafao yao.
Ningependa kujua kwa kuwa sasa hivi Serikali mnasema mmeshahakiki ni lini, na mnipe tarehe na mwezi hawa walimu watakuwa wamelipwa haya madeni kwa sababu wamechoka kila siku madeni ya walimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna walimu waliosimamia mitihani mwaka 2015. Leo hii tunazungumza mwaka 2017, kwa nini hadi leo hawajalipwa na ni lini Serikali itakuwa imewalipa hiyo stahili yao?
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na mikakati mizuri na mingi ya Serikali, lakini bei ya kahawa ya mkulima Mkoani Kagera bado ni Sh.1,000 kitu ambacho kinamuumiza mkulima. Kwa kuwa soko la kahawa linategemea soko la dunia, linategemea mauzo nje ya nchi, mahali ambapo mkulima wa kawaida au Vyama vyetu vya Ushirika hivi vya Msingi hawana uwezo wa kuyafikia hayo masoko. Pia kwa kuwa msimu unaofuata wa kahawa unaanza hivi keshokutwa mwezi wa Tano, ili makosa yasijirudie mkulima akaendelea kulipwa 1,000, je, Taasisi za Serikali ambazo zinahusika na utafutaji wa masoko wana mipango gani ya kwenda kule nje ya nchi wakawatafutia Watanzania masoko ikiwezekana wakaingia na mikataba na nchi hizo ili Watanzania wauze kahawa zao na waweze kupata bei nzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye baadhi ya super market huko China imeonekana kahawa ambayo inaonekana imetoka Uganda imekaangwa tu haijasindikwa zaidi ya hapo na ikawekwa kwenye kifungashio kizuri, robo kilo inauzwa kwa dola 40 ambayo ni zaidi ya Tanzanian Shillings 88,000 wakati sisi mkulima anapata 1,000 kwa kilo. Je, Wizara zinazohusika kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, wanawaandaaje Watanzania kwa maana ya wakulima na wafanya biashara wasindike kahawa badala tu ya wakulima kuuza zile zilizo ghafi kusudi Mtanzania aweze kupata bei nzuri na hasa hasa mkulima kutoka Mkoa wa Kagera?
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Bukoba Sekondari ina umri wa miaka 80, Rugambwa Sekondari ina umri wa miaka 55 lakini pamoja na uzee shule zote zilipitiwa na tetemeko na Bukoba Sekondari ikaja vilevile ikaezuliwa na kimbunga. Kwa niaba ya Mkoa wa Kagera na wanafunzi wanaosoma katika shule hizo, naipongeza sana Serikali kwa kutoa Sh.1,481,000,000 kwa ajili ya kukarabati Bukoba Sekondari na kuahidi kukarabati Rugambwa mwaka huu kuanzia mwezi huu wa Aprili. Kwa kuwa Rugambwa wakati wa tetemeko nyumba za walimu na zenyewe zilianguka na nyingine zikaathirika sana, hadi leo Mkuu wa Shule hana mahali pa kuishi, je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea nyumba za kuishi walimu wa Shule ya Sekondari Rugambwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, shule zote mbili, Bukoba Sekondari na Rugambwa zinahitaji kumbi za mikutano. Bukoba Sekondari haina ukumbi kabisa, Rugambwa ukumbi wake ni mdogo sana unachukua watoto 300 wakati wako wanafunzi karibu 700/800. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea kumbi za mikutano ili wanafunzi wapate mahali pa kufanyia mitihani na kufanyia mikutano?
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mto wa Kanoni kwa sasa umejaa sana mchanga na kina kimepungua sana, kwa watu wenyewe itakuwa si kazi rahisi kuondoa mchanga na zitahitajika fedha nyingi sana; pamoja na hatua zilizoainishwa kwenye jibu la swali ambazo ni za muda mrefu:-

