Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itamaliza kazi ya kuwapatia wananchi Vitambulisho vya Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, kwa miaka 14 tangu NIDA ianze kazi, pale Sikonge waliopatiwa vitambulisho ni watu 61,000 tu kati 91,000 ambao walipigwa picha, maana yake ni kwamba kuna watu 30,000 hawajapatiwa vitambulisho, sasa nina maswali mawili ya nyogeza.

Je, Serikali ina mkakati gani katika kipindi cha miezi sita itawapatia vitambulisho watu wengi hivyo 30,000, wakati wastani kwa mwaka imekuwa ni 4,300? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa bado tuna watu karibu 60,000 hawajapigwa hata picha na siku hizi kuna masharti, ukienda leseni unaambiwa sharti la NIDA na huduma nyingine.

Je, kwanini Serikali haioni umuhimu wa kuahirisha hayo masharti mengine ili wananchi wasiendelee kudaiwa kitambulisho cha NIDA wakati haiwezekani kupata? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, kuhusu swali la kwanza, uhakika ndani ya miezi sita kwamba tutakamilisha upatikanaji wa vitambulisho kwa wananchi ambao hawajapata, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kwamba katika utekelezaji wa shughuli za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nadhani Wabunge wote mnafahamu kwamba kwa miaka karibu mitatu hadi minne, mkataba ulikuwa umekuwa frustrated kwa sababu mkandarasi alikuwa anadai muda mrefu na madai yake yalikuwa hayajalipwa. Kwa dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tatizo lile amelikwamua, ametoa fedha tukalipa madeni tuliyokuwa tunadaiwa na uzalishaji wa vitambulisho umeanza.

Mheshimiwa Spika, tulichofanya kama Wizara ni kumsisitiza mkandarasi, kwa sababu kuna wananchi wengi walikuwa wanasubiri vitambulisho hivi, awe na mpango wa kasi wa kuzalisha na namshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani aliniruhusu nikaenda mpaka kwenye kiwanda, nimejiridhisha kuwa uzalishaji unaenda kwa kasi kubwa. Ndiyo maana tuna uhakika kwamba ifikapo Machi, wananchi wote ambao walikuwa hawajapata vitambulisho watapata vitambulisho hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; nimwondoe mashaka Mheshimiwa Mbunge. Tumeanza kuimarisha utendaji wa NIDA. Baada ya uzalishaji wa vitambulisho kuanza, NIDA imepanua uwezo wake kwa kuazima staff kutoka kwenye vyombo vyetu vingine vya usalama ili kuongeza kasi ya kuwafikiwa wananchi, waweze kupata zile namba za utambulisho.

Kwa hiyo, badala ya kusitisha zoezi zile, ngoja liendelee lakini tutaongeza idadi ya watu ili wananchi wako wa Sikonge ambao hawajapigwa picha na kupewa namba za utambulisho waweze kufanyiwa hivyo, nashukuru. (Makofi)