Je, ni kwa nini Serikali isiwasaidie sasa hawa watu wanaohangaika na mafuriko kila mwaka kwa kutoa fedha kiasi za kuanza kusafisha mto huu angalau mara moja kwa mwaka?
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali mawili.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera ni mkoa mkubwa, una watu zaidi ya 3,000,000 lakini hadi leo hauna Chuo kikuu hata kimoja. Vipo vyuo vikuu vilikuwa vimeanzishwa na Mashirika ya Dini, moja ni Lutheran, walianzisha kile cha Joshua Kibira; Roman Catholic walianzisha branch ya Saint Augustine lakini vyote Serikali ilivifunga: Kwa kuwa Serikali inasema kuanzisha Vyuo Vikuu ni gharama, badala ya Serikali kuvifunga, haioni ingekuwa ni vizuri wakaendelea kuvijenga, kuvipa miongozo na kuviwezesha hivi vilivyoanzishwa badala ya kuvifunga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; miaka ya nyuma huko Mkoa wa Kagera ulikuwa unawika kwenye elimu, uko katika the best three, lakini sasa hivi haiko hivyo: Je, Serikali haioni kwamba sasa wakati umefika, angalau waanzishe tawi moja la Chuo Kikuu cha Serikali kama Sokoine, kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkoa wa Kagera ili kuchochea maendeleo ya Mkoa huo? (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Ufungaji wa Benki ya Wakulima ya Kagera iliyopo pale Manispaa ya Bukoba, iliwaumiza watu wengi ambao hawakuwa na hatia wakiwepo vikundi vya akinamama, SACCOS za akinamama, wakulima, wajasiriamali na hata wale wastaafu waliokuwa wameweka akiba zao. Serikali iliwalipa Sh.1,500,000/= pekee hata kama mtu alikuwa na akiba ya shilingi milioni 40. Sasa hivi anatuambia kwamba Serikali imekuwa ikikusanya madeni, pamoja na kuuza mali za Benki hiyo tangu mwaka 2018. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha hilo zoezi la kuwalipa hiyo Sh.1,500,000/= pamoja na akiba zote walizokuwa wameweka kwenye hiyo benki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa nini Serikali isione umuhimu sasa badala ya kuzifunga, ikaziunganisha hizi Benki ndogo ndogo, kama ilivyofanya ikaunganisha Benki ya Wanawake, Benki ya Posta, Benki ya Twiga, TIB wakatengeneza Tanzania Commercial Bank kwa hiyo, mtaji ukawa umeongezeka kuliko kungoja sasa hizi Benki wakazifilisi na wakawaumiza wananchi ambao wanakuwa wameweka akiba zao kwenye hizo Benki? (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Taarifa za Polisi na mambo tunayoyaona kila siku kwenye jamii yanaonesha kwamba ukatili wa kijinsia unaendelea kuongezeka; je, nini sababu ya ongezeko hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeweka mikakati mingi ya kudhibiti ukatili wa kijinsia ikiwemo Mabaraza ya Watoto, Madawati ya Jinsia, Kamati za Ulinzi, nani anaratibu afua hizi zote? Kwa nini basi tunapata taarifa tu kutoka kwenye Dawati la Polisi, lakini kwenye hizi afua mlizoweka hatupati taarifa zake? (Makofi)
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Hadi sasa maeneo mengi katika Mkoa wa Kagera ambayo yamesambaziwa umeme wa REA umeme umefika tu kwenye ngazi ya vijiji haukuteremka chini. Swali la kwanza, je, ni lini sasa madi wa ujazilizi densification itaweza kuanza Mkoani Kagera ili vijiji vyote sasa na maeneo yote yaliyorukwa na vitongoji yaweze kupatiwa umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika Mkoa wa Kagera kwenye Manispaa ya Bukoba tunazo Kata kama Kahororo, Buhembe, Nshambya, Nyanga, Kagondo, Kibeta, Kitendaguro na Ijuganyondo ambavyo pamoja na kwamba kata hizo ziko kwenye Manispaa ya Bukoba lakini zimekaa kama vijiji. Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha mradi wa Peri- Urban ili sasa vijiji hivi au mitaa hii inayofanana na vijiji iweze kupata umeme wa REA kwa bei nafuu?
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mkoani Kagera kilimo cha vanila kilianza kwenye miaka ya tisini lakini hadi leo hakuna mfumo unaoeleweka wa kilimo cha vanila nchini. Je, ni lini Serikali sasa italeta mwongozo juu ya namna ya kulima, wakatoa huduma za ugani na wakaelekeza juu ya masoko?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa huko ulimwenguni katika nchi nyingine kilo ya vanilla inanunuliwa kati ya 800,000 mpaka 1,000,000 wakati mkulima wa Kagera anauza vanilla kwa 20,000, 15,000 mpaka 30,000 tu. Je, ni lini sasa Serikali kwa kutumia balozi zetu za nje wataweza kututafutia masoko yanayoeleweka ili kuweza kumnufaisha huyu mkulima kupata bei nzuri ya vanilla?
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Bukoba Government Referral Hospital haijafikia hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Hata Mheshimiwa Waziri wa Afya alisimama hapa na yeye mwenyewe akakiri kwamba ile hospitali bado haijafikia ile hadhi, na mkatuahidi kwamba mtatuletea fedha kusudi tuweze kujenga hospitali nyingine au kukarabati ile ifikie hadhi hiyo: Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha kuweza kutuhakikishia kwamba wanatujengea hospitali yenye hadhi ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mkoa wa Kagera uko mpakani na unapakana na nchi kadhaa. Kwa hiyo, yakitokea magonjwa ya mlipuko ni rahisi kuingia Mkoa wa Kagera kwa sababu magonjwa hayana mipaka. Kwa kuwa juzi juzi uliingia mgonjwa mbaya sana wa Marburg na mkaona Wizara na Mkoa walivyokuwa wanahangaika kutafuta mahali pa kuweka wale watu waliokuwa wamechangamana na wagonjwa, kwa sababu hakuna isolation centers ikabidi wawaweke mpaka kwenye mahoteli na hayo mahoteli yakafungwa yakawa hayatoi huduma kwa wakati huo: Je, ni lini sasa Serikali itaujengea Mkoa wa Kagera Isolation center? (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa duniani kwa sasa, watu zaidi ya 28 wanakufa kila sekunde kwa sababu ya magonjwa yasiyoambukiza na kwa sababu Tanzania kwa sasa kisababishi kikubwa cha vifo Tanzania ni magonjwa yasiyoambukiza. Kwa nini Serikali isitoe fedha za kutosha ili wananchi waweze kupata elimu, wajue visababishi, wajue na namna ya kujikinga kwa sababu haya magonjwa yanaweza kuzuilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku ni zao la biashara ndani ya Tanzania, lakini tumbaku hiyo hiyo ni kisababishi kikubwa kinacholeta magonjwa yasiyoambukiza kama kansa, stroke, presha na kisukari. Je, ni lini Serikali itawawezesha wakulima wa tumbaku nchini ikawapa mazao mbadala, wakawatafutia na masoko ili kusudi waondokane na hiki kilimo ambacho kinaathiri afya zao? (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa wa Kagera una maambukizi makubwa ya Malaria, ni namba tatu kwa maambukizi makubwa Kitaifa na kwa kuwa Wilaya ya Ngara ndiyo inayoongoza katika maambukizi ya Malaria Mkoani Kagera. Je, ni lini sasa Serikali itatusaidia kufanya unyunyiziaji wa viuatilifu (Indoor Residual Spraying) katika Wilaya ya Ngara ili kupunguza maambukizi ya Malaria?

Swali la pili, kwa kuwa zipo nchi duniani ambazo tayari zimeshatokomeza kabisa Malaria. Je, ni lini Tanzania tumelenga ni mwaka gani tutakuwa tumefikia zero Malaria, kwa maana ya kutokomeza kabisa Malaria? (Makofi)
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mafuriko katika Mto wa Kanoni ulio katika Manispaa ya Bukoba umewatesa watu kwa miaka mingi na sasa hivi naishukuru Serikali kwa kuweza kukubaliana na ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na sasa wanauingiza mto huu katika mradi wa TACTIC.

Je, kuna mvua za vuli zitaanza mwaka huu za mwezi Oktoba mpaka Januari; Serikali inaweza ikaongezea fedha kiasi kwenye ile milioni sita inayotengwa na Halmashauri ili kusudi angalau wakafanya ukarabati wa awali isije ikatokea tena mafuriko mwaka huu?

Swali la pili; ili kuweza kuondoa mafuriko kabisa katika mto huu, inabidi mto upanuliwe, kina kiongezwe, kuta zijengwe za mto huu kutoka kwenye Kata ya Kagondo, Rwamishenye, Amgembe, Gireye, Bakoba hadi kuingia kwenye Ziwa Victoria. Je, katika huu mradi unaokuja wa TACTIC haya maeneo yote yatazingatiwa?
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mashine za EFD ni za gharama sana lakini mtu akibadilisha biashara kwa maana ya TIN analazimika kununua mashine mpya. Kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa badala ya kununua mashine mpya wakaondoa ile program akaendelea kutumia mashine ile ile kwa kubadilisha tu program? (Makofi)

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's